Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Ally Simba.
*******
NA JACQUELINE MASSANO
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imevitaka vituo vya redio na
televisheni nchini kuepuka kurusha habari za uchochezi hasa katika
kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.
Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Ally Simba, alipokuwa
akikabidhi leseni, cheti na kanuni na taratibu za utangazaji kwa AFM
Radio.
Dk. Simba alisema vyombo vya habari vinatakiwa kuepuka kurusha na kuandika habari zitakazochochea vurugu na uvunjifu wa amani.
Alisema jamii ina imani kubwa na vyombo vya habari na waandishi wa
habari, hivyo hawana budi kutumia weledi katika utoaji wa taarifa katika
kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.
Alisema radio 106 na televisheni 28, zimesajiliwa nchini na kwamba
katika kuelekea uchaguzi mkuu, tayari vituo vitano vya televisheni
vimekuwa na makosa yaliyosababisha kupewa adhabu na onyo.
“Kwa wale ambao hukutwa na makosa, tunawaita TCRA na kuwaeleza makosa
yao, kisha tunawapa adhabu, lakini kosa linapojirudia tunawatoza faini
na mwisho kituo kinafungiwa... hivyo tunavisisitiza vituo kutoa taarifa
kwa usawa,” alisema.
Akikabidhi leseni kwa Radio AFM, Simba alisema kituo hicho ni cha tisa
kwa Mkoa wa Dodoma kukabidhiwa leseni ya utangazaji baada ya kukidhi
vigezo.
Alisema wamekuwa wakihimiza uwekezaji kwenye tasnia hiyo nchini ili
kuongeza ushindani ambao huleta ubora na ubunifu kwenye urushaji wa
matangazo.
Pia alikitaka kituo hicho kuzingatia masharti waliyopewa kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya utangazaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa AFM Radio, Egbert Mhada, alisema wapo
tayari kuihudumia jamii ya wana-Dodoma kwa kufuata kanuni na taratibu za
utangazaji.
“Tumejipanga vizuri na tumefanya tafiti mbalimbali za kile jamii wanachohitaji,” alisema Mhada.
#NIPASHE
0 comments:
Post a Comment