KIJANA Dullah amekumbana na matatizo mbalimbali baada ya kuzaliwa akiwa na homoni nyingi za kike na namna anavyotamani kuwa mwanamume wa ukweli, sasa hiki ndicho anachoeleza.
Anawachukia mashoga
“Nawashangaa mashoga, hizo haki wanazodai serikali iwapatie ni haki gani? Kama mimi Mungu ameniumba hivi najua ni kilema changu.
“Kwa sababu hao wote wanaodai haki za mashoga wanajifanyisha tu, kama kweli wana matatizo waonyeshe vyeti kutoka hospitali vinavyothibitisha kuwa wao wana dosari katika maumbile yao.
Mimi nina cheti kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na bado naendelea kwenda kliniki kila baada ya miezi mitatu ili nibadilishe hali yangu.
“Pia natumia dozi ya vidonge vitano vya Sh80,000 kila baada ya miezi mitatu, ndiyo maana najishughulisha na kazi halali, kama hivi natumia mikono yangu kufanya kazi naweza kupata hadi Sh250,000 kwa wiki,” alisema huku akiendelea kumchora mteja miguuni baada ya kumaliza mikononi.
“Nikikusanya hiyo fedha mama na watoto wa ndugu zangu ninao kaa nao nyumba moja wanakula vizuri,” aliongeza.
Uhusiano wa kimapenzi
“Sina bwana na sipendi kuwa na mabwana, ingawa nasumbuliwa sana na wanaume na hasa wanaume wa watu. Inatokea umefanya kazi watu wanachukua namba yako ya simu halafu wanawapelekea wanaume, ambao wananisumbua wananitaka kimapenzi jambo ambalo silipendi kwa sababu, mwanamume akishakuwa na wewe anakung’ang’ania na ndoa yake inakuwa kwenye matatizo.
“Nimewahi kufanya mapenzi kinyume na maumbile, japokuwa ni tendo ambalo silipendi, sipendi kufanya na vijana wadogo, nataka watu wenye heshima zao kwa sababu wanasaidia kutoa fedha ya kwenda hospitali kufanyiwa usafi.
”Naomba jamii ielewe kwamba mimi binafsi sifuati wanaume na kama wote wanaonitaka ningekuwa natembea nao ningekuwa nimetembea na watu wengi sana.
“Mimi mwenyewe nimejikubali na ninaendelea na kazi zangu na familia yangu imenikubali, maisha yanaendelea.
“Jamii ielewe kwamba wanaume wa sasa hivi baadhi yao wana laana mbaya, wafanyakazi wa serikali na wengine kama baba yako, lakini utashangaa wanakupigia simu wanakutaka kimapenzi.
“Baadhi ya watoa ushauri nasaha nao pia wanakupigia simu wanataka mkutane, wanaanza kukutongoza, basi ukikataa na kumshangaa kwa nini anafanya hivyo, anaanza kukubembeleza kwa ahadi mbalimbali ikiwamo fedha.
Anaeleza namna anavyoikumbuka siku aliyofanya mapenzi mara ya kwanza, kwamba hataisahau hiyo siku hadi anaondoka duniani, kwani kitendo hicho alikifanya bila ridhaa yake baada ya kuwekewa mtego na mtu ambaye alimwamini kama rafiki wa kawaida tu.
Anaeleza kuwa ilikuwa wakati wa sherehe (anaitaja), baada ya kula na kunywa na marafiki, kwa kuwa ilikuwa usiku na sehemu hiyo ilikuwa mbali na nyumbani, akaamua kutumia usafiri wa marafiki zake.
Anasema kuwa rafiki yake huyo alimkaribisha katika nyumba aliyokuwa amepanga maeneo ya (anayataja). Anasema kwa kuwa alikuwa amelewa hakujua nini kiliendelea hadi aliposhtuka na kujikuta amefanyiwa kitendo anachokitaja kuwa ni kibaya katika historia ya maisha yake.
“Nilijuta sana kukubali kupanda gari lao maana ningeondoka na usafiri wangu wa kawaida hayo yote yasingenikuta, nilitamani niende kuwashtaki, lakini niliogopa baadhi ya askari polisi nao wana mambo yao, maana ukienda unaambiwa unajifanyisha mambo hayo unayataka mwenyewe.
“Nilipotoka hapo nikarudi nyumbani kwa unyonge sana huku roho ikinisuta, nikikaa kidogo najifungia chumbani nalia sana, hadi mama yangu akanifuata chumbani kuuliza kulikoni.
“Kwa kuwa mama yangu ndiye kila kitu kwangu ikabidi nimweleze kila kitu kilichonitokea. Kwa kweli kama mzazi aliumia sana sipati kukwambia, na tangu wakati huo nikaanza kupunguza marafiki wa kiume kunikaribia hata nikiwa kwenye shughuli zangu. Matokeo yake nimekuwa najiweka karibu zaidi na marafiki wa kike kwa kuwa najisikia zaidi amani nikiwa nao,” anasema kwa uchungu.
Anaeleza kuwa kitu cha kushangaza kwa sasa ni kwamba hata baadhi ya marafiki hao wa kike alionaonao wamekuwa wakimgeuka kwa kuchukua namba yake ya simu na kuwapa wanaume wakora, ambao wamekuwa wakimpigia simu na kuanza kumtongoza wakitaka wakutane naye na kufanya naye mapenzi.
“Asikueleze mtu dada yangu, Mungu alikuwa na makusudio yake kuamua kuwa mwanamume aoe mwanamke na wazae watoto, kwa sababu kama ni laana basi mashoga wana laana tena mbaya sana.”
Alitaka kujinyonga
“Nilikuwa na mawazo mengi kuhusu hali niliyonayo. Namna watu wanavyonitania na kunizomea nikipita mitaani, ninaumia sana.
“Siku moja mama mmoja alinikasirisha sana, aliniita jina baya sana, nikaamua kurudi nyumbani nijinyonge. Nikafungua mlango wa chumbani kwangu nikachukua shuka nikapanda juu ya kabati la nguo, nikafunga kitanzi halafu nikaingiza shingo.
“Wakati nimeshaingiza shingo kwenye kitanzi nikasikia mlango unagongwa. Dada yangu alikuwa ananiita. Alikuwa anasema siyo kawaida yangu kujifungia chumbani. Alipoona kimya, alianza kugonga mlango. Akabomoa na kunikuta nimeshaanza kuning’inia, wakapanda kabatini huku mwingine akinishikilia miguuni. Wakakata shuka nikaanguka chini.
“Baada ya hapo walinipeleka hospitali. Niliumia sana shingoni hasa upande huu wa nyuma (anaonyesha), kumbe wanaojinyonga huwa wanaumia sana sehemu ya nyuma.
Tangu wakati huo mama yangu amekuwa na wasiwasi sana anaponiona sina raha au nina mawazo mengi,” ameeleza Dullah.
0 comments:
Post a Comment