Friday, November 25, 2016

SERIKALI YATOA TAHADHARI JUU YA UGONJWA WA HOMA YA MANJANO NA DALILI ZAKE

WANANCHI wametakiwa kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa homa ya manjano huku akisema licha ya ugonjwa kutoingia nchini, wananchi wanapaswa kupata chanjo ili kuepuka homa hiyo.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ambapo amesema kuwa wananchi wanatakiwa kupata chanjo ili kuepuka kupata ugonjwa huo.
“Ugonjwa huu wa homa ya manjano bado haujaingia nchini kwahiyo kwao ni motisha hata mtu anasafiri au anajihusisha na masuala ya utalii na uwindaji ni motisha kwao kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa manjano. Na pia nitoe rai kuepuka au kupokea vyeti bila kupata chanjo kwani kufanya hivyo kuna hatarisha maisha yako na ya watu wengine na chanjo hizo zinapatikana katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ,uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) na uwanja wa ndege wa Mwanza lakini pia bandarini, bandari ya Dar es salaam, bandari ya Tanga, bandari ya Mwanza, bandari ya Kigoma na mipaka ya nchi kavu, Morogoro, Namanga, Holili, Tarakea na Sirari,Kasumulu, Tunduma na Dar es Salaam. Pia tumeweka katika kituo cha afya cha Mnazi mmoja,” alisema Mwalimu.
“Wizara inatoa onyo kwa vituo vinavyotoa chanjo hii bila kibali kuacha mara moja lakini kwa upande wetu sisi wizara tuna wajibu wa kuhakikisha chanzo hizi zinakuwa katika vituo hivyo hivyo ambavyo tumevipa mamlaka ya kutoa chanjo hizo,” alionya.
Aidha Waziri Ummy alitoa dalili za ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na, “kuwa na homa, kuumwa na kichwa, maumivu ya misuli pamoja na maumivu ya mgongo,mwili kutetemeka, kupoteza hamu ya kula, kusikia kichefuchefu, kutapika na mwili kuwa na manjano. Dalili nyingine ni kutokwa na damu sehemu za wazi mdomoni, puani, machoni, masikioni pia wakati mwingine damu huonekana kwenye matapishi, kinyesi na figo kuacha kufanya kazi kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa huu wa manjano ni kati ya siku 3 hadi siku 6 baada ya kuambukizwa. Ugonjwa wa homa ya manjano hauna tiba kamili lakini kinachotibiwa ni zile dalili ambazo zinatokana na homa ya manjano hivyo mtu akiupata ugonjwa huu anaweza akapoteza maisha kama hajapata huduma za afya mapema,” alisema.
“Habari njema ni kwamba ugonjwa huu una chanjo ambayo mtu akipata kinga asipate maambukizi na chanjo hii imekuwepo kwa muda mrefu na imethibitishwa na shirika la afya duniani kuwa na uwezo wa kumkinga mtu dhidi ya maambukizi ya virusi.”

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI