Nesi Amina Mganda (27) anayedai kufa mara mbili.
NI JAMBO LA AJABU! Nesi aliyefahamika kwa jina la Amina Mganda (27), (pichani) mkazi wa Mbezi Maramba Mawili jijini Dar es Salaam, yupo katika mateso mazito yanayomfanya atamani kujiua na kudai kuwa ameugua na kupelekwa chumba cha maiti mara mbili baada ya kudhaniwa kuwa amefariki dunia.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwao mwishoni mwa wiki iliyopita, Amina alisema alianza kuugua miaka 10 iliyopita akiwa mwanafunzi wa kozi ya unesi katika Chuo cha Hospitali ya Muhimbili.
“Siku ambayo nilianza kuumwa nakumbuka ilikuwa mwaka 2006, nilikuwa nimefaulu mitihani yangu na kuwa wa kwanza ndipo mkuu wa chuo cha manesi Muhimbili akanipa ofa ya kwenda nchini China nikaendeleze ujuzi wangu.
“Nikiwa njiani narudi nyumbani siku hiyo ili kujiandaa na safari, nikataka kugongwa na gari lakini kwa mapenzi ya Mungu nikajitahidi kukwepa kwa bahati mbaya akagongwa mwanafunzi wa shule ya msingi na kufariki hapohapo.
Amina Mganda picha yake ya awali.
“Nilipofika nyumbani tu nikawa sijisikii vizuri, nikawaambia ndugu zangu kuwa natamani kufa, baada ya muda nikiwa nimekaa peke yangu nilijikuta nimerushwa kama vile nimenaswa na shoti ya umeme.“Nilipoteza fahamu kwa muda mrefu, nikapelekwa Hospitali ya Maghorofani hapa Mbezi na daktari aliponipima aliwaambia ndugu zangu kuwa tayari nilikuwa nimeshapoteza maisha. “Basi nikawekwa chumba cha maiti (mochwari) huku ndugu zangu wakifanya taratibu za mazishi na nilikuwa nimelazwa sakafuni, siyo kwenye friji, saa tisa usiku nilifumbua macho na wahudumu wa chumba kile wakanitoa, nikarudishwa nyumbani nikawa naombewa kila mara.
“Nilikata tamaa kabisa ya kuishi kwa sababu nilikuwa nikipelekwa hospitali nazungukwa na madaktari wengi ambao walikuwa wananitibu bila mafanikio, baadaye nikataka kujiua kwa kujichoma kisu au kujinyonga ikashindikana kwani ndugu zangu waliniwahi.
Amina Mganda wakati akiwa shule.
“Hivi sasa nakosa msaada, nimekata tamaa ya maisha, sina uwezo hata wa kutoka nje, nashinda ndani tu,” alisema mgonjwa huyo huku akitokwa na machozi.Alisema mwaka 2009 aliwahi kuugua na alipoteza fahamu tena na akadhaniwa amefariki dunia na kupelekwa mochwari ya Muhimbili huku watu wakijiandaa na mazishi kwa kupima vipimo vya sanda na jeneza, lakini alizinduka tena na kutibiwa kisha kurudishwa nyumbani.
Hivi sasa Amina amepooza kuanzia kiunoni hadi miguuni pia hana uwezo wa kusikia baada ya kupata homa kali iliyosababisha kuchomwa sindano 12 za quinini baada ya vipimo vya daktari kuonesha kuwa alikuwa akisumbuliwa na malaria.
Anaamini sindano hizo zimemfanya asisikie hali inayomfanya ashindwe kuwasiliana na mtoto wake mdogo.
Alisema ili aweze kupata matibabu anahitaji kiasi cha shilingi 800,000 kwani anasumbuliwa na tatizo la moyo kuwa mkubwa, uti wa mgongo, kutosikia na upungufu wa madini ya chuma mwilini. Kwa yeyote atakayeguswa na tatizo hili anaweza kumsaidia Amina kupitia namba ya simu 0784 098 829.
Chanzo: GP
0 comments:
Post a Comment