Sunday, April 6, 2014

HABARI KUTOKA TFF:- STAND YASHINDA MALALAMIKO DHIDI YA JKT KANEMBWA

KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekubali malalamiko ya Stand United dhidi ya JKT Kanembwa kulalamikia timu hiyo kuchezesha wachezaji waliosajiliwa dirisha dogo kwenye mechi yao ya kiporo ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Mechi hiyo ya kundi C namba 22 awali ilichezwa mjini Shinyanga na kuvurugika, ambapo Bodi ya Ligi Kuu ya TFF iliagiza irudiwe kwenye uwanja huru, hivyo kuchezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
JKT Kanembwa ilishinda mechi hiyo iliyochezwa Februari 16 mwaka huu bao 1-0, lakini Stand United katika malalamiko yake ilidai timu hiyo ilichezesha wachezaji wanane waliosajiliwa katika usajili wa dirisha wakati mechi hiyo ilikuwa ni ya kiporo.
Kamati ya Nidhamu iliyokutana leo (Aprili 5 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Tarimba Abbas imeyakubali malalamiko hayo, hivyo kuipa Stand United ushindi wa pointi tatu na mabao mawili kwa mujibu wa Kanuni ya 8(22) ya FDL.
Upande wa walalamikiwa (JKT Kanembwa) uliowakilishwa na Mwenyekiti wake Luteni Menauri ulikiri kupokea maelekezo kutoka TFF kuwa wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo wasitumike katika mechi hiyo kwa vile ilikuwa ni ya kiporo.
Pia aliyekuwa Kamishna wa mechi hiyo Khalid Bitebo aliimbia Kamati kuwa baada ya kupokea maelekezo ya TFF alizifahamisha timu zote, lakini JKT Kanembwa iliondoa wachezaji wawili tu huku ikiwachezesha wengine wanane.
Nayo timu ya Gwasa Sports Club ya Dodoma iliyolalamika mbele ya Kamati hiyo kupingwa kunyang’anywa pointi sita na Kamati ya Mashindano ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kwa kumchezesha mchezaji asiye halali kwenye Ligi ya Mkoa, malalamiko yake yametupwa
Kamati imesema Gwasa imeshindwa kuonesha ushahidi kuwa ilimhamisha mchezaji huyo (Jeremiah Haule Jeremiah) kutoka timu ya AC Angry ya mjini Dodoma, na leseni iliyowasilishwa kuwa ndiyo aliyokuwa akiitumia AC Angry haoneshi msimu aliochezea timu hiyo.
Hivyo, Kamati ya Nidhamu imeridhia uamuzi wa Kamati ya DOREFA juu ya suala hilo ambapo Katibu wa Gwasa, Khalifa Ismail Ibrahim alikiri kuitwa kwenye kikao kilichofanya uamuzi huo na kuoneshwa vielelezo vilivyotolewa vya picha na fomu kuwa mchezaji huyo msimu wa 2013/2014 alichezea timu ya Katesh katika Ligi ya Mkoa wa Manyara.
Vilevile Kamati ya Nidhamu imebaini kuwa malalamiko ya Gwasa dhidi ya DOREFA hayakustahili kusikilizwa kwa vile kwa mujibu wa Kanuni, uamuzi uliofanywa dhidi yao haupaswi kukatiwa rufani.

KAMATI YA MAADILI YAWARUDISHA DARASANI AKINA MBAGA
Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesikiliza malalamiko dhidi ya waamuzi wa FIFA, Oden Mbaga na Samwel Mpenzu na kuagiza wakafanye upya mitihani ya utimamu wa mwili (physical fitness test) katika robo (quarter) inayofuata.
Katibu Mkuu wa TFF alikuwa amewalalamikia waamuzi hao pamoja na Mkufunzi wa CAF, Riziki Majala na Mkufunzi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mchungaji Army Sentimea kwa kuwafanyisha waamuzi hao mtihani huo kinyume na utaratibu ikiwemo pia kughushi matokeo.
Waamuzi hao wametakiwa kufanya mtihani huo katika robo inayofuata ambapo wakifaulu waendelee kuchezesha mechi. Waamuzi wa FIFA hufanya mitihani hiyo mara nne kwa mwaka.
Mbaga alifeli mtihani wa robo ya nne uliofanyika Desemba mwaka jana wakati Mpenzu hakufanya kabisa kwa vile alikuwa mgonjwa. Baadaye Majala aliwafanyisha mtihani mwingine waamuzi hao ambao haukutambuliwa na TFF kwa vile uliandaliwa kinyume cha taratibu, huku Mkufunzi huyo akidai ana mamlaka ya kuandaa mafunzo hayo.
Kamati hiyo iliyokutana jana (Aprili 4 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake William Erio, imesema imebaini hakuna utaratibu unaoeleweka wa kuendelesha mitihani hiyo, hivyo kuagiza TFF kufanyia kazi suala hilo ili kubainisha mamlaka na mipaka ya kila mhusika wakiwemo wakufunzi.
Vilevile Kamati ilibaini kuwa Mchungaji Sentimea hakuhusika kwa lolote katika uendeshaji wa mtihani huo ulioandaliwa na Majala, hivyo kumuondoa kwenye malalamiko hayo.
Kwa upande wa Ofisa Takwimu wa TFF, Sabri Mtulla ambaye alilalamikiwa kwa kuidanganya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuwa hakukuwa na pingamizi dhidi ya mchezaji Emmanuel Okwi wakati wa kipindi cha usajili wakati akijua lilikuwepo, Kamati ya Maadili imeagiza suala hilo liwasilishwe kwao upya pamoja na ushahidi wa kuthibitisha kama kweli mlalamikiwa alifahamu juu ya suala hilo.
Mtulla alijitetea mbele ya Kamati ya Maadili kuwa hakuwahi kuona wala kukabidhiwa barua ya Simba iliyokuwa ikipinga usajili wa Okwi katika klabu ya Yanga.

YANGA YAMLALAMIKIA STRAIKA WA MGAMBO SHOOTING
Klabu ya Yanga imewasilisha malalamiko Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuwa mshambuliaji wa Mgambo Shooting Stars ambaye alicheza dhidi yao katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Mohamed Neto si raia wa Tanzania na hana Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
Ingawa malalamiko hayo yamewasilishwa nje ya muda (time barred), TFF imeyapokea na itayawasilisha kwenye Kamati husika kwa ajili ya kupitiwa na baadaye kutolewa uamuzi.
Kwa mujibu wa kanuni, malalamiko yote kuhusu mchezo yanatakiwa kuwasilishwa ndani ya saa 24 baada ya mchezo kumalizika.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI