Saturday, April 5, 2014

OPERESHENI SAFISHA JIJI YAWAGEUKIA OMBAOMBA

OPERESHENI ya kusafisha jiji ili kuwaondoa wafanyabiashara wadogo (wamachinga) kwenye maeneo yasiyo rasmi, imewageukia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na ombaomba.Operesheni hiyo inaendeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Akizungumza, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema uongozi wa Manispaa ya Ilala kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wanaendesha operesheni hiyo kwa ajili ya mkazi wa wilaya hiyo kufanya kazi zake kwa kufuata sheria.
Alisema hatua ya kuwaondoa watoto hao na ombaomba imetokana na ongezeko la watu hao, ambao wengi wao wamekuwa wakifanya vitendo hivyo huku wakiwa wanajiweza kifamilia.
"Sisi ni wasimamizi wa operesheni hiyo, wahusika wakuu ni halmashauri. Hata hivyo, wanapowaondoa mitaani yapo maeneo ya kuwahifadhi," alisema Minangi.
Alisema operesheni hiyo ya safisha jiji kwa utaratibu ulivyopangwa ni kwamba haitabakiza chochote na kusema kuwa kila anayejijua kuwa anakiuka sheria ni vema akajiepusha na vitendo hivyo kabla ya kufikiwa na mkono wa sheria.
Kamanda Minangi alisema operesheni hiyo inakwenda sambamba na zuio la pikipiki, bajaji na guta kuingia katikati ya jiji.
Jiji la Dar es Salaam sasa linaonekana kuwa safi ikiwemo hifadhi ya barabara kurudi kwenye hali ya kawaida na kuondoa msongamano, kutokana na operesheni hiyo iliyoanza siku mbili zilizopita.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI