Amissi Tambwe (kulia) ni moja ya washambuliaji hatari wa Simba sc.
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
KOCHA Patrick Phiri wa Simba amewataka mashabiki wa klabu hiyo kutokuwa na wasiwasi kufuatia kuumia kwa mshambuliaji Paul Kiongera kwa kuwa washambuliaji Emmanuel Okwi na Amissi Tambwe wanatosha kuongoza mauaji dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.
Kiongera raia wa Kenya aliyejiunga na Simba msimu huu, aliiumia goti dakika za majeruhi wakati wa timu yake ikishikwa kwa sare ya mabao mawili na mabingwa wa Tanzania Bara 1988, timu ya Coastal Union ya jijini Tanga.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa mshambuliaji huyo atakuwa nje ya uwanja kwa muda usiozidi wiki sita, hivyo kuikosa mechi ya msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga itakayochezwa Oktoba 12 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Emmanuel Okwi
Hata hivyo, katika mahojiano na mtandao huu akiwa Zanzibar leo mchana, Phiri amesema pengo la Kiongera litazibwa na wakali wengine wakiwamo Tambwe, Okwi, Elias Maguli na Amri Kiemba ambao wote alidai wanao uwezo wa kucheza nafasi ya Kiongera ya ushambuliaji.
“Kiongera ni mchezaji mzuri, lakini katika mpira lazima ukubaliane na hali yoyote. Kuna kipindi mchezaji nyota anashindwa kuitumikia timu yake kutokana na majeraha. Tunawaandaa wachezaji wetu hasa Kiemba achukue nafasi yake,” amesema Phiri na kuongeza:
“Tunamwandaa pia (Ibrahim) Twaha ili acheze nafasi ya (Haroun) Chanongo katika mechi yetu ya Jumamosi dhidi ya Polisi Morogoro. Kwa mujibu wa daktari wetu (Yasin Gembe), Chanongo atakuwa nje kwa siku 10 baada ya kuumia Jumapili.”
Amesema hakuna haja mashabiki wa Simba kuwa na presha kutokana na kuumia kwa wakali hao kwa vile "Simba ina wachezaji wengi mbadala katika kila nafasi."
Kikosi cha Simba kinaendelea na mazoezi Visiwani Zanzibar kujiandaa kwa mechi inayofuata dhidi ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Taifa.
Chanzo: Shaffih dauda
0 comments:
Post a Comment