Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
YANGA SC wanachuana vikali na Azam fc katika mbio za kuwania mwari wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.
Mpaka sasa mbio za ubingwa ni wazi na hakuna anayeweza kutabiri nani anaweza kubeba taji.
Mbeya City nao wanafuata nyuma yao wakiwa na dhamira ya kutwaa ubingwa au kushika nafasi tatu za juu katika msimamo.
Simba sc wameachwa mbali na hawazungumzwi kabisa katika kinyang`anyiro cha ubingwa.
Baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Tanzania Prisons, `Wajelajela` uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na Azam fc kushinda mabao 2-0 dhidi ya Mgambo JKT uwanja wa Mkwakwani Tanga, nafasi mbili za juu zimeonekana kuwa na ushindani mkubwa.
Kinachosubiriwa kwasasa ni timu moja kupoteza mchezo ili kuiruhusu nyingine kusogea juu zaidi.
Mpaka sasa Yanga wameshuka dimbani mara 21 na kujikusanyia pointi 46, huku Vinara Azam fc wakiwa wamecheza mechi 22 na kujikusanyia pointi 50.
Yanga wana mechi moja ya kiporo dhidi ya Kagera Sugar aprili 9 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Wakati timu hizi zikipigana kufa na kupona kuwania ubingwa, mechi zifuatazo zimebakia kwa kila klabu.
Ukiangalia uzito wa mechi zenyewe, pengine wale wataalamu wa kubashiri matokeo ndio wakati wao.
Kuna wakati soka linatabiriwa. Huwa ni bahati tu kwa wale wanaopatia utabiri, lakini mara nyingi matokeo ya mpira wa miguu hupatikana ndani ya dakika 90.
Sababu inayotumiwa na watabiri wengi ni ubora wa vikosi vya timu zitakazocheza, kuanzia mchezaji mmoja mmoja na timu kwa ujumla.
Ila mpira wa miguu huwa unaleta matokeo tafauti. Unaweza kuwa na timu bora na ukapoteza.
Azam fc wamebakiza mechi 4, huku mabingwa watetezi, Yanga wakibakiza mechi 5.
Machi 30 mwaka huu, Azam fc watakuwa wenyeji wa Simba katika dimba la Taifa.
Mechi hii inatazamiwa kuwa ngumu kwa timu zote kutokana na mazingira ya timu zote.
Simba sc hawana matumaini ya kutwaa ubingwa, lakini yawezekana wakaingia uwanjani kushindaa ili kulinda heshima.
Ukiwasikia mashabiki wa Simba sc, wanakiri kabisa kuwa hawana ujanja msimu huu, lakini bora kutoa pointi tatu kwa Azam fc jumamosi, ila si kwa Yanga aprili 19.
Sidhani kama benchi la ufundi nalo lina mawazo kama hayo. Bila shaka kocha Dravko Logarusic ataingia kwa nia ya kupata matokeo ya ushindi.
Joseph Marius Omog , kocha wa Azam fc ataingia kwa wembe ule ule anaotumia kuzinyoa klabu za ligi kuu.
Kwanza ataingia kulinda rekodi yao ya kutofungwa msimu huu katika mechi 22 walizocheza, lakini ataweka mkazo zaidi katika ushindi kwa kuvuna pointi tatu muhimu.
Kupoteza mechi au kutoa sare hayatakuwa matokeo salama kwa Azam fc , kwasababu Yanga atakuwa Tanga kukabiliana na Mgambo JKT.
Mechi nyingine iliyobakia kwa Azam fc ni aprili 6 mwaka huu uwanja wa Mabatini mkoani Pwani ambapo watakabiliana na Ruvu Shooting ya mkoani humo.
Hii mechi itakuwa muhimu zaidi kwa Azam fc, kwasababu wapinzani wao hawana cha kupoteza.
Hawawazi kushuka daraja wala kutwaa ubingwa. Hivyo `presha` itakuwa kwa Azam fc kutegemeana na matokeo ya Yanga.
Aprili 13, Azam fc watasafiri mpaka jijini Mbeya kuwafuata Mbeya city FC katika uwanja wa Sokoine jijini humo.
Hii dhahiri shahiri itakuwa mechi ngumu zaidi kwa Azam fc kwani Mbeya City ni washindani wao.
Haitakuwa kazi nyepesi kupata matokeo ya ushindi mbele ya wagonga nyundo hao wa Mbeya, kwasababu hawana rekodi ya kupoteza mchezo nyumbani kwao.
Baada ya kutoka Mbeya, Azam fc watarudi Chamazi kupambana na JKT Ruvu ya Fredy Felix Minziro.
Ugumu wa mechi hii utatokana na matokeo ambayo JKT Ruvu watakuwa nayo mkononi katika mechi nyingine watakazocheza kabla ya kipute hicho.
JKT Ruvu Wapo katika hatari ya kushuka daraja. Kama kufikia siku ya mechi dhidi ya Azam watakuwa wanahitaji pointi ili kujisalimisha, basi mchezo utakuwa mgumu kwa timu zote mbili.
Kama Azam fc watakuwa wamefanya vizuri katika mechi nyingine zote, bila shaka watakuwa wapo hatua ya mwisho kutangaza ubingwa wao wa kwanza tangu wapande ligi kuu msimu wa 2008/2009.
Kwa upande wa Yanga, machi 30 watakuwa ugenini kuwakabili Mgambo JKT katika uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga.
Hii itakuwa mechi ngumu zaidi kwa Mgambo kwasababu kupoteza tena baada ya kipigo cha 2-0 kutoka kwa Azam fc, itakuwa ni kujichimbia kaburi wenyewe.
Hakuna ufanano wa majina na ukongwe katika ligi kati ya Yanga na Mgambo.Pia timu hizi zina wachezaji wa aina tofauti.
Yanga wanaweza kupewa kura ya ushindi siku hiyo, lakini soka linachezwa uwanjani kwa dakika 90.
Baada ya kutoka Tanga, aprili 6 mwaka huu, wanajangwani watakutana na wapigania kukwepa kushuka daraja wengine msimu huu, JKT Ruvu.
Ugumu wa mechi hiyo utatokana na mazingira ya JKT Ruvu.
Yanga msimu huu wameshusha vipondo vikubwa kwa timu nyingi za majeshi.
Bila shaka kipigo cha mabao 7-0 walichokula Ruvu Shooting na cha mabao 5-0 walichoambulia Prisons vinatosha kukubaliana na hilo.
JKT Ruvu watahitaji kujipanga kwani kwa wakati huo Yanga watakuwa hawana cha kutafuta zaidi ya ushindi ili kutetea ubingwa wao.
Aprili 9, Yanga wataikaribisha Kagera Sugar katika dimba la Taifa jijini Dar es saalam.
Kagera wamekuwa washindani katika ligi kwa misimu kadhaa, lakini msimu huu mambo hayajawa barabara.
Si Kagera Sugar ya mwaka jana chini ya Abdallah Kibadeni `King Mputa`. Imekuwa ya kawaida sana. Ila huwezi kuwanyima kura ya kuwaharibia Yanga.
Aprili 13 katika dimba la Sh. Amri Kaluta Abeid jijini Arusha, Yanga watakuwa na vibonde, JKT Oljoro.
Mpaka kufikia siku hiyo hatima ya Oljoro kubaki au kushuka itakuwa imefahamika.
Kama watakuwa wameshakata tiketi ya kushuka daraja, basi kuna uwezekano wa kuwa mechi nyepesi kwa Yaga kwasababu Oljoro watakuwa hawana cha kufanya zaidi ya kuendelea na safari yao ya kuporomoka.
Mzinga wa mwisho kwa Yanga utakuwa aprili 19 mwaka huu ambapo watakabiliana na mahasimu wao, Simba Sc.
Hii ni mechi ambayo huwezi kuitabiri kwa kuangali ubora wa vikosi kuanzia mchezaji mmoja mmoja.
Utayakubali haya ukikumbuka mechi ya mzunguko wa kwanza ya mabao 3-3, halafu ile ya `Nani Mtani Jembe` ya 3-1.
Katika mechi hizi mbili, nje ya uwanja, Yanga walikuwa wanaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuwafunga Simba sc. Lakini haikuwa hivyo.
Kwa maana hiyo, usemi wa mechi ya Simba na Yanga haitabiriki, bado una nafasi katika mchezo huu.
Pia inawezekana mchezo huu ukaamua bingwa wa msimu huu, endapo Azam fc watakuwa na matokeo mazuri au Mbeya City.
0 comments:
Post a Comment