WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), bila shaka mko vizuri mnaendelea kusimamia jukumu zito katika taifa letu.
Usajili, Ufilisi na Udhamini siyo kazi ndogo. Ni kazi inayohitaji umakini wa hali ya juu maana matokeo ya ufanisi wenu ndiyo majibu ya shughuli nyingi katika nchi.
Watu wakitaka kusafiri, kutambulika katika maeneo mbalimbali nyinyi lazima mhusike kutatua.
Mkitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima.
Namshukuru Mungu naendelea na majukumu yangu kama kawaida. Nimewakumbuka leo kupitia barua hii ili niweze kuwafikishia yaliyoko katika akili yangu ndogo.
Madhumuni ya barua hii kwanza kabisa ni kutaka kuwauliza, hivi mmewahi kuwaza kwamba kuna uwezekano mkubwa wa watu kufanya madudu ya kufoji vyeti kama anavyodaiwa kufanya mshindi wa Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu?
Kwa kuanzia eneo hilo, ni vyema basi chombo chenu kikafanya tathmini upya katika kuhakiki taarifa mbalimbali na kuweka mfumo mzuri wa kudhibiti mtu kufanya udanganyifu wa aina yoyote.
Msisubiri hadi yatokee ya kutokea ndiyo muanze kuchukua hatua.
0 comments:
Post a Comment