NA BARAKA MBOLEMBOLE KWA MSAADA WA MTANDAO
SIKU YA Alhamis wiki hii, michuano ya 20 ya fainali za kombe la dunia itakata utepe wake nchini Brazil. Bila shaka pamoja na burudani inayotarajiwa kuonekana katika ardhi ya soka yapo matukio ambayo yanaweza kuvuta hisia kubwa zaidi wakati michuano ikiendelea na hata baada ya kumalizika kwake. Je, ni matukio gani ambayo unakumbuka msomaji wa mtandao huu?
Yafuatao ni matukio ambayo yamewahi kushangaza katika michuano ya kombe la dunia miaka ya nyuma.
VITA YA SANTIAGO:
Tukio hili linahusisha mpambano wa kukata na shoka kati ya Italia na waliokuwa wenyeji wa michuano ya Mwaka 1962, Chile dhidi ya mabingwa wa miaka ya 1934 na 1938, Italia . Ilikuwa ni mechi yenye rafu nyingi za hatari na ubabe wa kila namna. Mwamuzi kutoka England, Ken Aston alikuwa na wakati mgumu uwanjani katika mchezo ambao wenyeji waliibuka na ushindi wa magoli 2-0.
Giorgio Ferrinni, mlinzi huyo wa zamani wa Azurri alioneshwa kadi ya njano katika sekunde ya 12 tu ya mchezo, na kufikia dakika ya nane mchezaji huyo aliondoshwa nje ya uwanja na mwamuzi, Aston. Katika hali iliyoleta taharuki kubwa, beki huyo wa Italia aligoma kutoka uwanjani, na baada ya dakika kumi za kutumia nguvu hadi msaada wa askari polisi, ndipo mchezaji huyo akatoka uwanjani.
Wakati mechi ikiendelea kushika kasi mchezaji wa Chile, Lionel Sanchez akampiga ngumi kwa makusudi, Humberto Maschio wa Italia lakini bado mchezaji huyo hakupewa hata kadi ya njano achilia mbali nyekundu ambayo alistahili kupata kutokana na kitendo chake hicho kisicho cha kiungwana. David Mari wa Azurri alimrukia teke la shingo, Sanchez na kitendo chake hicho kilimfanya kuondoshwa uwanjani na Aston na kupelekea kadi ya pili nyekundu kwa Italia. Hii ilikuwa ni katika fainali za mwaka 1962 zilizofanyika nchini Chile ambazo Brazil walitwaa ubingwa wao wa kwanza katika bara la Marekani ya Kusini.
BRAZIL ILIPOCHEMKA NA PELE WAO
England walitwaa ubingwa wao wa kwanza na wa pekee mwaka 1962 katika michuano ambayo ilifanyika nchini humo. Mshambuliaji wa zamani wa Brazil, Pele alikwenda katika fainali zake za tatu za kombe la dunia baada ya kucheza zile za mwaka 1958 nchini Sweden akiwa na miaka 17 na kufunga magoli sita, kisha akaenda katika fainali za Chile miaka minne baadaye na kuisadia Brazil kutwaa ubingwa wake wa pili mfululizo. Akiwa na umri wa miaka 25, Pele hakuwa fiti kimwili katika michuano ya England
Ilikuwa ni faida kwa mabeki wa timu pinzani. Katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi dhidi ya Bulgaria, Pele alichezewa rafu nyingi sana na walinzi wa Bulgaria, ingawa alifunga goli moja katika ushindi wa Brazil wa magoli 2-0 siku hiyo. Pele hakuweza kufurahia michuano. Alikosa mchezo wa pili wa hatua ya makundi na aliporudi uwanjani katika mchezo wa mwisho dhidi ya Ureno hakuonekana kuwa fiti kwa asilimia mia. Ilikuwa ni mwisho wa Pele na Brazil katika michuano hiyo baada ya kuondolewa katika hatua ya makundi.
