Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Bw. Andrii Deshchytsia akiwasilisha mbele ya Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Azimio ambalo pamoja na mambo mengine limeitaka Jumuiya ya Kimataifa na Mashirika ya Kimataifa, kutoitambua kura ya maoni iliyopigwa March 16 ya kujitenga kwa Crimea kutoka Ukraine na hatimaye kujiunga na Urusi, Ukraine inasema kura hiyo ya maoni si halali na ni njama za kumega mipaka halali ya nchi yake. Azimio hilo lilipitishwa siku ya Alhamis kwa kura 100 za ndiyo, 11 za hapana na 58 hazikuegemea upande wowote.
Muwakilishi wa Kudumu wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Balozi Vitaly I. Churkin akitoa maelezo kuhusiana na Azimio hilo lilowasilishwa na Ukraine na kuungwa mkono na nchi nyingi za Magharibi na zile za Ulaya, kwamba, kujitenga kwa Crimea kulikuwa halali na Urusi haikuwa na namna nyingine bali kuitambua kura hiyo na kusisitiza kwamba kihistoria Crimea ni sehemu ya Urusi.
Na Mwandishi Maalum
WAKATI hali ya sintofahamu ikiendelea kuwa tete kufuatia Crimea kuamua kupiga kura ya maoni na hivyo kujitenga kutoka Ukraine na kasha kujiunga na Urusi.Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, jana alhamisi, limepiga kura kupitisha na kuunga mkono azimio ambalo pamoja na mambo mengine, linaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuto tambua kwa namna yoyote iile kura hiyo na kujitenga kwa Crimea kutoka Ukraine.
Kabla ya tukio la upigaji kura kufanyika, baadhi ya wajumbe wanaoziwakilisha nchi zao, walitoa maelezo ya kwa nini nchi zao zilikuwa zimeamua kupiga kura ya ama kuunga mkono azimio , kutoliunga mkono au kutoegemea upande wowote.
Baada ya maelezo hayo, matokeo ya kura yalikuwa ifuatavyo, Nchi 100 zilipiga kura ya ndiyo, nchi 11 zikipiga kura ya kulikataa azimio wakati nchi 58 zenyewe ziliamua kupiga kura ya kutoegemea upande wowote.
Azimio hilo liliwasilishwa mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na Bw. Andrii Deschcytsia, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine ambaye katika uwasilishaji wake alijenga hoja zilizowataka wajumbe kuliunga mkono azimio hilo.
Naye Muwakilishi wa Kudumu wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Balozi Vitaly I. Churkin yeye pamoja na kutetea uamuzi wa serikali yake wa siyo tu kutambua kura hiyo ya maoni lakini pia kujitenga kwa Crimea, alitoa hoja ya kutaka upigaji wa kura hiyo uwe ni wa kura zilizohesabiwa (recorded vote).
Balozi Churkin alisititiza kwamba, kura ya maoni iliyopigwa na wananchi wa Crimea na hatimaye kuamua kujitenga na kisha kujiunga na Urusi ilikuwa ni ni kura halali na kwamba Urusi haikuwa na namna nyingine zaidi ya kuitambua kura hiyo.
Aidha kupitia azimio hilo ambalo limepitishwa baada ya Baraza Kuu la Usalama kushindwa kupitisha azimio kama hilo mnamo March 15 siku moja kabla ya kura ya maoni kufanyika baada ya Urusi kulipinga, linayataka pia Mashirika ya Kimataifa kuto tambua kujitenga kwa Crimea na jiji la Sevastopol kwa mujibu wa kura ya maoni ya March 16.
Ingawa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, limepitisha azimio hilo, azimio linakosa nguvu kama ambavyo lingepitishwa na Baraza Kuu la Usalama.
Wengi wa wazungumzaji waliounga mkono azimio hilo, au hata wale ambao hawakuegemea upande wowote,wamesisitiza haja na umuhimu wa kuheshimu Katiba ya Umoja wa Mataifa pamoja na Misingi ya sheria za kimataifa, ambazo pamoja na mambo mengine zinasisitiza kuheshimiwa kwa mipaka ya nchi na kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyigine, pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano
Baadhi ya wazungumzaji, wameleezea wasiwasi wao kuhusu kupitishwa wa azimio hilo ambalo limeungwa mkono karibu na nchi zote za Magharibi na zile za Ulaya kuwa kwa kufanya hivyo ni sawa na kuchochea zaidi mgogoro huo.
0 comments:
Post a Comment