JE, wewe ni mchapakazi sana, wa kwanza kufika ofisini na kuwa busy na pia wa mwisho kutoka ukikabiliana majukumu yanayozidi saa za kawaida za kazi? Hongera kwa uchapakazi lakini utafiti huu unaweza kukufanya ubadili ratiba yako.
Tafiti nyingi zilizofanywa zimekuwa zikionesha madhara makubwa kwa watu wanaofanya kazi ofisini kwa muda mrefu zaidi, utafiti uliofanywa mwishoni mwa mwaka 2012 na kuchapishwa kwenye American Jounal of Epidemiology na kutolewa na mtandao wa Forbes, unaonesha kuwa mkusanyiko wa msongo wa mawazo (stress), shinikizo la damu (pressure), kutokuwa na hamu ya kula mlo kamili kunaweza kuwa kati ya sababu zaidi ya elfu moja zinaweza kusababisha matatizo makubwa ya afya.
Utafiti huo umebeba pia matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanywa katika miaka 50 iliyopita na kuonesha kuwa kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi ofisini kunaweza kusababisha uwezekano wa kuugua magojwa ya moyo kwa asilimia kati ya 40 na 80 ukilinganisha na mtu anaefanya kazi chini ya saa tisa kwa siku.
Tabia hii inaelezwa kusababisha pia tatizo la kumbukumbu hasa unapokuwa na umri mkubwa, hupunguza nafasi ya ubunifu wa hali ya juu na hupunguza uwezo wa kufanya maamuzi haraka kwa siku za usoni.
Dr. Marianna Virtanen na timu yake ya wafanya utafiti walikusanya data kutoka kwenye vyanzo vya tafiti 12 zilizowahi kufanyika tangu mwaka 1958, na walieleza kuwa watafiti wengi waligundua kuwa watu wanaofanya kazi muda mrefu zaidi kwa siku (zaidi ya saa nane) walikuwa katika hatari zaidi ya kuugua magonjwa ya moyo.
Katika utafiti wake, Dr Mariana aliwafanyia majaribio watu zaidi ya 22,000 kutoka Uingereza, Marekani, Japan, Sweden, Finland, Denmark na Netherlands.
Alisisitiza kuwa moja kati ya tatizo kubwa zaidi kwa wengi ni msongo wa mawazo wa muda mrefu, pia kukosa muda mzuri wa kufanya mazoezi ya viungo na zaidi wengi huwa hawana tabia ya kula vizuri kwa muda.
Inabidi ujiulize kama unafanya kazi muda mrefu, angalia pia matokeo ya harakaharaka yanayotokana na tabia hiyo. Utagundua afya yako huwa inakuwa hatarini ingawa unaingiza pesa nyingi au unakamilisha majumu kwa ubora uliotukuka.
0 comments:
Post a Comment