Watu wasiofahamika, wameteketeza kwa moto makanisa matatu ya Kipentekoste yaliyopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana kwa kuhusisha Makanisa ya Pentecostal Assemblies of God (PAG) lililopo Buyekera kata ya Bakoba, Living Water International na Evangelical Assemblies of God (EAGT), yote yakiwa eneo la Kashura, Manispaa ya Bukoba.
Mchungaji wa Kanisa la Living Water International, Vedasto Athanas, alisema saa 10:00 alfajiri, usiku wa kuamkia jana, alipigiwa simu na jirani yake na kuelezwa kuwa kanisa linaungua moto.
Mchungaji Athanas alisema alilazimika kwenda haraka eneo la tukio na kukuta moto mkali ambao usingeweza kuzimwa kwa maji.
Alisema moto huo uliteketeza kabisa vitu vyote vilivyokuwamo ndani ya kanisa hilo.
Alivitaja baadhi ya vitu vilivyoteketea kwa moto kuwa ni viti 60, meza, mabenchi, vifaa vya ujenzi na madhabahu. Hata hivyo, Mchungaji Athanas alisema bado hawajawafahamu watu waliohusika na tukio hilo lakini waliponusa baadhi ya vitu, walihisi harufu ya mafuta ya taa.
“Hali hiyo ilitufanya tunaamini kuwa wachomaji walitumia mafuta ya taa kuteketeza kanisa hilo,” alisema Mchungaji Athanas. Alisema hilo ni tukio la tatu kwa Makanisa ya Living Water International kuchomwa moto.
Kwa mujibu wa Mchungaji Athanas, tukio la kwanza lilitokea Septemba, 2013 na la pili Aprili, mwaka jana. Naye Mchungaji Aristides Kabonaki, wa Kanisa la EAG alisema saa 11:50 asubuhi ya kuamkia jana, aliitwa na msichana wake wa kazi na kumueleza kuwa kuna moto unawaka kanisani.
Mchungaji Kabonaki alisema kanisa lote limeteketea kwa moto pamoja na mali zilizokuwamo ndani yake. Hata hivyo, alisema waliohusika na tukio hilo hawafahamu walikuwa na lengo gani.
Alisema alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa mtaa pamoja na polisi na anasubiri hatua za kiuchunguzi za jeshi hilo ili kubaini waliohusika na sababu za kufanya hivyo. Mchungaji Kabonaki alisema kabla ya uchomaji huo, watu hao wasiofahamika waliingia ndani ya kanisa hilo na kuiba baadhi ya mali zilizokuwamo ndani yake ikiwamo viti na vitambaa vya madhabahuni.
Akizungumzia tukio hilo, Regina Bakera, ambaye ni jirani na Kanisa la EAG, alisema kama muumini amesikitishwa na matukio hayo na hawafahamu waliosababisha hilo. Bakera alisema matukio hayo yanadhihirisha kuna kikundi kilichoandaliwa kwa ajili ya kuchoma makanisa na kuiomba serikali kuyashughulikia kufanya upelelezi wa kina.
Kufuatia uchomaji wa makanisa hayo, Umoja wa Wachungaji mkoani Kagera, umepanga kufanya maandamano ya kulaani kitendo hicho katika mkoa wote kwa madai kwamba serikali ilishindwa kutatua matatizo yanayowakabili ikiwamo la makanisa yao kuchomwa moto.
Mwenyekiti wa Makanisa hayo mkoani Kagera, Crodward Edward, alisema kwa sasa wanachukua hatua ya kujilinda kwa sababu serikali imeshindwa kufanya hivyo licha ya vikao ambavyo wamekaa viongozi wa serikali na wa makanisa hayo.
“Tumekaa nao katika vikao, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea. Tutafanya maandamano ya kulaani vitendo hivi mkoa mzima, lakini sasa tunawatangazia rasmi tunachukua hatua ya kujilinda wenyewe,” alisema Edward.
Akizungumzia matukio hayo, alisema siku za nyuma yalichomwa makanisa saba katika Mkoa wa Kagera huku moja likihusisha pia mauaji ya muumini mmoja. Hata hivyo, alidai kuwa waliokamatwa waliachiwa huru bila kuelezwa kinachoendelea na sasa yamechomwa matatu kwa siku moja.
Naye Mchungaji Aneth Sebastian, ambaye ni Katibu wa Wachungaji katika Manispaa ya Bukoba, alisema sasa wanashindwa kuiamini serikali na polisi kwa sababu watakuwa wanawafahamu wanaohusika na vitendo hivyo bali wanawakingia kifua.
Tathmini ya hasara iliyotokana na uchomaji wa makanisa hayo ambayo mawili yameteketea kabisa, bado inaendelea. Akizungumza kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Augustine Ollomi, alisema kwa sasa yuko safarini lakini aliahidi kutoa ufafanuzi kuhusiana na tukio hilo baadaye.
0 comments:
Post a Comment