Tuesday, November 1, 2016

ZIJUE FAIDA ZA MBEGU ZA MABOGA

NI vizuri ifahamike kuwa mbegu za maboga hutokana na tunda liitwalo boga, tunda ambalo asili yake haifahamiki vizuri ni wapi, ingawaje baadhi ya tafiti zinasema kuwa asili yake ni Amerika ya kaskazini.

Zao la maboga mara nyingi hushamiri zaidi katika msimu wa joto na inashauriwa kupanda zao hili mwanzoni mwa mwezi Julai hasa katika udongo unaotunza maji vizuri.

Hata hivyo zao hili huweza kuathirika endapo kutakuwa na upungufu wa maji au joto dogo sana, lakini pia zao hili huweza kuathirika linapopandwa katika udongo ambao hauchuji maji vizuri.

Lakini tukiachana na hayo ni vizuri ifahamike kwamba mbegu za maboga zinafaida nyingi sana kiafya na hujumuisha kiwango kingi cha protini na vitamin, huku ikiaminika kwamba, mbegu hizo huweza kupunguza mafuta kwenye mishipa ya damu na jambo la msingi zaidi ni kwamba gramu moja ya mbegu za maboga huwa na protini sawa na glasi moja ya maziwa.

Watu wengi wanaweza kudharau mbegu za maboga pengine kwa kutokufahamu faida zake, lakini wazi kwamba mbegu hizi ni miongoni mwa mbegu zenye faida kubwa mwilini, kwani huweza kuzuia na kutibu hata baadhi ya magonjwa hatari yaliyoshindikana hospitalini.

Zifuatazo ni faida za kiafya ambazo mtu anaweza kuzipata kwa kula mbegu za maboga zikiwa mbichi au zilizo kaangwa:
Huimarisha moyo na mifupa
Mbegu za maboga huwa kiwango kingi cha madini aina ya magnesium, ambayo ni muhimu kwa afya ya moyo na uimarishaji wa mifupa pamoja na mishipa ya damu sambamba  na kuongeza ufanisi wa utumbo mpana . Magnesium inaonesha uwezo mkubwa wa kuzuia mshtuko wa moyo na kiharusi.

 Kinga ya mwili
Mbegu za maboga zina kiwango cha madini aina ya zink, ambayo pia yana faida nyingi mwilini ikiwa ni pamoja na na uimarishaji wa kinga mwilini , ukuaji wa seli, macho na ngozi ya mwili. Hali kadhalika zinki huimarisha nguvu za kiume.

Saratani ya kibofu
Kutokana na kuwa na kiwango kingi cha zinki, tafiti zinaonesha kuwa mafuta ya mbegu zenyewe za maboga huweza kutumika kama dawa ya kutibu saratani ya kibofu.

Ugonjwa wa ini
Mbegu za maboga pia zina kamba lishe na kinga kubwa ya kupambana na magonjwa nyemelezi. Mbali na hayo mbegu hizi zina virutubisho vinavyotoa kinga dhidi ya magonjwa ya ini na moyo.

Usingizi
Kwa watu wenye matatizo ya kukosa usingizi, wanashauriwa kula punje kadhaa pamoja na tunda lolote muda mfupi  kabla ya kupanda kitandani, utafiti umeonesha kwamba mbegu za maboga zina kirutubisho kinachohamasisha uzalishaji wa homoni za usingizi kwa wingi
 
Uvimbe
Mbegu za maboga zimeonesha kuwa na virutubisho vingi vyenye uwezo wa kuzuia magonjwa yote ya uvimbe mwilini, ikiwa ni pamoja na kuvimba miguu, vidole na hata majipu.

Mambo ya kuzingatia
Hakikisha unakula mbegu ambazo hazijaoza na zilizo safi na ambazo hazijakaa muda mrefu, lakini pia tumia mbegu hizo kwa usalama zaidi ikiwa ni sambamba na kuziosha na maji safi na salama kisha zianike na inapendeza zaidi ukila bila kukaanga, lakini ukila pia baada ya kukaanga bado utapata faida zake. Isipokuwa hakikisha haziungui wakati unapozikaanga unaweza kutumia dakika 10 tu katika zoezi hilo la kuzikaanga.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI