Vijana mjini Mombasa.
Watu wanne wameuawa kwa kudungwa visu na vijana waliokuwa wamejihami mjini Mombasa Pwani ya Kenya.
Watu kadhaa pia walijeruhiwa katika shambulio hilo la usiku wa kuamkia leo kwenye vituo vya basi Kisauni.
Mwandishi wa BBC mjini humo Emmanuel Igunza anasema hali ya wasiwasi imetanda Mombasa huku maafisa wa polisi wakipiga doria mitaani.
Walioshuhudia mashambulio hayo wanasema vijana waliokuwa wamejihami kwa mapanga na silaha nyingine butu, waliwavamia watu katika vituo vya magari ya abiria.
Aidha inadaiwa vijana hao walikuwa wameziba nyuso zao, wakipeperusha bendera nyeusi sawa na ile iliyopatikana katika msako wa jana kwenye miskiti ya Musa na Sakinah, jijini Mombasa.
Awali Polisi walionya kuwa wako tayari kukabiliana na chochote kitakachotokea kufuatia msako huo.
Zaidi ya vijana mia mbili hamsini walikamatwa na silaha kadhaa ikiwemo magurunedi na bastola kupatikana katika misikiti hiyo.
Hata hivyo viongozi wa Kiislamu na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu wamelaani msako huo, ambao wanasema utaenndeleza dhana kuwa polisi wanailenga jamii nzima ya waislamu.
Mwezi Februari, msako sawa na huo uliotekelezwa katika msikiti wa Musa ulisababisha ghasia na kifo cha afisa mmoja wa Polisi.
Chanzo BBC Swahili
0 comments:
Post a Comment