Thursday, March 27, 2014

HAYA NI MANENO YA MASHABIKI WA TANGA KWA AZAM FC BAADA YA KUWAPIGA MGAMBO JKT

KWELI “Sasa mmekuwa, Mnacheza kama mabingwa, Mwaka huu wenu, Duh… wale mabeki hawana masihara…, Ukiwa na mshambuliaji kama Bocco lazima uwe unaongoza, Mmemtoa wapi kipa yule? Hakika mtakuwa mabingwa mwaka huu”
Hayo yalikuwa maneno ya mashabiki wa soka wa mkoa wa Tanga walioketi jirani na mwandishi wa ukurasa huu waliosikika wakitoa kauli tofauti baada ya mwamuzi kupuliza kipenga cha kumaliza mchezo,
Kauli hizi zimetokana na Azam FC kuendelea kujinafasi kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 2-0 jioni hii dhidi ya Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga licha ya washindani wao Yanga kushinda 5-0.

Ushindi huo, unaifanya Azam ifikishe pointi 50 baada ya kucheza mechi 22 na kubaki kileleni mwa Ligi Kuu, mbele ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 46 za mechi 21.
Mabao ya Azam FC ambayo jioni hii wamecheza kwa kujituma sana yamefungwa na washambuliaji wake, John Bocco dakika ya 63 kwa kichwa akiunganisha krosi ya kinda Gardie Michael na Mganda, Brian Omony aliyeingia dakika ya 53 kuchukua nafasi ya Gaudence Mwaikimba.

Bao la pili lilifungwa na Omony dakika ya 82 kwa shuti hafifu ambalo lilimteleza kipa Salehe Tendega na kuingia nyavuni.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Gaudence Mwaikimba/Brian Umony dk53 , John Bocco ‘Adebayor’ na Kipre Tchetche/Waziri Salum dk81.

Mgambo JKT; Salehe Tendega, Bashiru Chanache, Salim Gilla, Salum Kipanga/Salum Malima dk28, Bakari Mtama, Novart Lulunga, Mohamed Samatta/Nassor Gumbo dk78, Peter Mwalyanzi, Fully Maganga, Bolly Shaibu/Mohammed Neto dk35 na Malimi Busungu.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI