Friday, September 19, 2014

SERIKALI YAAGIZA WATUMISHI WOTE WA UMMA WALIPWE MISHAHARA MOJA KWA MOJA KUPITIA AKAUNTI ZAO SAHIHI ZA BENKI

 Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu
*****
 Eleuteri Mangi - MAELEZO
Serikali imeagiza watumishi wote wa umma walipwe mishahara moja kwa moja kupitia akaunti zao sahihi za benki ambazo zitatumika kupitishia mihahara yao.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisi za Hazina leo jijini Dar es salaam.“Mishahara ya Watumishi wote wa Serikali, wakala na taasisi za umma italipwa moja kwa moja kupitia akaunti zao za benki” alisema Mwigulu.

Ili kufanikisha adhima hiyo ya Serikali, Mwigulu aliwaagiza waajiri wote wa sekta ya umma kuwa wawe na akaunti namba za benki za watumishi wao wote waliochini ya fungu husika ambazo zinataarifa sahihi na wakizingatia mfumo sahihi wa taarifa za kiutumishi.
Mwigulu alionya kuwa mtumishi asiye na akaunti benki asilipwe mshahara wake dirishani ambapo amewahimiza waajiri kuwasisitiza watumishi walio chini yao kufungua akaunti sahihi ya benki kwenye mfumo ambayo itatumika kulipa mshahara husika kupitia orodha ya malipo ya mshahara (payroll) inayotolewa na Hazina.

Aidha, Mwigulu amasema kuwa kila ifikapo tarehe 10 ya kila mwezi waajiri wote wawe wamewasilisha maombi ya fedha za kulipa mishahara kwa mwezi unaohusika wakiambatisha orodha ya malipo ya watumishi ya kuthibitisha kiasi kinachoombwa.

“Waajiri watakaoshindwa kutoa ‘Payroll’ watasababisha watumishi wanaowaongoza kushindwa kupata mishahara yao kwa mwezi husika jambo ambalo sio nia ya Serikali” alisisitiza Mwigulu.
Utaratibu huu wa kulipa mishahara utakuwa endelevu na umedhihirisha kuwa na tija kwa matumizi ya fedha za umma kwani umeonesha mafanikio ambayo kwa mwezi wa saba na wa nane hakuna mtumishi, Wakala za Serikali wala Taasisi iliyolalamika kukosa mishahara.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI