Na Elizabeth Edward
Niwapongeze Baraza la Sanaa Taifa (Basata) kwa kuonyesha wazi kusimama kidete kulinda utamaduni wa Mtanzania na sanaa kwa ujumla.
Nikiwa kama mdau wa burudani kwa muda mrefu, nimekuwa nikishuhudia vitu vya ajabu kwenye sanaa ambavyo vinaonekana wazi kwenda kinyume na utamaduni wetu.
Uamuzi wa hivi karibuni wa Basata kuvunja ukimya kuhusiana na kuzagaa kwa picha za kudhalilisha za msanii Shilole umeibua matumaini mapya kwa Watanzania wengi ambao walianza kuhisi kuwa chombo hicho hakifanyi kazi yake ipasavyo.
Katika hali ya kawaida ilikuwa lazima kauli itolewe kuhusiana na picha hizo ambazo licha ya kumdhalilisha Shilole zimedhalilisha utu wa mwanamke.
Mbaya zaidi zimekwenda mbali na kuwadhalilisha wasanii wa Tanzania na taifa kwa ujumla kwani zilipigwa akiwa stejini nchini Ubelgji.
Kumradhi kwa muonekano wa picha za msanii Shilole, zinazomdhalilisha msanii huyo na wanawake kiujumla ambapo wasanii wa kike wamekuwa na tabia ya kuviweka viungo vyao vya siri hadharani.
Mithili ya upepo, picha hizo zilisambaa kwa muda mfupi kwenye mitandao ya kijamii na kuwafikia Watanzani ambao wengi wao walionyesha kukerwa.
Basata kama chombo kinachoangalia mwenendo wa sanaa na wasanii nacho kimeonyesha kusikitishwa na picha hizo hata kufikia uamuzi wa kumtaka aeleze sababu za kufanya udhalilishaji huo.
Kwa mujibu wa Basata, ilishawahi kumuita na kumuonya msanii huyo kutokana na tabia yake ya kutokujiheshimu awapo jukwaani na kuahidi kubadilika na kuachana na tabia hiyo chafu.
Hata hivyo, kuendelea kwake kufanya matukio hayo na kwa sasa katika ardhi ya nchi nyingine ni uthibitisho kwamba hajabadilika.
Kutobadilika huko kunamfanya aonekane kwamba ameendelea kuidhalilisha sanaa na wasanii wa Kitanzania wenye kujitambua na kuiheshimu kazi hiyo.
Nashindwa kuelewa tunaelekea wapi maana taratibu wasanii wa Tanzania wanaonekana kuachana na maadili yao na kuiga tamaduni za magharibi.
Hili limeonekana sana kwa sababu siku hizi dunia imekuwa kama kijiji ni rahisi kujua kinachoendelea mahali popote tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Inawezekana Shilole ndiye amekumbwa na fedheha hii ya kuonekana lakini hii ni tabia ya wasanii wengi wa kike ambao hujifanya wamechanganyikiwa wapandapo jukwaani.
Mara nyingi huwa najiuliza hivi muziki hauwezi kuchezeka au kunoga mpaka ukae nusu utupu au uonyeshe maumbile yako.
Hatukatazwi kuiga vitu kutoka ughaibuni lakini ni vyema tukawa tunachuja na kuangalia tunavyoviiga vinaweza kuwa na madhara gani.
Inawezekana wasanii wa Tanzania bado hawajajitambua kuwa wao ni kioo cha jamii, watoto wanawaangalia na kujifunza vitu vingi kutoka kwao.
Jamani wakati mwingine tunapaswa kuweka kando umaarufu na kuangalia utu na maadili maana ndiyo nyenzo pekee zitakazokufanya uheshimike.
Kila kukicha tunajiuliza kwa nini wasanii wa kike hawafiki mbali tunahangaika kumtafuta mchawi lakini tunasahau kuwa hali hiyo tunaisababisha sisi wenyewe.
Unafikiri ni watu wangapi wanaweza kuvumilia tabia hizi taratibu unajikuta unapoteza mashabiki hivyo soko la kazi zako litaporomoka.
Binafsi siamini kama utupu wa msanii unaweza kuwa chachu ya kuwavutia mashabiki wakapenda au kufurahia kazi zako.
Sitaki kuamini kama usanii au umaarufu wenu unawafanya mjione kuwa siyo wanajamii hata muishi kana kwamba mpo sehemu ambayo hakuna anayewaangalia.
0 comments:
Post a Comment