ITALIA WALITAKA KUNUNU MECHI
Italia ilikuwa ikihitaji sare tu ili kuvuka hatua ya makundi. Poland wakiwa tayari wamefuzu kwa hatua ya mtoano walikwepa mtego wa kupanga matokeo ambao ulitaka kuchezwa na Italia. Azurri walikuwa wakihitaji sare dhidi ya Poland katika michuano ya mwaka 1974 iliyofanyika nchini Ujerumani. Walijaribu kuwafuata Poland ili wawauzie mechi lakini katika hali ya kimchezo, Poland walikataa kufanya hivyo.
Na mara baada ya mchezo kumalizika, Italia walikuwa wamelala kwa kuchapwa magoli 2-1 na kuondoshwa mashindanoni katika hatua ya awali. Ujerumami waliokuwa wenyeji wa michuano hiyo walitwaa ubingwa. Italia ni wataalamu wa kupanga matokeo katika mchezo wa soka ila mbinu hiyo iligonga mwamba mbele ya Poland.
ARGENTINA ILICHUKUA UBINGWA WA KWANZA KWA NJIA CHAFU?
Ujerumani ilitwaa ubingwa ilipokuwa wenyeji wa michuano ya mwaka 1974. Safari katika fainali zilizorudi barani Amerika ya Kusini, katika nchi ya Argentina ilishuhudia wenyeji wakitwaaa ubingwa katika ardhi ya nyumbani na kufuata nyayo za mataifa ya Uruguay, England na Ujerumani. Katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi, wenyeji Argentina walihitaji ushindi usiopungua magoli 4-0 mbele ya Peru ili kufuzu kwa hatua ya mtoano Argentina walipata magoli mawili ya mapema kupitia kwa wakali wake, Mario Kempes na Alberto Talantallini. Hadi kufika mapumziko walikuwa mbele kwa magoli 2-0.
Mchezo ukaonekana kuwa na lengo la kuwabeba wenyeji na kuwaacha Brazil wakirudi nyumbani. Baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Argentina iliongeza magoli mengine manne na kufikia dakika 90 matokeo yakawa ni 6-O. Aliyekuwa kipa wa Peru, Ramos Quiroga ambaye ni mzaliwa wa Argentina alidaiwa kuachia magoli kimakusudi ili kuhakikisha Argentina wanavuka kundi na kuwatupa nje Brazil.
RAFU MBAYA ZAIDI
Italia ilitwaa ubingwa katika michuano ya mwaka 1982 nchini Hispania, Azurri walikuwa wakitamba kwa ‘ wataalamu wa rafu’. Lakini muda wote wa michuano hakujawaji kutokea rafu mbaya kama ile ambayo ilichezwa na golikipa wa Ujerumani i, Harald Schumacher dhidi ya mlinzi wa Ufaransa, Battison katika dakika ya 65 katika mchezo wa nusu fainali. Matokeo yakiwa ni goli 1-1 kipa huyo wa Ujerumani alitoka nje ya eneo lake la hatari na kumrukia mlinzi wa kushoto wa Ufaransa, Battison lakini kipa huyo hakupewa adhabu yoyote na mwamuzi.
Hakuoneshwa kadi ya njano, achilia mbali nyekundu aliyostahili kupata. Battison alibebwa kwa machela hadi nje ya uwanja ikiwemo kufanyiwa huduma ya kwanza kwa kuwekewa mashine ya hewa ya oxygen kabla ya kukimbizwa hospitali. Schumacher ambaye hakustahili kuendelea kuwepo uwanjani aliokoa penati ya mwisho ya Ufaransa baada ya mchezo kufika katika hatua ya kupigiana mikwaju ya penalty, na Ujerumani ikatinga fainali ambayo walipoteza mbele ya Italia waliotwaa taji lao la tatu la michuano na kulingana na Brazil wakati huo.
Tutaendelea kuwaletea matukio ambayo yamewahi kutokea na kushangaza watu wengi katika michuano hii mikubwa zaidi ya soka duniani. Nawe pia ndugu msomaji unaruhusiwa kutoa tukio ambalo unalikumbuka.
0 comments:
Post a Comment