Wednesday, May 13, 2015

RAIS KIKWETE ATEMBELEA MAENEO YALIOKUMBWA NA MAFURIKO, DAR ES SALAAM

RAIS Jakaya Kikwete jana alitembelea maeneo mbalimbali ya  Dar es Salaam  ambayo yameathirika na mafuriko kutokana na mvua inayoendelea kunyesha.

Ziara hiyo ilianzia  katika daraja linalotenganisha  Mbagala Kuu na Mtoni Kijichi katika Wilaya ya Temeke na kumalizia katika Daraja la Jangwani   katika Wilaya ya Ilala.

Rais Kikwete baada ya kuona daraja linalotenganisha Mbagala Kuu na Mtoni  Kijichi, alitoa agizo kwa Jeshi la Ulinzi wa  Wananchi Tanzania (JWTZ) kuweka daraja la muda katika  eneo hilo huku ujenzi ukiendelea.

Hata hivyo Rais Kikwete alipotembelea katika Daraja la Jangwani aliwataka wahandisi   kutumia  maarifa  kuondoa taka zinazosababisha madaraja hayo kuziba ili maji yaweze kupita kwa urahisi.

“Katika eneo hili tuliwaambia watu wahame lakini walikataa sasa tutafanyaje. Inabidi wahandisi mtumie maarifa ya kutoa taka zilizoziba katika madaraja haya ili maji yasipite juu ya daraja bali yaweze kupita chini kwa urahisi.

“Nimeanza ziara yangu ya kuangalia madhara yaliyotokana na mafuriko na nimeanzia  katika eneo la Mbagala na Jangwani.

“Kesho (leo) nitamalizia katika eneo la Mkwajuni na Tegeta na hapo ndipo nitakapotoa hitimisho  la athari za mafuriko   Dar es Salaam,” alisema Rais Kikwete.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia  Mjema, alisema imepokelewa msaada wa Sh bilioni 250 kutoka  Benki  ya  Dunia  kwa ajili ya kutengenenezea daraja la Mbagala Kuu na barabara kwa kiwango cha lami.

Alisema daraja hilo pamoja na barabara vitatengenezwa  kwa   miezi mitatu hadi minne.  


Naye Mhandisi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Eliseus Mtenga, alisema   itatafutwa  mashine itakayotoa taka zote zilizoziba katika daraja la Jangwani maji  yaweze kupita kwa urahisi.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI