Meneja wa Tip Top Connection na wa Diamond Platnumz, Babutale anakabiliwa na mtihani mzito baada ya mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam kutoa hati ya kukamatwa kutokana na kudaiwa kutotii amri iliyomtaka amlipe Shekh Hamis Mbonde, shilingi milioni 250.
Kwa mujibu wa habari iliyoandiwa na gazeti la Mwanahalisi Jumanne hii, Tale anatakiwa alipe kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa kudaiwa kuvunja mkataba kati yake na Sheikh Mbonde wa kuuza na kusambaza nakala za mawaidha (DVDs) bila ridhaa ya sheikh huyo.
Tale na kaka yake Idd waliamriwa na mahakama hiyo kulipa kiasi hicho Februari 18 mwaka huu huku hati ya kukamatwa kwao ilitolewa July 8.
Mahakama ilitoa maelekezo kwa kamanda wa polisi kanda ya Ilala kuwa hadi Jumanne hii, July 19 wawili hao wawe wamekamatwa na kupandishwa kizimbani kujitetea kwanini wasipewe adhabu kwa kukiuka amri ya mahakama.
Hati nyingine ilitolewa Jumanne hii kwaajili ya kukamatwa kwa Babutale. Bongo5 imezungumza na Tale ambaye amedai kuwa makubaliano hayo yalifanywa baina ya sheikh huyo na marehemu kaka yake, Abdu Bonge na kwamba yeye hahusiki.
“Mimi na marehemu brother yangu tulifungua kampuni ya Tip Top Connection pamoja, mimi nifanye muziki yeye anisaidie.. Alipoona nimesogea akaona aachane na mimi ili afanye movie. Kwahiyo hakuwa anajua mimi ninachokifanya kwenye muziki, mimi pia sikuwa najua anachokifanya kwenye movie, imeenda akawa anafanya movie, sijawahi hata kushiriki hata kwa njia ya kuonekana location, hata kukaa nao kuongea nao lolote au kusainisha nao mkataba, so I know nothing,” amesema Tale.
“Mwaka juzi wakati nipo Uingereza yule Mzee akasikika kwenye U Heard kwamba anaidai Tip Top Connection milioni 50. Soudy Brown alimhoji akamuambia unamjua Babutale, akasema namjua lakini sijawahi kuongea naye hata siku moja. Akapeleka kesi mahakamani wakati brother yupo hai baadaye akaja akawa amefariki mimi nikawa sijui tena kinachoendelea. Kumbe yule mwanasheria alikuwa na marehemu brother na yule mzee wanakutana mahakamani. Mwaka huu kama mwezi mmoja uliopita akanipigia mtu simu, simu yangu napigiwa na watu wengi sana hii ‘mimi mwanasheria, unashtakiwa kwa kosa la kumdhulumu mtu kazi.’ Nikamuambia hizi kazi alikuwa akisimamia marehemu brother yangu kwahiyo story unazoniletea mimi unanirusha roho. Nikamwambia mimi naishi maisha yangu sijui kinachoendelea na sijawahi kujihusisha na chochote na hata huyo sheikh kama ana sehemu yoyote ambayo ameona kuna jina langu nimesaini naye niko tayari hata akisema ananidai,” anasisitiza.
“Kwahiyo wakati wanazunguka na kesi yao wakapita Brela kuchunguza hii kampuni wako nani na nani? Wakagundua kuna marehemu Abdul Bonge, mimi hapa na brother yangu mwingine lakini hawajui labda kwamba sisi tuligawana kila mtu na majukumu yake kwasababu kila mmoja alikuwa anafanya kile ambacho anakiweza.”
“Kwahiyo wameenda mahakamani wamepata barua wanikamate kwasababu mimi ninadaiwa. Mimi niko nyumbani wamekuja kugonga nyumbani kwangu kama majambazi. I was like wewe unakuja unajua hapa kwa nani? Mbona unataka kuniharrass rafiki yangu? Wewe unakuja kumkamata mtu usiyemfahamu! ‘Wewe si Tale’ walikuwa hawajui kama mimi ndio Babutale. Kama wao wananitaka wangeniambia mimi nipo Oysterbay polisi hapa, hawajaja. Mimi asubuhi ndio nikatoka nikaenda kumfuaya yule mwanasheria ambaye anasimamia kesi kuaniambia kuna nini naona kama watu wananitumia meseji kwamba nimeshtakiwa, akanihadithia in and out.”
“Tangu nijue kila kitu leo nina siku ya nne, I know nothing, sijawahi kumuona huyo mzee hata akitokezea sehemu simjui kwa sura. Lakini sasa yule mwanasheria wa yule mzee anasema Babutale ana hela, tukimshtaki Babutale atauza nyumba au watu watamchukua au tukimdhalilisha kwenye mitandao ataona aibu atataka kulipa. Vaa kiatu changu, wewe ni sehemu gani unalipa hapo? Sijui chochote, lakini wao wanaamini kwasababu mahakama imewaamuru nimewalipe milioni 250 na wanaamini mimi nina hela basi nitawalipa tu, haiwezekani,” amesema Tale.
Hata hivyo meneja huyo bado yupo njia panda kutafuta njia ya kujinasua kutoka kwenye hukumu hiyo nzito.
“Sijajua nini nitakachofanya, I know nothing,” anasema. “Anachokifanya ameamua kunichafua bila sababu, hajui kwamba mimi najianda kuwa waziri wa hii nchi na kuwa mbunge, anajiandaa kunifanya nionekane tapeli halafu ni mtu wa dini labda.”
Marehemu Abdul Bonge aliyefariki March 2015 na Mbonde waliingia makubaliano hayo June 16, 2013 kufanya biashara ya kurekodi mawaidha na kutengeneza nakala DVDs na kuziuza nchini.
Pia alimuahidi kumjengea nyumba, kumnunulia gari na kuitangaza kazi yake na kumpa shilingi milioni mbili na kumnunulia kanzu na kofia (baraghashia) na kurekodi DVDs zenye ujumbe Uzito wa Kifo, Fitina Juu ya Wanawake, Umuhimu wa Swala, Mwanadamu Yumo Ndani ya Hasara na Maadui wa Uislam, kwa mujibu wa Mwanahalisi.
Kwa mujibu wa Jaji Augustine Jangwa, makubaliano ya awali yalikuwa kurekodi halafu baadaye wakubaliane kuhusu bei na jinsi ya kuziuza na kwamba badala yake waliziuza na kuzisambaza nakala hizo na kujipatia faida bila kumshirikisha Mbonde ambaye alitumia ujuzi wake.
Awali Mbonde kupitia wakili wake Muhingo, Gwamaka Mwaikugile na Clement Kihoko alitaka alipwe shilingi milioni 700 kama fidia ya kuvunja makubaliano yao.
#Mwanahalisi Online
#Mwanahalisi Online
0 comments:
Post a Comment