Maelfu waandamana kupinga utawala wa kijeshi Ouagadougou.
Jumuiya ya kimataifa lataka jeshi Burkina Faso kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia wakati maelfu wakiandamana katika mji mkuu kupinga unyakuzi wa madaraka wa jeshi kufuatia kupinduliwa kwa rais.
Wapatanishi wametishia kuiwekea vikwazo nchi hiyo ya kimaskini ya Afrika magharibi iwapo jeshi litagoma kufanya hivyo.Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema baada ya jeshi kutangaza utawala wa kijeshi "Tunatowa wito kwa jeshi kukabidhi madaraka mara moja kwa maafisa wa kiraia."
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika magharibi Mohamed Ibn Chambas ameuambia mkutano wa waandishi wa habari katika mji mkuu wa Burkina Faso Ouagadouguo yeye na viongozi wengine wa Afrika wameshinikiza dai hilo katika mkutano wao na viongozi waandamizi wa jeshi.
Amesema iwapo jeshi litakataa kufanya hivyo matokeo yake ambayo hayatakuwa mazuri yanajulikana wazi na kwamba wanataka kuepuka kubidi kuiwekea vikwazo Burkina Faso.
Ombwe la madaraka
Luteni Kanali Isaac Zida wa kwanza kulia.
Jeshi lilingia kuziba ombwe la madaraka lililoachwa baada ya mtawala wa muda mrefu wa nchi hiyo Rais Blaise Compaore kujiuzulu hapo Ijumaa kufuatia maandamano ya ghasia ambayo baadhi ya watu wameyalinganisha na Vuguvugu la Majira ya Machipuko ya Nchi za Kiarabu.
Mamia kwa maelfu ya waandamanaji wakikasirishwa kutokana na mipango ya kurefusha utawala wa miaka 27 wa Compaore walikusanyika katika mitaa ya Ouagadouguo hapo Alhamisi na wengine wakalichoma moto jengo la bunge na majengo mengine ya serikali.
Kwa mujibu wa katiba ya Burkina Faso spika wa bunge alitakiwa kuchukuwa nafasi ya kuwa kiongozi wa nchi wa muda kufuatia kujiuzulu kwa rais.
Lakini jeshi badala yake likamtangaza Luteni Kanali Isaac Zida anayeshika nafasi ya pili ya uongozi katika kikosi cha ulinzi cha rais kuwa mkuu wa serikali ya kipindi cha mpito.
Zida amesema amechaguliwa kuhakikisha "mchakato wa demokrasia unafanyika kwa utulivu" katika nchi hiyo na kuahidi kushauriana na viongozi wa upinzani na wa mashirika ya kiraia.
'Ondoka Zida!'
Lakini maelfu ya watu wameungana katika maandamano Jumapili kupinga utawala wa kijeshi kufuatia wito wa viongozi wa upinzani na mashirika ya kiraia.
Waandamanaji wakiwa na bango la "Ondoka Zida!" Ouagadougou.
Mojawapo ya mabango yaliokuweko yalikuwa na maandishi "Hapana kwa utaifishaji wa ushindi wetu,wadumu wananchi!" na jengine lilikuwa na tamko la "Ondoka Zida!"
Wasulihishi kutoka Umoja wa Mataifa,Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi walimwambia Zida na viongozi wengine wa kijeshi kwamba kuna haja ya kuurudisha utawala wa kiraia.
Chambas amesewa wamewahakikishia kwamba wameufahamu vyema ujumbe wao huo.
Marekani yalaani hatua ya jeshi
Vikosi vya usalama vikiwasili katika makao makuu ya televisheni ya taifa Ouagadougou.
Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Jen Psaki ameelezea kutoaminika kwa hatua hiyo iliochukuliwa na jeshi na kusema Marekani inailani kwamba inajaribu kulazimisha matakwa yake kwa wananchi wa Burkina Faso.
Taarifa ya wizara hiyo imehimiza utawala wa kiraia uongozwe na katiba ya Burkina Faso na zichukuliwe hatua za haraka kuelekea kwenye uchaguzi huru wa rais.
Viongozi wa upinzani wamesema takriban watu 30 wameuwawa katika ghasia za maandamano hapo Alhamisi zilioukumba mji mkuu wa nchi hiyo lakini shirika la habari la AFP liliweza kuthibitisha vifo vya watu wanne tu.
Jeshi lataifisha madaraka
Viongozi wa upinzani na wanaharakati walitowa taarifa baada ya jeshi kunyakuwa madaraka wakidai mchakato wa kidemokrasia na serikali ya mpito ya kiraia katika nchi hiyo yenye watu milioni 17.
Taarifa yao imesema jukumu la kusimamia serikali ya mpito liko mikononi mwa haki ya wananchi na haliwezi kabisa kutaifishwa na jeshi."
Rais Blaise Compaore aliyelazimika kujiuzulu kutokana na shinikizo la waandamanaji.
Compaore na mke wake wameomba hifadhi katika nchi jirani ya Ivory Coast baada ya kundoka nchini mwao kupitia kusini mwa nchi hiyo kwa kile duru moja ya usalama ilichosema kwa kutumia msafara wa magari 27.
Ofisi ya rais ya Ivory Coast na vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo vimethibitisha uwepo wa rais huyo wa zamani nchini mwao ambapo inaelezwa kuwa amewekwa kwenye jumba la kifahari la serikali katika mji mkuu wa Yamaoussoukro.
Mzozo ulioko Burkina Faso ambayo ilikuwa ikijulikana kama Upper Volta wakati wa enzi ya ukoloni wa Ufaransa kabla ya kupatiwa uhuru wake hapo mwaka 1960 na kubadili jina lake hapo mwaka 1984 ni mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tokea wimbi la machafuko kuikumba nchi hiyo miaka mitatu iliopita.
Chanzo: DW
0 comments:
Post a Comment