Watu wasiopungua watano wameuawa jana usiku nchini Burundi ambapo imearifiwa kuwa mapigano yamejiri karibu na ofisi ya rais katika mji mkuu Bujumbura.
Wakaazi wa mtaa wa Rohero karibu na ofisi ya rais wamesema walisikia milio ya risasi usiku wa kuamkia leo. Maafisa wa serikali na polisi hawajatoa taarifa yoyote na pia vyombo rasmi vya habari vya serikali havijaripoti kutokea mapigano yoyote karibu na ofisi ya rais.
Hata hivyo Meya wa Bujumbura Freddy Mbonimpa amethibitisha kuuawa watu wanne mjini Bujumbura na kwamba maafisa wawili wa polisi wamejeruhiwa na watu wengine 28 wamekamatwa. Wakaazi wa Bujumbura wanasema limekuwa jambo la kawaida kusikia milio ya risasi na maguruneti mjini humo.
Mgogoro wa kisiasa nchini Burundi ulianza mwezi Aprili mwaka huu baada ya chama tawala cha nchi hiyo cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu mfululizo.
Nkurunziza ameshagombea na kushinda uchaguzi wa rais na huku wapinzani nchini humo wakisema hatua hiyo ilikwenda kinyume na katiba ya nchi pamoja na makubaliano ya Arusha, Tanzania.
0 comments:
Post a Comment