Wednesday, November 26, 2014

MBUNGE FELIX MKOSAMALI AFIKISHWA MAHAKAMANI

MBUNGE wa jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo mkoani Kigoma kupitia chama cha NCCR Mageuzi Felix Mkosamali amefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Kibondo akituhumiwa kumzuia  karani mwandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa na vijiji kufanya kazi yake.
Mh.Mkosamali ambaye alilala rumande baada ya kukamatwa na polisi Jumatatu jioni amefikishwa mbele ya hakimu wa wilaya  ya Kibondo Erick Maley na kusomewa shitaka lake na mwendesha mashtaka wa jeshi la polisi Peter Makala.
Ilidaiwa kuwa Mkosamali alimzuia karani  mwandikishaji wapiga kura Kadiri Hamidu katika kituo cha Nduta katika kitongoji cha Nduta kijiji cha Kumuhasha kata ya Murungu wilayani Kibondo kuendelea na zoezi la kuandikisha wapiga kura baada ya kuchukua vitabu na karatasi alizokuwa akiandikia kinyume cha sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa na vijiji.
Baada ya kusomewa shitaka hilo, mh.Felix Mkosamali alikana na ameachiwa kwa dhamana hadi Disemba 29 kesi yake itakapotajwa tena.
Tukio hilo liliilazimu jeshi la polisi wilayani kibondo kuimarisha ulinzi katika eneo la mahakama kutokana na idadi kubwa ya watu waliofika kushuhudia ambapo baadhi yao wameshauri viongozi kushirikiana ili uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Disemba 14 uende vizuri

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI