Monday, August 17, 2015

WATAALAM WA TEHAMA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA MAADILI, WELEDI NA UBUNIFU

Naibu Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.HAB Mkwizu akifungua mkutano wa kwanza wa mwaka wa Serikali Mtandao leo jijini Arusha.Zaidi ya wataalam wa TEHAMA 500 kutoka Wizara, Idara, Wakala,Taasisi, Halmashauri wako jijini Arusha kujadili mafanikio na changamoto za Serikali mtandao.
********
Na Aron Msigwa
Serikali imewataka watalaam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) walio katika utumishi wa umma kote nchini kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili, weledi na ubunifu ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za serikali kwa njia ya mtandao  katika maeneo mbalimbali na kuondoa malalamiko yanayotokana na utoaji wa huduma   usiokidhi viwango.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Arusha na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.HAB Mkwizu wakati akifungua Mkutano wa kwanza wa mwaka wa Serikali mtandao wa Maofisa TEHAMA kutoka Wizara, Idara,Wakala na Taasisi mbalimbali za Serikali.
Amesema Watumishi wa umma wasipotimiza wajibu wao kikamilifu wanasababisha malalamiko kwa wananchi na kuifanya Serikali kushindwa kufikia malengo iliyojiwekea.

"Ni muhimu wote mtamtambue kuwa utumishi wa umma imara hujenga serikali na Taifa imara, utumishi wa kufanya kazi kwa mazoea na kusukumwa  hauna tija kwa taifa letu" Amesema.

Ameongeza kuwa ili kufikia malengo ya kuimarisha utawala bora na kuongeza tija na ufanisi Serikali imekuwa ikisisitiza matumizi ya TEHAMA ili kuimarisha mawasiliano ya haraka, yenye uhakika na salama ndani ya taasisi mbalimbali za Serikali; kuanzia kwenye Wizara, Mikoa hadi ngazi za Halmashauri pamoja na Balozi mbalimbali nje ya nchi.

 Amefafanua kuwa katika  kupanua wigo wa upatikanaji wa taarifa muhimu na kuimarisha usalama wa Serikali na raia wake Serikali imeendelea kujenga na kuongeza uwezo wa kupambana na majanga kwa kutumia teknolojia.

Aidha, amesema   Serikali kwa kutambua mchango wa TEHAMA inaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zikiwemo za baadhi ya mifumo  kutokuongea, kutowasiliana na kutobadilishana taarifa kati ya taasisi na taasisi pia rudufu ya mifumo ambapo kila taasisi inakuwa na juhudi za kipekee katika kusimika na kutumia miundombinu ya TEHAMA ambayo ingeweza kutumiwa na zaidi ya taasisi moja pamoja na changamoto ya mifumo kuwa na viwango vya usimikaji tofauti.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt.Jabiri Bakari akitoa ufafanuzi kuhusu Serikali Mtandao kwa washiriki wa Mkutano wa kwanza wa Serikali Mtandao unaofanyika katika ukumbi wa AICC jijini Arusha leo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt.Jabiri Bakari akizungumza na waandishi wa habari
Mtaalam wa masuala ya Serikali Mtandao kutoka nchini Singapore Bw.Tan Kim akiwasilisha mada kuhusu Umuhimu wa Serikali mtandao kwa washiriki wa Mkutano wa kwanza wa Serikali mtandao unaofanyika jijini Arusha leo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao ( e Government Agency) Dkt. Jabiri Bakari awali akiwakaribisha Wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano waliohudhuria Kongamano hilo amesema  kuwa katika kuimarisha uwazi na upatikanaji wa Takwimu huria, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya TEHAMA  ili  kuwawezesha wananchi kupata huduma zinazotolewa na Wizara na Taasisi kwa njia ya mtandao.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya vizuri katika kufanikisha lengo kubwa la kufikisha huduma kwa wananchi na kuongeza kuwa mpango wa  Serikali uliopo sasa ni kuwa na mfumo mmoja utakaowezesha taarifa zote za wananchi kuwa katika sehemu moja.

 Akizungumza kuhusu mkutano huo  Dkt.Jabiri amesema kuwa washiriki zaidi ya 500 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali watapata fursa ya kujadili  masuala mbalimbali ya ushirikiano katika kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao nchini pamoja na Kutafuta ufumbuzi wa changamoto za serikali mtandao zilizopo nchini ili kuleta  maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, wataalam wa TEHAMA wa Tanzania waliohudhuria kongamano hilo watapata fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalam wengine wanaohusika na Serikali Mtandao kutoka nchi zinazofanya vizuri katika eneo la Serikali mtandao zikiwemo India na Singapore.

 Ameongeza kuwa katika mkutano huo mada mbalimbali zitajadiliwa zikijikita  katika usimamizi wa Serikali Mtandao nchini Tanzania, Hali ya miundombinu  ya Serikali mtandao na Utekelezaji wa Mpango wa Uendeshaji wa Serikali kwa uwazi.

Mada nyingine zitahusu uimarishaji wa uwazi na Mfumo wa Takwimu huria nchini Tanzania na uimarishaji wa huduma za Serikali kupitia simu za mkononi na mifumo inayotumika kutoa huduma kwa wananchi.
Wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kutoka maeneo mbalimbali nchini wakifuatilia Masuala mbalimbali wakati wa mkutano wa kwanza wa mwaka wa Serikali mtandao unaofanyika jijini Dar es salaam.


Naye Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha Bw.Agostin Mapunda akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Arusha amesema kuwa Matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Serikali yamerahisisha utendaji wa kazi na kuboresha maisha ya wananchi.

Amesema sasa wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali zikiwemo za upataji wa hati za ardhi kwa haraka zaidi kupitia mifumo ya TEHAMA iliyoanzishwa na serikali.

Ameongeza kuwa ni vema mabadiliko hayo yakaendelezwa kutokana na umuhimu wake katika kufanikisha utendaji wa Serikali, kupunguza muda na kuokoa gharama!

"Tuko kwenye njia sahihi ya kuufanya utendaji wa Serikali kupata mafanikio kupitia mtandao, hali hii tunaona imepunguza matumizi na gharama kubwa waliyokuwa wanaipata wananchi kufuata huduma ambazo sasa zimerahisishwa kupitia mtandao"

Amefafanua kuwa wananchi sasa wanaweza kulipia ankara zao za umeme, maji na huduma nyingine kupitia simu zao za mkononi jambo ambalo hapo awali halikuwepo.
#MAELEZO

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI