Sunday, October 4, 2015

LOWASSA AMTOSA BINTI WA SOKOINE ....AMTAKA AHAMIE UKAWA AU AMSAMEHE

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa jana amefanya kampeni kwa mara ya kwanza katika jimbo la Monduli na kumnadi mgombea ubunge wa Chadema, Julius Kalanga huku akieleza kuwa atazungumza na mgombea ubunge wa CCM, Namelock Sokoine kuona kama atakubali kupanda basi la Chadema chini ya Ukawa.

Lowassa aliwaeleza wananchi wa Mto wa Mbu katika uwanja wa Barafu kuwa atakutana na Namelock leo ili waelewane kwa kuwa asingependa kuvunja umoja wao wa muda mrefu.

“Nimekuwa mbunge kwa miaka 20 hivyo natakiwa nimjue mbunge atakayefuata, nitakubaliana na Namelock akikataa kupanda basi hili basi,” alisema Lowassa.

Lowassa alisema anataka Monduli ibaki ile ile yenye amani na utulivu na ambaye hataki kupanda kwenye basi la Lowassa atabaki.

Wakati Lowassa akizungumzia suala la kujadiliana na Namelock, mgombea wa Chadema, Julius Kalanga alikuwapo akisubiri kunadiwa na mgombea huyo ambaye alitumia muda mwingi kumzungumzia Namelock badala yake (Kalanga).
Binti wa Waziri mkuu wa zamani, Edward Sokoine, Namelock Sokoine
Baadaye Lowassa alimnadi Kalanga akimwombea kura kwa wananchi na kumpa nafasi ya kunadi sera zake.

Kabla ya Lowassa kumzungumzia Namelock, waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alianza kuzungumzia suala hilo akisema, “Najua tunaye mtoto wetu tumemtunza Namelock lakini hatuwezi kumsaidia kwa kuwa amebaki kwenye gari bovu.”

Sumaye alimtaka Namelock kuachana na kadi ya kijani ili aweze kupata nafasi nzuri kwenye serikali ya Lowassa.

“Namelock atoke huko aungane na Lowassa hatuna sababu ya kuwa na tatizo naye. Nchi nzima inahitaji mabadiliko na Lowassa atashinda kwa asilimia 80, nashangaa Namelock anafanya nini huko CCM,” alihoji Sumaye na kuongeza: “Namwomba aachane na CCM aungane na sisi katika safari hii kwa kuwa nina uhakika Namelock atampigia kura Lowassa.”

Mbali na Lowassa kuzungumzia suala la ubunge, aliwaomba wananchi wa Monduli kumtafutia kura popote pale nchini kwa kuwa anahitaji kura nyingi ili aweze kushinda urais.

“Mpigie shangazi yako kule Tabora na mwingine yeyote ili tupate kura,”alisema Lowassa.

Pia, aliwaambia wananchi hao kuwa maendeleo yatakuja nchini kwa kushirikiana, hivyo waache kuwa na ugomvi kati ya wakulima na wafugaji.

Alisema amefika Mto wa Mbu kufanya kampeni ila atapanga siku ya kwenda kuwaaga rasmi ili waweze kula nyama pamoja.

Alisema pamoja na kwamba anaachia ubunge, ahadi zake alizozisema akiwa mbunge ikiwamo ya benki, atazitimiza.

Akizungumzia wito wa Lowassa, Namelock alisema hawezi kuzungumzia wito huo na kwa sasa anaendelea na kampeni za ubunge kupitia CCM.

“Sina maoni kuhusu kauli ya Lowassa, kwani sijamsikia mimi na hajawahi kuniambia, nimepewa taarifa hizi kwa simu, ninaendelea na kampeni, kesho (leo) nitakuwa Mto wa Mbu na Selela,” alisema jana.

Hata hivyo, Jumatano alipozungumza kwenye uzinduzi wa kampeni zake katika Kijiji cha Nanja, Namelock alimmwagia sifa Lowassa akimtaja kuwa mwalimu wake kisiasa na kuahidi kuendeleza mema yote aliyoyaasisi na kuyasimamiwa.

“Uhusiano kati ya Lowassa na familia ya Edward Moringe Sokoine umejengwa katika misingi isiyoweza kutetereshwa na harakati za kisiasa.

“Nitajidanganya kubeza kazi aliyofanya Lowassa kwa Monduli ikiwamo kuboresha huduma za elimu, afya, miundombinu na nyingine nyingi. Nitayaendeleza yote,” alisema Namelok.

Namelock pia aliwamwagia sifa wabunge wengine waliowahi kuongoza jimbo la Monduli akiwemo baba yake, Edward Sokoine na Lepilal ole Moloimet.

Alisema Lowassa ndiye alimtambulisha kwa wazee wa mila na wana Monduli kuwa anafaa kurithi kiti chake cha ubunge, hivyo ana imani atashinda na hatamwangusha kwa kuwavusha salama wana Monduli.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI