Mkazi wa Mbondole, Kata ya Msongola, Dar es Salaam Uwesu Mansuri (28) akiwa kwenye kibanda alichotengenezewa na wazazi wake huku akiwa amefungwa mnyororo mguuni, jana. Picha na Pamela Chilongola.
Dar es Salaam. Unakumbuka masaibu ya mtoto, hayati Nasra Mvungi aliyeishi kwenye boksi miaka mitatu? Mkazi wa Mbondole, Wilaya ya Ilala, Uwesu Mansuri (28) naye ameishi kwa kufungwa mnyororo mguuni na wazazi wake kwa miaka mitatu kwa madai ya kulinda usalama wake.
Kijana huyo ambaye anapata huduma zote za kibinadamu chini ya kibanda kidogo kilichopo chini ya mwembe nyumbani kwao, ameonekana kudhoofika na kutoa harufu mbaya kutokana na kutoogeshwa kwa muda mrefu.
Taarifa za kufungwa kwa kijana huyo zilisikika kutoka kwa wakazi wa eneo hilo na mwandishi wetu alifika eneo hilo na kushuhudia jinsi alivyofungwa na kuishi katika mazingira machafu.
Kijana huyo anakula na kujisaidia hapohapo, jambo ambalo limeelezwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kuwa ni la unyanyasaji na hatari kwa afya yake.
Wakizungumza jana, wakazi wa eneo hilo walisema kijana huyo alifungwa mnyororo huo kwa zaidi ya miaka mitatu huku akiwa analala kwenye kibanda kidogo ambacho si salama kwake. Mmoja wa wakazi hao, Imelda Saburi alisema wanaona uchungu kwa kitendo cha wazazi hao kumfunga mnyororo kijana huyo huku akipata maumivu makali yanayomfanya awe analia kwa sauti kila siku usiku.
Alisema walijaribu kuwashauri wazazi hao wamfungue mnyororo huo na wampeleke hospitalini kupata huduma za afya lakini walikataa. “Tulimfuata baba wa mtoto huyo na kumshauri amfungue hiyo minyororo lakini alikataa ushauri wetu,” alisema Saburi.
Mkazi mwingine, Hassan Abdul alisema, wanashangazwa na wazazi hao kutojali huku wakimtenga na kumlaza nje akinyeshewa na mvua na kupigwa na jua.
Wazazi wajitetea
Mama mzazi wa kijana huyo, Zuena Ngarima alisema walilazimika kumfunga mnyororo mguuni kwa kuwa amekuwa akifanya fujo na kuharibu vitu mbalimbali vya wakazi wa eneo hilo.
Alisema mwaka 2009, kijana huyo alianza kuchanganyikiwa na walimpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MHN) na alilazwa kwa siku 19, alipopata nafuu aliruhusiwa kurudi nyumbani.
Ngarima alisema wakati kijana huyo akipata ugonjwa huo, baba yake mzazi alikataa kumpeleka hospitalini akidai atapona, ndipo alipoamua kuwafuata ndugu zake na kumlazimisha amchukue ili akapatiwe matibabu. “Mwanangu amelazwa Muhimbili mara tatu lakini baba yake haonekani na huwa hachangii na kuniachia peke yangu nikimuuguza.”
Alisema kutokana na kukosa mtu wa kumsaidia kumhudumia kijana huyo, analazimika kutombadilisha nguo zilizochafuka kwa haja ndogo na kubwa jambo ambalo limemfanya awe anatoa harufu kali.
Alisema yeye na baba wa mtoto huyo waliachana kutokana na matatizo ya kijana huyo, hivyo inampa wakati mgumu kumhudumia kijana huyo kutokana na kukosa fedha.
“Nina wakati mgumu sana. Kijana wangu hana mtu wa kumhudumia, hivyo ninalazimika kutoa hela siku mojamoja aweze kunyolewa nywele na kubadilishwa nguo,” alisema. Baba wa mtoto huyo, Mansuri Mchoi alidai kwamba mtoto huyo alianza kuchanganyikiwa baada ya kuvuta bangi, hivyo walimshauri asitumie kilevi hicho lakini alikuwa anaendelea.
Alisema baada ya kumtibu bila mafanikio, walikubaliana yeye na mama wa mtoto huyo wamfunge mnyororo huo ili asiwe mbali na wazazi kwa kuhofia kuharibu vitu vya watu.
“Tuhuma ninazopelekewa kuwa simtibii si za kweli. Huyu ni mtoto wangu ninamhangaikia sana aweze kupona, kama kuna mtu atajitokeza kumponyesha nipo tayari,” alisema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbondole, Thomas Nyanduli alisema ofisi yake imewaita wazazi hao ili kuchukua maelezo yao na baadaye hatua za kisheria zichukuliwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Merry Nzuki alisema hajapata taarifa juu ya tukio hilo na kuahidi kutuma askari wake kulifuatilia.
#MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment