*Wazazi watathmini ujuzi wa watoto japo ni wa chini ila kwa usahihi.
*Na wala hawaoneshi kudai kubadili hali hii katika siku zijazo
MWANANCHI 1 tu kati ya 10 ndiye anayefikiri kuwa watoto wengi wanaomaliza darasa la 2 wana uwezo wa kusoma na kufanya hisabati wa darasa hilo hilo (ngazi ya darasa la 2). Mbaya zaidi, wananchi 3 tu kati ya 10 (31%) wanafikiri kuwa watoto hawa wanapaswa kuwa na uwezo wa kusoma na kuhesabu kwenye ngazi yao; ikimaanisha kuwa wananchi hawana matumaini kama kweli mfumo wa elimu utawafundisha watoto ujuzi na stadi wanazotakiwa kupata wakiwa shuleni.
Matokeo haya yalitolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Nini kinaendelea kwenye shule zetu? Wananchi watafakari juu ya hali ya elimu. Muhtasari huu umetokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika kwa njia ya simu mkononi wenye uwakilishi wa kitaifa ambao unauwakilishi wa kaya zote Tanzania Bara.
Muhtasari huu unachunguza hali ya shule zetu, ufundishaji na ujifunzaji pamoja na ushiriki wa wazazi kwenye elimu ya watoto wao. Licha ya matarajio ya chini kwenye mfumo wa elimu, wazazi mara nyingi hutimiza wajibu wao kuhamasisha na kusimamia ujifunzaji. Wanafunzi 7 kati ya 10 waliripoti kuwa wazazi wao hupitia na kukagua madaftari yao mara kwa mara.
Walimu wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanajifunza shuleni. Hata hivyo, hawawezi kufanya kazi hii kama walimu wenyewe hawaingii darasani. Wanafunzi 3 kati ya 10 walithibitisha kuwa mwalimu wao muhimu aliingia darasani vipindi vyote siku iliyopita. Wanafunzi 4 kati ya 10 (38%) waliripoti kuwa mwalimu wao hakuingia darasani siku nzima, na wanafunzi 3 kati ya 10 (28%) walisema kuwa, mwalimu aliingia baadhi ya vipindi tu vya siku hiyo.
Sauti za Wananchi iliuliza pia maswali kuhusu hali ya mazingira ya shule. Karibu wanafunzi wote (99%) wanafundishwa wakiwa madarasani, siyo nje, na wanafunzi 9 kati ya 10 (91%) hukaa kwenye fomu au dawati shuleni. Hata hivyo, ni nusu tu ya idadi ya wanafunzi (49%) waliosema hupewa chakula shuleni. Ingawa kukosekana kwa viti na madarasa kuna uwezekano wa kuathiri viwango vya kujifunza, watoto wanapokuwa na njaa wanakuwa na uwezo mdogo kupokea na kumiliki maarifa mapya.
Njia nyingine ambayo watoto huhifadhi maarifa ni kupitia kazi za masomo kufanyia nyumbani. Kazi hizi za masomo nyumbani husaidia wanafunzi kukumbuka na kupitia upya masomo ya siku hiyo na kufanya mazoezi elimishi ya yale waliyojifunza akiwa mwenyewe. Hata hivyo, wanafunzi 7 kati ya 10 (69%) waliripoti kuwa ni mara chache sana (au hawapewi kabisa) kazi za masomo za kufanyia nyumbani. Wakipewa kazi za masomo nyumbani, wanafunzi walisema kuwa mara nyingi kazi hizo husahihishwa.
Hivi karibuni Tanzania ilizindua Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Mpango huo umeiweka sekta ya elimu kuwa moja ya vipaumbele vyake muhimu. Sauti za Wananchi iligundua kuwa ni mtu 1 tu kati ya 7 (16%) ndiye aliyewahi kusikia kuhusu Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.
Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza, alisema "Utafiti wa Serikali na utafiti wetu (Uwezo) umeonesha kuwa watoto wako shuleni lakini hawajifunzi. Utafiti huu pia umegundua hali ya kutisha- theluthi mbili ya walimu hawaingii madarasani kwa siku nzima au baadhi ya vipindi. Hali mbaya ya mfumo wetu wa elimu sasa ni jambo la kawaida kiasi kwamba wazazi hawatarajii kama watoto watajifunza stadi wanaopaswa kujua. Kama tutaendelea katika hali hii, tutakuwa na kesho isiyo na mafanikio. Ingawa mpango kama BRN unatafuta kuinua ubora wa elimu, haiko wazi masuala gani ni kipaumbele muhimu kwa hali ya sasa."
"Kila shilingi inayotumika kwenye elimu inaweza kutumika mara moja tu. Kama raia wa nchi hii tunapaswa kudai kuwa sera zote za elimu, jitihada, vitendo na hatua kwa uaminifu kabisa zijikite kuboresha matokeo ya kujifunza. Bila kufanya hivyo, hakuna uhakika kwamba thamani ya fedha itapatikana. Kwa maneno mengine, watunga sera wanapaswa kutumia ushahidi kuwashawishi walipa kodi, Washirika wa sekta na wanasiasa kuwa fedha za kodi zinatumika kwenye sera zinazoleta manufaa na ambazo "zinanunua" matokeo ya kujifunza.”
0 comments:
Post a Comment