Sunday, October 28, 2012

NSSF: "HATUIPINGI FAO LA KUJITOA''

Mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa Taifa wa hifadhi ya jamii NSSF Dkt. Ramadhan K Dau akijibu maswali yaliyoulizwa na Wabunge wa kamati ya kudumu ya Bunge ya POAC (hawapo pichani).
Katika Kamati ya kudumu ya Bunge ya Mahesabu za Mashirika ya UMMA (POAC) mnamo tarehe 24/10/2012 Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dkt. Ramadhani K. Dau akijibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge alitoa maelezo ya msingi kuhusu umuhimu na dhana kamili ya Hifadhi ya Jamii.

Katika maelezo hayo alifafanua kuhusu madhara ya kujitoa kwenye mfuko kwa mwanachama aliye na uwezo wa kuendelea na kazi, na alisisitiza kuwa madhara ni kwa Mwanachama zaidi kuliko kwa Mfuko. Dkt.Dau alifafanua kuwa uamuzi wa kusitisha kwa Mafao ya kujitoa hauna uhusiano wowote na hali ya sasa ya kifedha ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Dkt. Dau aliieleza Kamati ya Bunge kuwa hali ya kifedha ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii hupimwa kwa kufanya Actuarial Valuation. Kwa upande wa NSSF zoezi hilo limefanywa mwaka 2009 na Kampuni kutoka Canada iliyoteuliwa na ILO na mwaka 2010 na Kampuni kutoka Afrika Kusini iliyoteuliwa na SSRA.

Matokeo yameonyesha kuwa NSSF HAINA MATATIZO YA KIFEDHA kwa sababu ina uwezo wa kuwalipa Wanachama wake na kulipia gharama za uendeshaji kwa kipindi cha miaka 50 ijayo bila kutetereka.

Dkt. Dau alifafanua zaidi kuhusu kutokuwepo kwa mafao ya kujitoa katika mfumo mzima wa Pensheni ulimwenguni kwa muongozo wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) namba 102 wa mwaka 1952 [The ILO Social Security (Minimum Standards) Convention, 1952 No. 102] ambao ndio unatoa maelekezo ya jumla kuhusu Sekta ya Hifadhi ya Jamii ulimwenguni kote.

Katika Muongozo huu ILO imetamka wazi kuwa kuna aina tisa (9) za mafao yanayotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na katika hayo hakuna mafao ya kujitoa. HITIMISHO Tunapenda kuwataarifu Wanachama na Wananchi kwa ujumla kuwa majibu haya ndio yaliyotolewa katika Kamati ya Bunge.

Taarifa zilizotolewa na baadhi ya Vyombo vya Habari kuwa “Mkurugenzi Mkuu wa NSSF apinga Mafao ya Kujitoa” zimetolewa nje ya maudhui yaani “Out of Context” Suala la Mafao ya kujitoa (Withdrawal Benefit) linashughulikiwa na Serikali na iwapo itaamuliwa na Bunge kurudisha mafao hayo,

NSSF HAINA PINGAMIZI na uamuzi huo na italipa mafao hayo bila wasiwasi wowote kwani ina uwezo mkubwa wa kifedha.

IMETOLEWA NA IDARA YA UHUSIANO - NSSF

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI