Saturday, April 5, 2014

KUELEKEA KUMBUKUMBU YA 'KARUME DAY' TUJIKUMBUSHE KILICHOPELEKEA KIFO CHAKE

Miaka 42 iliyopita, Aprili 7, 1972; Rais wa Serikali ya awamu ya kwanza ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abeid Amani Karume, aliuawa kwa kupigwa risasi katika mazingira na sababu za kutatanisha.
Risasi nane zilitolewa mwilini kwake mwili wake ulipofikishwa kwenye Hospitali ya V. I. Lemin, mjini Unguja kwa uchunguzi, sawa na idadi ya miaka minane ya utawala wake tangu 1964 hadi kifo chake.
Ilikuwa hivi:  Rais Karume na Makomredi wenzake wa Chama cha Afro-Shirazi (ASP) alikuwa na mazoea ya kucheza karata, damma au dhumuna kwenye ukumbi wa ofisi za makao makuu ya Chama hicho Kisiwandui, kila jioni kama sehemu ya mapumziko.  Siku hiyo alifika saa 11.00 jioni akiwa na walinzi wake, akaingia ndani nao wakabaki nje kulinda.
Ikafika zamu yake kucheza; akawa anacheza na Mzee Maalim Shaha Kombo ambaye alionekana kulemewa.  Ndipo Karume akamwita Mzee Mtoro Rehani ajitayarishe baada ya Kombo, naye akaitikia kwa kuaga kwanza aende msalani kujisaidia.
Sekunde chache baada ya hapo na kabla Mzee Mtoro Rehani hajarejea kutoka msalani, ghafla watu wawili wenye silaha walivamia chumba alimokuwa Karume na wenzake na kumimina risasi wakimlenga; na kufumba na kufumbua, akawa katika dimbwi la damu kimya, amepoteza uhai.  Hakuna mtu mwingine aliyeuawa mbali na kujeruhiwa tu, mmoja wao akiwa Katibu Mkuu wa ASP, (sasa) Hayati Thabit Kombo Jecha.
Risasi uaji (the fatal bullet), mbali ya risasi zote, iliyochukua uhai wa Karume ilitoka kwenye bunduki ya Luteni Hamoud Mohammed  Hamoud wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT), ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa uvamizi huu na aliyefyatua risasi ya kwanza wakati Karume akicheza na wenzake.  Inasemekana, Hamoud aliuawa papo hapo na mlinzi wa Karume.
Wauaji wengine waliofuatana na Hamoud katika uvamizi huo ni Kapteni Ahmada Mohamed, Koplo mmoja wa jeshi ambaye jina lake halijafahamika hadi leo, na raia mmoja aliyekwenda kwa jina la Ali Khatibu Chwaya, ambao inaelezwa wote hao waliuawa kwenye mapambano ya silaha nje ya eneo la tukio.
Dakika chache baada ya mauaji kutokea, alifika Kanali Ali Mahfoudhi na askari mwingine, Kapteni Makame Hamis, wakauchukua mwili wa Karume na kuukimbiza hospitali.
Itakumbukwa, Kanali Mahfoudhi ni mmoja wa vijana wa Umma Party (UP) cha Abdulrahman Mohamed Babu, kilichoungana na ASP baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na kuunda Serikali ya mseto. Ni kati ya vijana waliopelekwa Cuba kwa mafunzo ya kijeshi, na ni mmoja wa wapiganaji walioendesha mapambano ya kisayansi usiku wa Mapinduzi na kukamata uwanja wa ndege mchana Aprili, 1972.
Ni mmoja wa wanaharakati wa siasa za mrengo wa Kikomunisti ambao hawakutakiwa Zanzibar wakati wa utawala wa Karume, hivi kwamba kufuatia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, 1964, Karume alishinikiza kwa Nyerere wapewe kazi Tanzania Bara aweze “kupumua” ambapo Mahfoudhi alipewa cheo cha Mkurugenzi wa Operesheni katika JWT.
Wengine ambao hawakutakiwa ni pamoja na Babu mwenyewe aliyepewa Uwaziri wa Mipango ya Uchumi, na kama tulivyoona makala zilizopita, hasimu mwingine wa Karume, Othman Sharrif, ambaye alifanywa Afisa Mifugo wa Mkoa, Mtwara au Mbeya, na Balozi Salim Ahmed Salim wakati huo Balozi wa Zanzibar nchini Misri ikaridhiwa aendelee kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano nchini humo.
Tuache hayo, lakini hapa swali linazuka:  Kwa kuwa Kanali Mahfoudh hakuwa kipenzi cha utawala wa Karume tangu mwaka 1964, ilikuwaje akawa Afisa wa kwanza kuwa kwenye tukio kabla ya maafisa wengine vipenzi, kama vile Kanali Seif Bakari ambaye alikuwa pia Mkuu wa Usalama wa Taifa Zanzibar ambalo halikuwa jambo la Muungano, na wengineo?
Je, alikuwa katika ziara ya kikazi wakati mkasa huu ukitokea au alijua kilichotarajiwa kutokea? Kwa nini alikuwa mmoja wa washitakiwa zaidi ya 100 kwa tuhuma za mauaji hayo, na mmoja wa watuhumiwa 18 miongoni mwa hao walioshitakiwa wakiwa Tanzania Bara, Abdulrahman Babu akiwa mmoja wao.
Kuna dhana mbili kinzani kuhusu jinsi Karume alivyouawa na hatima ya wauaji. Dhana moja inadai kwamba, watu wanne walivamia mahali alipokuwa Karume na wenzake, wakamimina risasi mara nne au mara tano hivi, risasi ya kifo ikampata Karume shingoni akafa, huku zingine zikiendelea kumiminwa kulenga meza walipokuwa.
Inadaiwa kuwa Hamoud aliuawa kwenye eneo la tukio, ambapo wawili waliuawa baadaye na vyombo vya usalama (kwa mapambano?) na mmoja alijiua.Dhana ya pili inadai kwamba Hamoud alikufa kwenye eneo la tukio katika mazingira ya kutatanisha, ama kwa kujipiga risasi kuepuka kukamatwa hai na kuteswa baada ya kuona asingeweza kutoroka; au alijeruhiwa vibaya na walinzi wa Karume, kisha Ahmada akampiga risasi na kumuua kumwepusha kuteswa na kutoa siri kama angekamatwa hai, kisha (Ahmada) akaweza kutoroka kwenye eneo la tukio. 
Juu ya utata huu kuhusu hatima ya wauaji, ni ukweli kwamba ni Luteni Hamoud pekee aliyeuawa kwenye eneo la tukio na washiriki wengine katika mauaji waliweza kutoroka eneo la tukio na baadaye kuuawa katika mazingira yasiyofahamika.
Kufuatia mauaji hayo, watu 1,100 walikamatwa na kuhojiwa juu ya kuhusika au kutohusika kwao na mauaji, wengi wakiwa viongozi na wanachama wa zamani wa Umma Party, chama cha Babu na wanachama mashuhuri wa ASP wenye siasa za mrengo wa kikomunisti.
Yote haya yanaturejesha kwenye swali letu la awali:  je, kuuawa kwa Karume kulikuwa na lengo la kulipiza kisasi kwa chuki binafsi, kama baadhi ya watu wanavyodai, au lilikuwa jaribio la Mapinduzi lililoshindwa kwa Serikali ya Mapinduzi? Ni nani huyu Luteni Hamoud Hamoud aliyeongoza mauaji na kwa nini?
Je, lengo lilikuwa ni mauaji hayo pekee au kulikuwa na mpango mkubwa zaidi nyuma? Ukiongozwa na nani?
Kupata majibu ya maswali haya, hatuna budi kuiangalia hali ya kisiasa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na baada ya Muungano na Tanganyika, Aprili 26, 1964.
Kama nilivyoeleza katika mfululizo wa makala nne hivi karibuni katika gazeti hili kuhusu jinsi “Field Marshal” John Okello alivyoongoza Mapinduzi ya 1964, na kuundwa kwa Serikali ya Mseto kati ya vyama vya ASP na Umma, lengo kuu la Karume lilikuwa ni kuzivunja nguvu za wanaharakati wa Umma Party na za wakomunisti wa ASP walioshabihiana kimawazo na kimtazamo wa kitaifa na wana-Umma Party na kumnyima Karume usingizi.
Lakini tofauti na matarajio ya Karume, hatua hiyo iliwaleta karibu zaidi wanamapinduzi hao na kumnyima zaidi usingizi kwa hofu ya kupinduliwa, wakimtuhumu kushindwa kuongoza na kusimamia madhumuni ya Mapinduzi Visiwani.
Mungu bariki kwa Karume, ukatokea Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika mwaka huo, akaona vyema awasambaratishe kwa kuwatafutia nafasi Tanzania Bara ambako wasingeweza kufurukuta.
Waliokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na Abdulrahman Babu (Umma) na aliyepewa Uwaziri wa Mipango na Uchumi kwenye Serikali ya Muungano; Kassim Hanga (ASP) aliyeteuliwa Waziri katika Ofisi ya Rais wa Jamhuri, Mambo ya Muungano; Salim Ahmed Salim (Umma) aliyeteuliwa Balozi nchini Misri.
Wengine ni Othman Sharrif (ASP) aliyeteuliwa Balozi nchini Marekani, lakini Karume akampinga Nyerere akidai hastahili, uteuzi ukafutwa; badala yake akateuliwa kuwa afisa mifugo katika moja ya mikoa ya Kusini Tanzania, Mbeya au Mtwara, na Kanali Ali Mahfoudh (Umma) aliyeteuliwa Mkurugenzi wa Operesheni katika Jeshi la Wananchi (JWT), na wengineo.
Kwa wale wenye maoni tofauti na ya kukosoa Serikali waliobaki Visiwani, hasira ya Karume aliyetawala kwa mkono wa damu iliwashukia, wengi walikamatwa na kutiwa kizuizini na pengine kupoteza au kuuwawa kikatili na katika mazingira ya kutatanisha. Mmoja ya waliouawa kikatili kizuizini ni Mzee (mwanaharakati) Mohamed Hamoud, baba yake Luteni Hamoud Mohamed muuaji wa Karume.
Tangu Mapinduzi ya Januari 12, 1964, Zanzibar haikuwa na Katiba wala Sheria; iliongozwa kwa Amri za Rais  (Presidential Decrees) kadri alivyoona inafaa.  Na kwa mujibu wa Gazeti la “The Tanganyika Standard” la March 9, 1968, Karume aliapa kutofanya uchaguzi wala kuwa na Katiba Kisiwani kwa miaka 50 tangu 1964 – 2014 Kwa madai kwamba  “chaguzi zote ni vyombo vya mabeberu kuwakandamiza wananchi”.
Na kadiri kalamu ya Karume ya wino wa damu ilipozidi kuandika historia ya ukatili, udikteta na umwagaji damu kwenye kurasa ngumu za kukwaruza ndivyo alivyojichongea na kujiongezea upinzani na uadui kwa jamii ya Kizanzibari.
Kufikia mwaka 1967 hofu ya Karume dhidi ya wenzake na kwa nafasi yake ilitia fora kiasi cha kuogopa kivuli chake mwenyewe. Na ili kuendelea kuwamaliza wenzake, mwaka huo zilitungwa tuhuma za uongo dhidi ya watu 14 makada wa ASP katika kumpindua, zikiwalenga hasa wenye fikra za kikomunisti.
Walioingizwa kwenye tuhuma hizo ni pamoja na mawaziri wa Serikali yake mabwana Abdallah Kassim Hanga, Salehe Saadallah Akida, Abdul Aziz Twala na makatibu wakuu wa wizara, Aboud Nadhif na Mdungi Ussi na baadaye Othman Sharrif.
Wote waliokuwa Visiwani walikamatwa, kisha Karume akamwomba Nyerere kuwarejesha Zanzibar kutoka Bara, Othman Sharrif na Hanga ili “wakahojiwe” lakini wote wakaishia kuuawa kikatili bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mmoja wa mashahidi wa uongo walioandaliwa dhidi ya “watuhumiwa” kwa vyombo vya Karume, alikuwa Ahmada ambaye kwa uongo wake, watu wanne akiwamo Hanga, Twala, Saadallah na Othman, walinyongwa mwaka 1969.  Kwa uongo huo, Ahmada alizawadiwa cheo cha kapteni jeshini.  Ni Kapteni Ahmada huyu, aliyeshiriki kwenye mauaji ya Karume miaka mitatu baadaye.
Kwa hofu ya jamii ya Kizanzibari kufikiwa na fikra na mawazo mapya ya kimaendeleo, Karume alipiga marufuku vijana wa Kizanzibari kwenda nje kwa masomo ya juu ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam; alipiga marufuku pia ujenzi wa Chuo Kikuu Visiwani.
Mbali na kutokuwapo kwa utawala wa sheria enzi za Karume, unyanyasaji wa kijinsia na ubaguzi kwa misingi ya historia na kisiasa ulitia fora. Kwa mfano, mwaka 1966, alitoa amri (decree) kuwanyima wazazi haki ya kuwakataa wanaume walioposa binti zao kama njia ya kuondoa ubaguzi wa rangi.
Kwa sababu hii, wasichana, hasa wale wa Kiarabu walilazimishwa kwa nguvu ya Serikali kuolewa kwa nguvu. Karume mwenyewe, wakati huo akiwa na umri wa miaka 65, aliwania kuoa kwa nguvu, wasichana wanne wa Kiajemi, na alipokataliwa, aliamrisha wazazi wao watiwe kizuizini na kuchapwa viboko kwa kosa la kuzuia mpango wa ndoa mchanganyiko, na baadaye kutimuliwa Zanzibar.
Chini ya mpango huo, raia wa kigeni waliotaka kuchumbia wasichana wa Kizanzibari walitakiwa kuilipa Serikali Sh. 64,000,000, bila hivyo hawakuruhusiwa kuwaoa.
Karume alikuwa ameanza kuwa mwiba kwa Mwalimu Nyerere pia juu ya Muungano. Kwa mfano, alimkatalia Nyerere kwa lugha ya dharau na kejeli juu ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha kutumika Zanzibar.
Na kuhusu akiba ya fedha za kigeni ya Zanzibar iliyofikia dola milioni 80 mwaka 1972, alimuonya asithubutu kuitolea macho, akamwambia:  “Fedha ya kichwa cha Malkia si yako na usiniulize, labda niulize juu ya hii (sh.) yenye picha ya kichwa chako”.
Na kuhusu Muungano, Karume alikuwa ameanza kuchoka nao. Siku moja alisema, “Muungano ni kama koti tu; likikubana unalivua”.
Ufa huu kati ya viongozi hao wawili juu ya Muungano, ndio uliosababisha kamati ya kupendekeza Katiba (Constitutional Committee) isiundwe na Bunge la Katiba (Constitutional assembly) lisiteuliwe ndani ya muda wa mwaka mmoja tangu Muungano, kama ilivyotakiwa chini ya Mkataba wa Muungano wa Sheria ya Muungano ya 1964.
Wadadisi wa mambo ya siasa wanakubaliana kuwa, kama Karume angeendelea kutawala miaka kadhaa baada ya 1972, Muungano ungefikia kikomo kwa njia ya kutisha na kusikitisha.
Kufikia mwaka 1972, upinzani kwa Serikali ya Karume ulikuwa umechukua harakati za uasi wa umma, chini kwa chini kwa mara ya kwanza tangu Hanga na wenzake wanyongwe mwaka 1969.
Kwa kifupi, tuliona kwamba, kwa vigezo vyovyote vile vya utawala na uongozi, Karume alitawala kwa mkono wa chuma; alitawala kidikteta katika nyanja zote za maisha ya Wazanzibari kisiasa, kiuchumi na kijamii.   Alikuwa kero pia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kwa Muungano.KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya toleo lililopita, tuliona jinsi Rais wa Serikali ya awamu ya kwanza Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Abeid Amani Karume, alivyouawa kikatili na wanajeshi wakati akicheza bao, Aprili 7, 1972 mjini Unguja.
Kwa kusema haya sina maana kwamba Karume hakutenda mema kwa Zanzibar na kwa Wazanzibari; bali najaribu kutafiti tu kuona ni mazingira na sababu zipi zilizochochea na kuharakisha kuuawa kwake; kati ya sababu hizi kuu za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimuungano.  Kwa vyovyote vile, moja au zaidi ya mambo haya manne yalichangia.
Tunajua kwa mfano, kwa baadhi ya Wazanzibari, Karume alikuwa mtawala mkatili asiye na huruma wala hakujua kusamehe; lakini pia alikuwa na sifa za pekee nzuri kama kiongozi na binadamu; alikuwa mhimili na mtetezi wa Waafrika wa Kizanzibari na hakuyumbishwa na siasa za migogoro Visiwani.
Alikuwa mwenye fikra zenye kujitegemea, alifanya maamuzi yake bila woga wala kuhofia matokeo; alikuwa kiongozi mwenye kuthubutu na mwenye kujituma.
Mwisho tutaona jinsi mpango mzima wa mauaji ulivyoandaliwa kwa wasomaji kuona kama ilikuwa chuki binafsi au mapinduzi.  Si madhumuni ya makala haya kumwona Karume kama dikteta mwema (benevolent dictator) au dikteta katili (ruthless tyrant), maana hilo ni jambo la maoni ya kila mtu binafsi.
Alitawala kwa mkono wa chuma
Tumeona jinsi Karume alivyoitawala Zanzibar kwa mkono wa chuma, na namna alivyowaengua wote aliodhani hawakuwa upande wake, ama kwa kuwahamishia kwenye Serikali ya Muungano, ama kwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Sambamba na hatua hiyo, jamii ya Kiarabu wasio Wazanzibari, iliamriwa kuondoka, na wale Waarabu raia waliobaki waliishi chini ya jicho kali la Serikali; waliweza kukamatwa, kama Wazanzibari wengine na kutiwa kizuizini bila kufunguliwa mashitaka.   Walifanyiwa jinsi serikali ilivyofikiri inafaa; mashamba na mali zao zilitaifishwa bila kufidiwa.
Wapo waliohukumiwa na “Mahakama ya wananchi” (tutaiona baadaye), kifungo na kuchapwa viboko kuonyesha kwamba Serikali ya Karume haikuwa ya mchezo; akaionya jamii ya Ki-Athnasheri wa Kiajemi kwamba kama wangeendelea kuleta “mgogoro”, wangefukuzwa wote Zanzibar licha ya kuwa raia.
Alitawala bila Sheria wala Katiba
Karume alitangaza utawala wa chama kimoja cha ASP na kuamrisha kila Mzanzibari mtu mzima, kuwa mwanachama. Kila familia ilitakiwa kutundika picha ya Karume nyumbani; kutofanya hivyo lilikuwa kosa la jinai lenye adhabu kali.
Kikosi cha Usalama wa Taifa chini ya Kanali Seif Bakari, kilichopewa jina la “Viwavi Jeshi”, na kufunzwa Ujerumani Mashariki kikaiva kwa mbinu za utesi na mauaji, kilipewa mamlaka ya kukamata, kutesa, kutia kizuizini na hata kuuwa bila mashitaka.  Yeyote aliyelalamika, hata juu ya upungufu wa chakula tu, aliitwa “adui wa Mapinduzi” na hivyo mhaini.  Enzi hizo, nduguyo akigongewa mlango usiku na kutakiwa kwa mahojiano na Serikali, usingemwona tena milele.
Wakati wa Karume hapakuwa na utawala wa Sheria wala Katiba;  amri za rais (decrees) ndizo zilizotawala nchi.  Mapema mwaka 1966, mfumo wa mahakama wa kawaida ulipigwa marufuku; na Oktoba 1966, rais alijipa madaraka ya kuteua mahakama maalumu za watu wasiozidi 14 wenye mamlaka ya kusikiliza kesi za makosa ya kisiasa kama vile uhaini, uhujumu uchumi na wizi wa mali ya umma.
Mahakama hizi hazikufungwa na kanuni zozote katika kusikiliza kesi; huduma za kisheria kwa watuhumiwa zilifutwa na mawakili kupigwa marufuku Zanzibar.  Upande wa mashitaka ndio uliokuwa pia upande wa utetezi; kwa maana kwamba, mwendesha mashtaka wa serikali alipomaliza kuwasilisha mashtaka dhidi ya mtuhumiwa aligeuka kuwa mtetezi wa mtuhumiwa.
Mahakama hizi zilipewa uwezo wa kutoa hukumu za kifo.  Mwaka huo huo (1966), Baraza la Mapinduzi lilipiga marufuku pia haki ya kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki [EACA] na rufaa zote zikawa kwa Rais Karume pekee.
Mwaka 1970, Karume alipitisha amri (decree) ya kuanzishwa mahakama (za kienyeji) za watu watatu.  “Mahakimu” wapya wa mahakama hizo waliteuliwa na Karume mwenyewe kutoka miongoni mwa makada wa ASP.
Moja ya sifa ya kuteuliwa ni kutokuwa msomi wa sheria, na ikiwezekana uwe hujui kusoma na kuandika.  Adhabu ya kifo ilipanuliwa kuingiza makosa kama vile utoroshaji wa karafuu, uhaini na utoaji mimba.   Matumizi ya vidonge vya uzazi wa majira lilikuwa kosa kubwa pia.
Karume alichochea hasira na chuki kubwa ya Wafanyabiashara wa Kiasia mwaka 1971, pale alipowapa notisi ya mwaka mmoja kufungasha virago kwa madai ya kuonekana kudhibiti uchumi wa Zanzibar.  Hasira yao iliungana na ile ya Waarabu ugenini waliofukuzwa mwaka 1964 na kupokonywa mali na mashamba yao bila kulipwa fidia; achilia mbali wale ambao mabinti zao waliozwa kwa nguvu kwa Wazanzibari Waafrika.
Wakati huo huo, Karume aliendelea kuwaachisha kazi na kuwatimua Visiwani, watumishi wa serikali waliojulikana au ndugu zao kuwa wafuasi wa zamani wa vyama vilivyopigwa marufuku vya ZNP na ZPPP na nafasi zao kujazwa na “watiifu” kwake.  Hata hivyo, kwa huruma ya Nyerere, walipewa utumishi serikalini Tanzania Bara.
Mapema mwezi Januari 1972, Waziri mdogo, Ahmed Badawi Qualletin, na afisa mwingine wa Serikali, Alli Sultani Issa, walifukuzwa kazi.  Kisha, Februari 1972, ujumbe mzito wa watu sita ulitumwa kwa Nyerere kumwambia awarejeshe Zanzibar, Abdulrahman Babu na wenzake kadhaa wakahojiwe kwa tuhuma za kutaka kuiangusha Serikali.
Babu ambaye alikuwa bado mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa Zanzibar, na aliyeamua kutorejea Zanzibar ya Karume kwa kuhofia usalama wake, kivuli chake na mzimu wa wahanga wa ukatili vilimtisha na kumnyima usingizi Karume, mithili ya Macbeth kwa mzimu wa Mfalme Duncan na Banquo, aliowaua kwa upanga ili atawale.
Nyerere, kwa kuhofia yaliyompata Hanga, Twala, Othman Sharrif na wengine kutokea alipowarejesha Zanzibar mwaka 1967, safari hii alikataa kumrejesha Babu Zanzibar, ingawa alikubali shinikizo la Karume la kumwachisha uwaziri katika Serikali ya Muungano.
Karume aliwatimua pia wataalamu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na kufunga Kituo chao cha Utafiti na Udhibiti wa malaria Visiwani kwa madai kwamba, Wazanzibari walikuwa “malaria proof”, yaani hawaguswi wala kuugua malaria.
Kwa hatua hiyo, ugonjwa wa malaria uliongezeka kwa asilimia 45.  Na ingawa Zanzibar ilikuwa na akiba kubwa ya fedha za kigeni, zaidi ya pauni za Uingereza milioni 14 kwenye Benki ya Urusi mjini London, (taarifa nyingine zinadai dola milioni 80), Karume hakuwa tayari kutumia fedha hizo kudhibiti malaria wala kuagiza chakula; badala yake akaona muhimu zaidi kuanzisha kituo cha televisheni ya rangi na ya pekee barani Afrika wakati huo.
Mwaka huo huo (1971), katikati ya mrindimo wa njaa Visiwani, Karume alipiga marufuku uagizaji wa chakula (mchele, sukari, unga wa ngano) kutoka nje, kama hatua ya kujitegemea kwa chakula.
Hatua hii ilizua tafrani na malalamiko na kusababisha biashara ya magendo ya chakula kushamiri; hapo, “Viwavi Jeshi” na mahakama za “kangaroo” zikapata wahanga kukamatwa, kushitakiwa na kunyongwa.  Watu wengi wakaikimbia Zanzibar. Aprili 1972, ukosefu wa chakula ulikithiri. Ni wakati huo Rais Karume alipouawa ghafla.
Kwa yote hayo, pamoja na tabia yake ya kutoamini wasomi na kuchukia wataalamu, Karume hatimaye alianza kuchukiwa pia na Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi wenye siasa za mrengo wa ki-Karl Marx.
Karume adha kwa Nyerere na Muungano
Nyerere alikuwa ameyatoa sadaka mengi ya Tanganyika kwa Zanzibar, ilimradi tu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ufikiwe. Kwa mfano, wakati Tanganyika ilipoteza hadhi ya kuwa nchi na baadaye jina lake, pale Muungano ulipobadili jina kutoka “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”,  kutwa “Jamhuri ya Muungano wa Tan-zan-ia”, Zanzibar ilibakia kuwa Zanzibar, na Karume akabakia Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania.
Si hivyo tu, Wazanzibari watano walipewa uwaziri kamili katika Baraza la Mawaziri 14 la Muungano.  Na ingawa idadi ya Wazanzibari ilikuwa asilimia tatu tu ya Watanganyika, lakini Zanzibar iliruhusiwa kuwa na Wabunge 52 katika Bunge la Muungano, wakiwamo Wajumbe wote 32 wa Baraza la Mapinduzi.
Licha ya upendeleo huu, Nyerere hakufanikiwa kudhibiti mhimili wa kisiasa Zanzibar chini ya Karume.  Mfano, Zanzibar chini ya Karume, ilikataa kuhamishia kwenye Muungano mambo mengi yaliyopaswa kuwa chini ya Serikali ya Muungano;  kwa mfano, iliendelea kudhibiti jeshi lake la ulinzi na Idara ya Uhamiaji, Karume akiwa amiri jeshi wake Mkuu.  Ndiyo kusema, aliuawa na wanajeshi  wa jeshi lake la Zanzibar, si Wanajeshi wa JWTZ.
Karume alikataa Serikali ya Muungano kugusa akiba ya fedha za kigeni ya Zanzibar, japokuwa fedha lilikuwa jambo la Muungano.  Aidha, Karume na Baraza lake la Mapinduzi walikiuka mara nyingi mapendekezo ya kisera kutoka Bara kiasi kwamba Nyerere hakuwa na kauli tena juu ya sera za kiserikali.
Karume akakataa pia mazungumzo zaidi ya kikatiba kwa hofu ya Zanzibar kupoteza hadhi na mamlaka yake.  Karibu kila alichopendekeza Nyerere, alipata jibu la mkato kutoka kwa Karume:  “Kama hivyo ndivyo, tuvunje Muungano”.
Mitazamo hasi ya viongozi hawa wawili juu ya Muungano, ndiyo iliyosababisha mchakato wa kupata Katiba ya Muungano ndani ya mwaka mmoja kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano usifanyike, na Muungano kuongozwa kwa Katiba ya Muda kwa miaka 13 hadi 1977 na baada ya Karume kufariki.
Nyerere alipowasilisha na kupitishwa kwenye Bunge la Muungano, Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa miaka mitano, na kutangaza nia yake kuona unatumika pia Visiwani, Karume aliupinga; akaja na mpango wake tofauti wa miaka mitatu kwa Zanzibar ulioandaliwa na mchumi kutoka Ujerumani Mashariki.
Kwa yote hayo na mengine, Nyerere alianza kuonyesha dhahiri chuki yake kwa utawala wa kimabavu wa Karume.  Naye (Karume) alipotambua hilo, alizuia mwingiliano huru wa watu kati ya Visiwani na Tanzania Bara kwa hofu na kwa sababu zinazofahamika.
Si mara moja, hofu na wasiwasi wa kimaasi vilipojionyesha Zanzibar, mamlaka za usalama zilimshauri Mwalimu kufuta ziara zake Visiwani.  Hofu hizi zilijidhihirisha zaidi pale Othman Sharrif, baada ya uteuzi wake wa Ubalozi Marekani kufutwa kwa shinikizo la Karume na kurejea Zanzibar, alipokamatwa na kutiwa kizuizini bila kosa.
Ilibidi Nyerere aingilie kati na kumwita Karume Ikulu, kuonyesha jinsi alivyochukizwa na kitendo hicho; lakini Karume alimkatalia, kuonyesha kwamba Nyerere hakuwa na mamlaka kwake. Sharriff aliachiwa baadaye kwa hiari ya Karume, na Nyerere akamteua kuwa Afisa Mifugo Tanzania Bara.
Hata hivyo, Oktoba 1969, wakati Nyerere akiwa ziarani nchi za nje, Sharrif alikamatwa Tanzania Bara na kurejeshwa Zanzibar alikouawa.
Zipi adha nyingine kwa Nyerere?  Ni nani huyu Luteni Hamoud Hamoud?  Kwa nini aliongoza mauaji ya Karume?
Tulimaliza kwa kuona kwa sehemu tu, jinsi alivyogeuka kuwa adha na kero kubwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kwa Muungano wenyewe, kiasi cha kuuweka Muungano huo kwenye hati hati ya kuvunjika.  Tuendelee na sehemu ya Tatu, kuona kilichofuata.KATIKA sehemu ya pili ya makala haya wiki iliyopita, tuliona jinsi Rais Abeid Amani Karume alivyotawala kwa mkono wa chuma bila kufuata katiba wala utawala wa sheria, na hivyo kujitengenezea maadui wengi katika jamii ya Kizanzibari na kwa makada wenzake wa ASP wenye siasa za mrengo wa kushoto ambao, alianza kuwatimua kazi au kuwahamishia kwenye Serikali ya Muungano.
Karume alikuwa mwiba kwa Nyerere
Mbali ya Karume kuweka wazi kwa kusema kwamba, “Muungano ni kama koti tu; likikubana au kukuzidishia joto unalivua na kuendelea na safari yako”, pia alijipa ujasiri usio wa kawaida kwa kumkatalia Nyerere hadharani kila mara juu ya baadhi ya mambo ya Muungano akisema: “…..kama ni hivyo, sikubali, bora tuvunje Muungano”.
Ni ujasiri huu wa Karume usio wa kawaida juu ya jambo nyeti kama hili, uliofanya Nyerere atoe tamko lake maarufu juu ya hatima ya Muungano akisema:  “Kama watu wa Zanzibar, bila ya ulaghai kutoka nje, wataona ni bora kuvunja Muungano, mimi siwezi hata kidogo kuwapiga mabomu na kuwaua wananchi wa Zanzibar.  Kama waliingia katika Muungano kwa hiari yao, vivyo hivyo wanaweza pia kujitenga kwa hiari yao.  Hatukuishinda Zanzibar (kuwafanya mateka) vitani” (Soma:  William Edgett Smith, “Mwalimu Julius K. Nyerere”, tafsiri ya Kiswahili na Paul Sozigwa, uk. 154).
Wakati Mwalimu alikuwa mstari wa mbele katika kupinga ubeberu wa Marekani wakati wa vita ya Vietnam, na kwa ukombozi wa nchi za dunia ya tatu kwa ujumla, Karume alimbeza na kutangaza adhabu kali Visiwani kwa yeyote aliyelaani na kupinga ubeberu, au kuimba nyimbo za kuikashifu Marekani.
Mwalimu alipokosana na Uingereza kwa nchi hiyo kuukingia kifua utawala wa kidhalimu, kibaguzi na wa mabavu (UDI) wa Ian Smith nchini Rhodesia Kusini (sasa Zimbabwe), na kwa sababu hiyo uhusiano wa Mwalimu na Balozi wa Uingereza nchini, Sir Horace Phillip kuingia mkwara, Karume alionyesha hadharani kila mara kusuhubiana na Balozi huyo kwa kicheko cha bashasha na uswahiba kwa chukizo kwa Nyerere.
Tunaweza kutua kidogo hapa kuangalia nyuma mazingira aliyokuwamo Karume, miezi michache kabla ya kifo chake; bila shaka tutabaini kuwa, kiongozi huyo alikuwa katikati ya uhasama na uadui wa kujitakia.
Kwanza alikuwa na uhasama mkubwa na jamii pana ya Kizanzibari kwa udikteta wake uliokithiri uliosababisha mauaji, watu kutiwa kizuizini au kuhamishiwa Bara.  Pili, kulikuwa na tatizo la njaa na mlipuko wa malaria; mambo ambayo hakuonekana kujali.
Tatu, kulikuwa na uhasama mkubwa wa kisiasa kati yake na makada wenzake wenye siasa za Ki-Karl Marx ndani ya ASP waliomtuhumu kushindwa kuongoza, achilia mbali jamii ya Kiarabu aliyoitimua kikatili Zanzibar na iliyoendelea kutema laana kwake ughaibuni.
Nne,  kulikuwa na Nyerere ambaye alianza kumuona kama mzigo na kero kwa Serikali ya Muungano na kwa siasa za kimataifa.  Yote haya yalikuwa baruti tosha kuweza kulipuka na kumdhuru Karume kwa namna yoyote iwayo.
Ni nani huyu Luteni Hamoud?
Luteni Hamoud Mohamed Hamoud, alikuwa mtoto wa mzee Mohamed Hamoud ambaye alikamatwa na kutiwa kizuizini na Karume miezi kadhaa baada ya Mapinduzi ya Januari 1964, na hatimaye kufariki dunia akiwa kizuizini.
Miaka kadhaa baadaye, wakati Hamoud Hamoud akichukua mafunzo ya kijeshi huko Tashkent nchi iliyokuwa katika  Shirikisho la Urusi ya zamani, alifahamishwa na mmoja wa wanafunzi wenzake juu ya kuuawa kwa baba yake.  Kwa uchungu mkubwa, aliapa sawia na baadaye, kwamba angemuua Karume kulipiza kifo cha baba yake.
Mfumo wa Usalama wa Zanzibar ulioenea kila mahali, ulijulishwa haraka na mmoja wa ma-ofisa usalama waliokuwa kwenye mafunzo pamoja na Hamoud, juu ya kusudio hilo la Hamoud.
Lakini cha kushangaza ni kwamba, Hamoud aliporejea Zanzibar baada ya mafunzo hakukamatwa wala kuwekwa kwenye uangalizi; badala yake alipandishwa cheo kuwa luteni usu, katika sherehe iliyohudhuriwa na Karume mwenyewe kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Zanzibar.
Ikumbukwe kuwa, suala la Usalama wa Taifa halikuwa jambo la Muungano; liliongezwa kwenye orodha mwaka 1984 kufuatia kadhia ya Aboud Jumbe ya kuchafuka kwa hewa ya kisiasa Zanzibar, likaunganishwa kusomeka kwa pamoja na jambo la Ulinzi kuwa “Ulinzi na Usalama”.
Pale risasi ya Hamoud ilipochukua uhai wa Rais Karume miezi kadhaa baadaye, Serikali ilisisitiza kwamba, mauaji hayo yalikuwa sehemu ya njama kubwa ya kuangamiza Mapinduzi ya 1964, kutokana kwamba, Hamoud na wauaji wenzake walikuwa wanachama wa zamani wa Umma Party, kilichokiunga mkono ASP huko nyuma, na kukipa [ASP] mwelekeo bora wa kiitikadi [Ukomunisti] na kuheshimika kisiasa.
Kufuatia mauaji hayo, watu 1,100 walikamatwa na kuhojiwa.  Babu alikamatwa na kutiwa kizuizini Tanzania Bara kwa tuhuma za kuongoza mpango mzima; nao maofisa wa ngazi za juu wa Kizanzibari Jeshini Bara, kama Ali Mahfoudh na wengine, nao walishukiwa na kuondolewa kwenye utumishi wa Jeshi Tanzania Bara bila kurejeshwa Zanzibar.
Mgongano dhana ya mauaji
Kuna dhana mbili zinazogongana, lakini zote zenye nguvu; juu ya sababu za kuuawa kwa Karume.  Dhana ya kwanza ni hii ya Hamoud kulipiza kisasi.
Lakini suala la kulipiza kisasi linakoma pale tunapoona watu kama Kapteni Ahmada na raia Ali Chwaya ambao hawakuwa na uhusiano wa kifamilia na marehemu Mohamed Hamoud aliyeuawa, kujiingiza katika kulipiza kisasi.
Lakini, kama tutakavyoona baadaye, Kapteni Ahmada alijiingiza kama hatua tu ya kujisafisha kwa kujutia ushahidi wa uongo aliotoa dhidi ya Hanga na wenzake 18 waliouawa mwaka 1969, na yeye kuonekana kama adui na msaliti wa umma wa Kizanzibari.  Inapofikia hapo, inakuwa dhahiri kwamba mpango huo ulibeba hasira za jamii pana ya Kizanzibari.
Dhana ya pili ambayo ndiyo msimamo wa Serikali ni kwamba, mauaji hayo yalikuwa mpango mpana wa kupindua Serikali.  Dhana hii inapata nguvu kutokana na watu wengi kuhusishwa na tuhuma hizi, lakini kama tu tuhuma dhidi yao zilikuwa za kweli; vinginevyo dhana ya kwanza inashinda.
Mipango ilivyopangwa na kupangika
Chuki binafsi?  Hapana, Hamoud hakuwa peke yake; ilikuwa ghadhabu ya umma kwenye jamii pana ya Kizanzibari, kila kundi au sehemu ya jamii na malalamiko yake.
Kwa mujibu wa taarifa za Usalama wa Taifa Zanzibar, mipango ya kupindua Serikali ya Karume ilianza kusukwa tangu 1967 – 1972 ndani ya Zanzibar na Tanzania Bara, ambako nyumba ya Abdulrahman Babu ilikuwa kituo cha mikutano ya Wazanzibari ya kupanga Mapinduzi hayo.
Kama hivi ndivyo, Karume alikuwa na sababu tosha kumtaka Nyerere kumrejesha Babu Zanzibar “kuhojiwa”, Februari 1972.
Mkutano wa mwisho ulifanyika Aprili 2, 1972, ambapo ilikubaliwa Mapinduzi yatekelezwe Aprili 7, 1972, yakihusisha makundi mawili: kundi la Wazanzibari kutoka Bara, wengi wao wakiwa wanajeshi, na kundi la Wazanzibari ndani ya Zanzibar, likihusisha raia na wanajeshi wachache.
Pamoja na uamuzi huo, kikao kilitoa majukumu mazito kwa baadhi ya washiriki, ikiwa ni pamoja na Hamoud na Ahmada kupewa jukumu la kuiba silaha kutoka kambi ya kijeshi, Bavuai.
Ilikubaliwa kuwa, Babu na wafuasi wake kutoka Bara wasafiri kwa mtumbwi kwenda Zanzibar Aprili 6 kuamkia alfajiri ya Aprili 7, na kufikia eneo lililopo kati ya mitambo mikuu ya mawasiliano [Cable and Wireless] na Klabu Starehe.  Baada ya hapo, Babu abakie amejificha kwenye nyumba ya Hamoud Hamoud, iliyotizamana na Klabu Starehe eneo la Shangani, kusubiri saa ya mapambano kuwadia.
Kwa mujibu wa taarifa, Babu aliondoka Dar es Salaam kwa mtumbwi uliofungwa redio mbili za mawasiliano, jioni ya Aprili 6, safari iliyoelezwa kuwa ya “kuvua samaki”; wakati madhumuni halisi yalikuwa ni kuwafikisha Babu na wafuasi wake Visiwani usiku wa Aprili 6, kwa maandalizi kamili ya kupindua Serikali
Jioni hiyo, Aprili 6, Uongozi wa Jeshi uligundua upotevu wa silaha nyingi Kambini Bavuai.  Na ingawa uongozi ulikuwa bado haujamhusisha mtu yeyote, lakini Hamoud, Hamada na askari wengine walianza kufuatiliwa kwa siri.
Yaelekea kufikia hapo, Babu alijulishwa na kuonywa kwa njia ya redio akiwa baharini, juu ya kugunduliwa kwa mpango mzima wa Mapinduzi; akakatiza safari na kurejea haraka Dar es Salaam hima.  Haijulikani kama wafuasi wake walikuwa wamekwishafika Zanzibar au la; au kama nao walijulishwa na kurejea Dar es Salaam.
Lakini kuwapo Visiwani wanajeshi kama Kanali Mahfoudh  (Mkurugenzi wa Operesheni JWTZ, Dar es Salaam) na Luteni Hashil Seif (Kikosi cha Wanamaji, Ukonga, Dar es Salaam) saa ya kuuawa Karume, kunaonyesha baadhi yao tayari walikuwa Zanzibar kusubiri wenzao.
Saa 12.00 asubuhi, Aprili 7; Ali Khatibu Chwaya (raia) alikwenda kwa Ali Mshangama Issa (afisa wa tatu, meli M.V. Afrika, mkazi wa Zizi la Ng’ombe, Zanzibar), kumweleza juu ya kutowasili kwa kundi la Dar es Salaam.
Baadaye asubuhi hiyo, Ali Mshangama, Chwaya, Miraji Mpatani  (karani wa shirika moja, Zanzibar), Mohammed Abdullah Baramia (Mtunza Bohari, Idara ya Elimu), Ahmada na Hamoud, walikutana nyumbani kwa Hamoud na kuonyesha kukerwa na kusikitishwa kwa kutowasili kwa wapanga mapinduzi kutoka Dar es Salaam, hasa wakijua pia kwamba, silaha zilizoibwa bado zilikuwa nyumbani kwa Hamoud, na hatari ya kuweza kugunduliwa.
Ilipofika saa 6.00 adhuhuri siku hiyo, Mshangama, Hashil Seif, Amar Saad Salim, maarufu kama “Kuku” (afisa usafirishaji, Idara ya Siha, Zanzibar) na Chwaya, walikutana nyumbani kwa Amar Saad ambako Mshangama, Hashil Seif na Baramia walipendekeza mpango wa kupindua Serikali uahirishwe hadi watakapopata taarifa tofauti kutoka Dar es Salaam.
Kwa hiyo, saa 9.00 mchana siku hiyo, saa mbili tu kabla ya kuuawa kwa Karume, Baramia alikwenda nyumbani kwa Hamoud eneo la Shangani kuwasilisha pendekezo hilo.  Alimkuta Miraji Mpatani nje ya nyumba na kumweleza Baramia kwamba, pamoja na kundi la Dar es Salaam kutowasili, Ahmada na Hamoud walishikilia Mapinduzi yafanyike tu siku hiyo, kwa sababu Ahmada alikuwa anatafutwa na maafisa wa Jeshi.
Je, ni kwa sababu hii Luteni Hamoud, Kapteni Ahmada na Chwaya waliamua kufanya Mapinduzi, licha ya wenzao kutaka yaahirishwe?.
Tuliona, baada ya kundi la Dar es Salaam kutowasili Zanzibar saa iliyopangwa, na Serikali ya Zanzibar kugundua kuibiwa kwa silaha Kambi ya Bavuai ambazo zingetumika katika Mapinduzi, na Luteni Hamoud na Kapteni Ahmada kuanza kufuatiliwa na wakuu wa Jeshi, wanajeshi hao waliamua kutekeleza zoezi hilo wenyewe kwa kumuua Rais Abeid Amani Karume dhidi ya ushauri wa washirika wao wa kuahirisha mapinduzi.SEHEMU ya tatu ya makala haya toleo lililopita, tuliona jinsi na namna mipango ya kupindua Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilivyoandaliwa kwa kuhusisha vikundi viwili; yaani kundi la Wazanzibari, wengi wao wakiwa wanajeshi, kutoka Dar es Salaam lililopanga kuwasili Zanzibar usiku wa manane kuamkia Aprili 7 na kundi la Wazanzibari ndani ya Zanzibar, lililojumuisha wanajeshi na raia.
Tuseme, kwa mfano, kwamba kundi la Dar es Salaam lingewasili Zanzibar kwa kazi hiyo kama ilivyopangwa, Mapinduzi yangetekelezwaje?
Kwa mujibu wa mkakati wa Mapinduzi uliofikiwa Aprili 2, 1972, Suleiman Mohamed Abdullah Sisi (mwanajeshi wa JWTZ, mkazi wa Ilala Flats, Dar es Salaam) alipangwa kuongoza utekaji wa kambi ya Jeshi, Mtoni, ambapo Kapteni Ahmada, alitakiwa kuteka kambi ya Jeshi, Bavuai, Makao Makuu ya Jeshi na Chuo cha Jeshi cha mafunzo ya Redio, vyote hivi viko eneo la Migombani.
Kituo cha Polisi cha Malindi kingeshambuliwa na kutekwa na kikundi chenye silaha kikiongozwa na Luteni Hamoud ambacho kingeweza kuteka magari yenye Redio za mawasiliano.
Askari Yusufu Ramadhan angeongoza kikundi cha maafisa wa Polisi walioingizwa kwenye mpango huo na kuteka Kituo cha Polisi cha Ziwani.
Amour Dughesh (mwanajeshi; Zanzibar), yeye angeteka Ikulu na kumkamata Karume, kisha kumpeleka Kituo cha Redio kumlazimisha atangaze kupinduliwa kwa Serikali yake.  Baada ya hapo, Kituo hicho kingeachwa chini ya udhibiti wa Badawi, Mpatani na Mohamed Said Mtendeni (mwandishi wa habari, gazeti la China, mkazi wa Vuga, Unguja).
Uwanja wa Ndege ungetekwa na kikosi cha wanajeshi na baada ya hapo kingeachwa chini ya udhibiti wa Ali Sultan Issa (meneja wa Shirika la Mafuta, Zanzibar).
Mpango huo ulilenga pia kuteka Makao Makuu ya Umoja wa Vijana wa ASP, ambayo yalikuwa pia Makao Makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa Zanzibar, ikiongozwa na Kanali Seif Bakari na kuwekwa chini ya udhibiti wa Mohamed Abdullah Baramia, Kapteni Khamis Abdullah Ameir, wa Makao Makuu ya Jeshi, Zanzibar; yeye alipangwa kuzuia mashambulizi kutoka nje kama Mapinduzi yangefanikiwa.
Mapinduzi au mauaji ya Kisiasa?
Mapinduzi ni kitendo cha kutaka kubadili sawia hali, serikali au mfumo fulani wa kijamii kwa matumizi ya nguvu, ikiwa ni pamoja na kuondoa mhimili wa mfumo huo.
Mapinduzi yanaweza kuwa kwa njia ya jeshi kama jeshi limetumika au ya kiraia kama raia walitumika, kama yalivyokuwa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Mauaji ya Karume hayawezi kuitwa mapinduzi ya kijeshi wala ya kiraia kwa sababu kifo chake hakikubadili mfumo wala muundo wa serikali.  Haya yanaweza kuitwa mauaji ya kisiasa yenye lengo la kuondoa chanzo au mhimili wa kero katika jamii bila kubadili serikali.
Mwanazuoni mahiri Barani Afrika, Profesa Ali Mazrui, anatafsiri “mauaji ya kisiasa (political assassination) kuwa ni kitendo cha siri cha kutoa uhai wa mtu mashuhuri kisiasa, kinachofanywa na wakala asiye wa serikali; kwa sababu za kisiasa au zisizofahamika.
Naye Profesa William Gutteridge wa Chuo Kikuu cha Aston, anasema mauaji ya kisiasa kuwa ni kitendo cha kutoa uhai wa mtu mashuhuri katika jamii kwa sababu za kisiasa na kinajumuisha pia jaribio la mapinduzi lililoshindwa na watu wengi kuuawa katika kutekeleza kilichokusudiwa.
Kwa mantiki hii, mauaji ya Karume, kama yalivyokuwa mauaji ya Rais Anwar Sadat wa Misri, kwa kupigwa risasi wakati akiangalia gwaride la jeshi lake, yalikuwa na lengo la kuiondolea jamii kero bila umuhimu wa kubadili serikali.  Katika mauaji kama hayo, mlengwa huwa mmoja tu kama chanzo au mhimili wa kero.
Karume aliuawa kwa sababu ya utawala wa kimabavu, ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu kama tulivyoona hapo juu; wakati Sadat aliuawa kwa kuisaliti jamii ya Kimisri, kwa kusaini Mkataba wa suluhu kati ya Misri na Israeli uliojulikana kama “Camp David” ili kusitisha harakati za Waarabu dhidi ya Uzayuni wa Kiyahudi.
Sababu nyingine ilikuwa ni kukumbatia sera za kiuchumi za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), hatua iliyoathiri maisha ya Wamisri kiuchumi na matarajio ya kijamii ya Waislamu nchini humo na Jumuiya pana ya Kiarabu kwa ujumla.
Malengo ya mauaji ya Karume yanajidhihirisha kwa vielelezo kwa yale yaliyofuatia chini ya utawala wa mrithi wake, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, aliyechukua uongozi Aprili 11, 1972.
Baraza la Mapinduzi lililoketi Aprili 10 – 11, 1972, pamoja na kumthibitisha Jumbe kuanzia Aprili 7, 1972 kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza hilo, pia lilipitisha azimio la kudumisha, kulinda, kutetea na kuendeleza fikra, malengo ya kimapinduzi na sera alizoacha Karume.
Hata hivyo, Wazanzibari wengi walitaka Kanali Seif Bakari amrithi Karume kwa kuwa alikuwa mtu wa karibu zaidi kwa Karume kuliko Jumbe, kwamba ndiye pekee miongoni mwa Wazanzibari ambaye angeweza kuendeleza fikra za mwasisi huyo wa Taifa la Zanzibar.
Nyerere aliingilia kati akiwa na hoja kwamba, kwa kuwa Rais Karume aliuawa na mwanajeshi, kumteua Bakari ambaye alikuwa mwanajeshi kumrithi kiongozi wa kiraia, kungetafsiriwa kuwa mapinduzi ya kijeshi yaliyoweka mwanajeshi madarakani.  Hoja ya Nyerere ikashinda.
Kwa kuanzia, Jumbe alifuta Amri ya Karume ya kutoagiza chakula na bidhaa nyingine kutoka nje; akaruhusu akiba ya fedha za kigeni kutumika kuagiza chakula kumaliza tatizo la njaa na upungufu wa vitu, jambo lililokuwa mwiko wakati wa Karume.
Vivyo hivyo, kwa mara ya kwanza, Serikali ya Zanzibar iliruhusu wanafunzi 17 kutoka Zanzibar, kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuahidi kupeleka wengi zaidi.
Desemba 1972, ASP kilifanya Mkutano Mkuu wake wa kwanza tangu 1962 uliohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 900 kutoka Visiwani, Mwalimu Nyerere na viongozi wengine wa TANU, pamoja na wageni wengine kutoka nchi 12 za Kiafrika, wakiwamo wawakilishi wa chama cha MPLA cha Angola.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Jumbe alilaani tawala za kimabavu na ubabe, ukandamizaji na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya raia, alisema:  “Viongozi lazima wawatumikie watu, na si watu wawatumikie viongozi…..”
Kwa maneno hayo, alikuwa amefungua milango ya demokrasia Visiwani, utawala bora, uwajibikaji na kuongoza kwa mifano, tofauti na enzi za Karume.    Februari 5, 1977, Nyerere na Jumbe waliunganisha vyama vyao, TANU na ASP, kuunda Chama cha Mapinduzi – CCM, jambo ambalo lisingewezekana wakati wa Karume ambaye hata Muungano wenyewe aliweza kuusigina kwa kisigino cha nguvu.    Vivyo hivyo, mwaka 1979, Zanzibar ilijipatia Katiba yake ya kwanza baada ya Katiba ya Uhuru ya 1963, chini ya Serikali ya Mseto wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP).    
Ni wakati wa utawala wa Jumbe, Zanzibar ilipata Bunge (Baraza la Uwakilishi) lake la kwanza kwa njia ya uchaguzi, wakati kabla ya hapo, Karume aliapa pasingekuwa na uchaguzi Zanzibar kwa miaka 50, kuanzia 1964 hadi 2014.Chini ya Jumbe, kwa mara ya kwanza tangu 1964, wanasheria waliruhusiwa kufanya kazi Zanzibar; watu hawakugongewa tena milango usiku na kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Na tazama, yote yalifanywa kuwa mapya, ambapo isingewezekana chini ya utawala wa Rais Karume.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI