SIKU moja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuagiza Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akamatwe kwa kushindwa kuhudhuria kortini, mbunge huyo amedai hana taarifa hizo hivyo hawezi kujisalimisha popote.
Lissu ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, alidai atajisalimisha tu kwenye vyombo vya dola au kwenda mahakamni ikiwa atapelekewa barua aliyoandikiwa na mahakama na kutiwa saini na kugongwa muhuri na hakimu.
“Kaka, mimi siwezi kufanyia kazi za magazeti katika masuala ya kisheria, nipo hapa ninaendelea na shughuli zangu kama kawaida na kama mnavyoniona niko katika kuwawakilisha wananchi wa jimbo langu,” alieleza Lissu.
Mwanasheria huyo mkuu wa Chadema alitoa maelezo hayo jana alipohojiwa kuhusiana na habari zilizoandikwa na vyombo vya habari, kwamba Mahakama ya Kisutu juzi iliagiza mbunge huyo akamatwe baada ya kushindwa kuhudhuria katika kesi inayomkabili.
Mbali ya mahakama hiyo kutoa hati ya kukamatwa kwa Lissu, pia iliagiza iandaliwe hati ya kuitwa mahakamani kwa wadhamini wake ili wajieleze kwa nini wasilipe fungu la dhamana walilotia saini ambalo ni Sh10 milioni.
Kwa mujibu wa Hakimu Mkazi wa Kisutu, Thomas Simba, Lissu amekuwa hahudhuri kortini kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili pamoja na wahariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina na Jabir Idrisa na mchapaji wa magazeti, Ismail Mehboob.
Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14 mwaka huu, Dar es Salaam, Lissu na wenzake walikula njama za kuchapisha chapisho la uchochezi katika gazeti la Mawio lenye kichwa cha habari: “Machafuko yaja Zanzibar”.
Juzi, siku ambayo kesi hiyo ilipangwa kutajwa tena, Lissu hakuwapo mahakamani kutokana na kile mdhamini wake Robert Katula alichodai kuwa mshtakiwa huyo anaendesha kesi ya uchaguzi Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Mwanza hivyo asingeweza kuhudhuria.
Kutokana na maelezo hayo wakili wa upande wa Jamhuri, Patrick Mwita aliomba mahakama hiyo kutoa hati ya kukamatwa mshtakiwa jambo ambalo Hakimu Simba alikubali pamoja na wito kwa wadhamini kufika mahakamani Novemba 21, mwaka huu.
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Lissu alisema kuwa wito wa kwenda mahakamani ni lazima barua iwe imeandikwa na kugongwa muhuri na kutiwa saini ya hakimu wa mahakama na siyo kusikia na kwenda bila ya kuwepo kwa wito kamili.
0 comments:
Post a Comment