Thursday, May 14, 2015

TAYLOR SWIFT AMBWAGA JAY Z KWA MKWANJA

HAYUMO katika orodha ya wanamuziki 10 bora waliotengeneza fedha nyingi kwa mwaka 2014, lakini ukweli kwamba amemfunika Jay-Z katika orodha hiyo, ni jambo la kujivunia kwa Taylor Swift.
Kwa mashabiki wengi wa muziki, Jay Z ni jina kubwa na ndiye anayefahamika kuliko Swift, lakini katika kujiingizia fedha nyingi, Swift amempiga bao Jay Z.
Kwa mwaka 2014 kwa mujibu wa Jarida la Forbes, pato la Swift katika muziki lilifikia Dola 64 milioni na ameshika nafasi ya 11 miongoni mwa wanamuziki 30 waliojiingizia fedha nyingi kwa mwaka huo wakati, Jay Z ni wa 12 akiwa na pato lililofikia Dola 60 milioni.
Jina lake kamili ni Taylor Alison Swift na alizaliwa, Desemba 13, 1989, Pennsylvania, Marekani na hadi sasa ni mwanamuziki anayetamba katika miondoko ya country na pop.
Nyota ya Swift katika muziki ilianza kuonekana akiwa na miaka tisa, alipenda kufanya maonyesho ya muziki katika matamasha ya watoto.
Baadaye alionekana kuvutiwa na makali ya mwanamuziki, Shania Twain, alishiriki mashindano ya muziki ya vijana wadogo mara kadhaa na kushindwa lakini hakukata tamaa. Alidiriki kutumia siku zake za mapumziko ya mwisho wa wiki kwa kufanya maonyesho.
Akiwa na miaka 12 alianza kufundishwa namna ya kupiga gitaa jambo ambalo pia linadaiwa kumhamasisha kuanza kutunga nyimbo na wimbo wake wa kwanza kuutunga ulikuwa ni ‘Lucky You.’
Nje ya mafanikio hayo, Swift pia anakumbukwa hapo kabla alipoibuka kinara na kutwaa tuzo ya uimbaji mashairi kwa shairi lililoitwa, “Monster in My Closet,”.
Njia hizo alizopitia ndizo zilizomfanya awe gumzo na hata suala zima la kumfunika Jay Z kimapato kwa mwaka 2014 msingi wake umejengwa na mafanikio au nyota iliyoanza kuchomoza mapema.
Kwa sasa Swift ni mwanamuziki ambaye licha ya kujiingizia fedha nyingi kutokana na kazi ya muziki lakini pia ametwaa tuzo mbalimbali ikiwamo tuzo maarufu ya Grammy.
Ni kati ya wanamuziki wenye mauzo makubwa ya kazi zao duniani kote, akiwa ameuza nakala zaidi ya 40 milioni, kati ya hizo 27 milioni ameuza nchini Marekani.

Kwa wakati huu Swift anakimbiza na albamu yake aliyoipa jina la 1989 aliyoitoa Oktoba mwaka jana, ni albamu ambayo hadi Machi mwaka huu iliuza nakala 4.6 milioni Marekani pekee na kuzizidi albamu zilizotangulia za Speak Now ya mwaka 2010 na Red ya 2011.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI