Friday, November 9, 2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - UCHAGUZI TAREFA, TAFCA SASA DESEMBA 22


Novemba 9, 2012
 
UCHAGUZI TAREFA, TAFCA SASA DESEMBA 22
Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) na Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) sasa utafanyika Desemba 22 mwaka huu.
 
Kwa mujibu wa ratiba za uchaguzi za vyama hivyo, Kamati zao za uchaguzi zitatangaza kuanza mchakato wa uchaguzi Novemba 10 mwaka huu wakati fomu kwa wanaotaka kugombea uongozi zitaanza kutolewa Novemba 12 mwaka huu. Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni Novemba 16 mwaka huu.
 
Kamati ya Uchaguzi ya Shirkisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa mwongozo huo kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA baada ya kuomba hivyo kutokana na wagombea sita tu kujitokeza kuomba nafasi tatu za uongozi katika mchakato wa awali.
 
Kwa waombaji ambao awali walichukua na kulipia ada ya fomu za kugombea uongozi TAFCA na TAREFA, hawatatakiwa kulipia tena ada kwa nafasi zile zile walizoomba, isipokuwa watatakiwa kujaza fomu upya.
 
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA FA MWANZA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Novemba 8 mwaka huu.
 
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa MZFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo katika Mkoa wa Mwanza.
 
TFF inaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati za Utendaji ya MZFA iliyochaguliwa chini ya uenyekiti wa Patrick Songora aliyechaguliwa kwa kipindi cha pili mfululizo.
 
Uongozi huo mpya wa MZFA una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba ya chama chao pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yao.
 
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya MZFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
 
Viongozi waliochaguliwa kuongoza MZFA ni Patrick Songora (Mwenyekiti), Nassoro Mabrouk (Katibu) na Richard Kadutu (Mwakilishi wa Klabu TFF).
 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI