POLISI aliyejiua kwa kujipiga risasi mdomoni, Aloyce Mafuru (24), amezikwa katika makaburi ya Mugumu, Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara bila huduma za kidini na kijeshi.
Askari huyo aliyekuwa dereva wa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Manyoni, Alute Makita alijiua Februari 2 nyumbani kwake na kuacha ujumbe kuwa polisi wasiangike kufanya uchunguzi kwani huo ni uamuzi wake binafsi.
Paroko wa Kanisa Katoliki Mugumu, Padri Aloyce Magabe jana aliwaeleza waombolezaji kuwa ingawa Mafuru alipata kipaimara, lakini kujiua kumesababisha kanisa kushindwa kuendesha ibada ya mazishi kwa kuwa kitendo hicho siyo mapenzi ya Mungu.
“Haifai kusema bwana ametoa na bwana ametwaa, maana tendo alilofanya huyu halimtukuzi Mungu bali shetani, maana ni kama ilivyofanyika kwa Kaini na Abel.
“Kaini alimuua ndugu yake na Mungu akamwambia atubu dhambi, akawa mkaidi kwa sababu alikuwa na roho ya shetani na matokeo yake alipata shida,” alisema Padri Magabe.
Aliwataka waombolezaji kushirikisha watu wengine matatizo yao badala ya kujiua, kwa kuwa uamuzi wa kujiua ni matokeo ya kutotafuta ushauri na kueleza kuwa tendo kama hilo linakosa utukufu kwa Mungu.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Manyoni, taratibu za mazishi ya kijeshi hufanywa kwa askari aliyeuawa, aliyeugua au aliyepata ajali, lakini anayejiua hapewi heshima hizo.
“Kwa askari aliyejiua hawezi kupewa heshima hizo kwa sababu anachukuliwa kama mwoga,” ilisema sehemu ya risala ya polisi katika mazishi hayo.
Katika tukio jingine, kwa mila na desturi za Kijita, maiti ya mtu aliyejiua haiingizwi ndani ya nyumba yake na badala yake shughuli zote hufanywa nje.
Mama wa marehemu Elizabeth Dalali alisema hana taarifa zozote kuhusu chanzo kilichomfanya mtoto wake ajiue kwa risasi.
Dalali alisema maiti ya mwanaye haikuingizwa ndani badala yake kilitengenezwa kibanda nje, kwani katika mila zao, kujiua ni kitendo kinachoashiria mikosi.
0 comments:
Post a Comment