Monday, November 26, 2012

SHARO MILIONEA AFARIKI DUNIA KWA AJALI YA GARI

Msanii maarufu wa Luninga, Sharo Milionea (pichani), amefariki dunia leo katiak ajali ya gari iliyotokea kijiji cha Lusanga, Muheza, mkoani Tanga. Kamanda wa Polisi Tanga, Constantine Massawe, amethibitisha kutokea kifo cha msanii huyo aliyekuwa aliyekuwa na vipaji vingi ikiwemo kuimba na kufanya michezo ya runinga.
 
MSANII nyota wa vichekesho na muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Ramadhani, maarufu kwa jina la Sharo Milionea amefariki dunia kwa ajali ya gari jana saa mbili usiku katika barabara ya
Segera-Muheza wakati alipokuwa akitoka Dar es Salaam kwenda Muheza.

Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Constantine Massawe amesema kwa njia ya simu kuwa, Sharo alipata ajali katika eneo la Maguzonizoga wilayani Muheza baada ya gari alilokuwa akiendesha kuacha barabara na kupinduka mara kadhaa.

Kwa mujibu wa Kamanda Massawe, marehemu Sharo alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 478 BVR na kwamba alikuwa peke yake kwenye gari.

Kamanda alisema hakukuwa na kona kali sana wala ubovu wa barabara kwenye sehemu aliyopata ajali Sharo Milionea na kwamba gari hilo limehifadhiwa mahali salama kwa sababu halitembei.

Kamanda Massawe alisema mwili wa marehemu Sharo umehifadhiwa katika hospitali teule ya wilaya ya Muheza.

Marehemu Sharo alianza kujipatia umaarufu baada ya kushiriki kwenye filamu za vichekesho zilizokuwa zikitayarishwa na msanii mkongwe wa fani hiyo, Amri Athumani maarufu kwa jina la King Majuto.

Baadaye alijitosa kwenye fani ya muziki wa kizazi kipya, ambapo alifanikiwa kuteka soko la muziki huo baada ya kuibuka na kibao cha Chuki za nini.

Hivi karibuni, Sharo alijiongezea umaarufu zaidi baada ya kushiriki kutengeneza matangazo ya Kampuni ya Simu moja hapa nchini akiwa na King Majuto.

Mtandao huu wa ULIMWENGU WA HABARI unatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wapenzi wa kazi za marehemu Sharo Milionea.
Habari na Liwazozito

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI