Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akijibu swali Bungeni leo mjini Dodoma.
Na Jacquiline Mrisho, Dodoma.
Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 13.17 katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa lengo la kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vya mkoa wa Ruvuma ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata maji safi na salama.
Kiasi hicho cha fedha kimetajwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge alipokuwa akijibu swali la Mhe. Jacqueline Ngonyani (Viti Maalum) lililohoji juu ya muda ambao Serikali itapeleka majisafi na salama katika Mkoa huo.
Waziri amesema kuwa Mpango wa Utekelezaji wa Maji Vijijini ulioanza mwaka 2006/ 2007, mkoa wa Ruvuma ulipangiwa vijiji 80 na kati ya vijiji hivyo jumla ya vijiji 76 vilipata maji safi na salama.
“Asilimia kubwa ya vijiji vilivyokuwa katika miradi hiyo vimepata maji safi na miradi iliyobakia ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji hivyo kwa mwaka huu wa fedha Ruvuma imetengewa kiasi cha fedha cha bilioni 13.17 ili changamoto ya maji safi na salama katika mkoa huo iishe kabisa”, alisema Lwenge.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea na mipango ya kuboresha huduma hizo katika miji ya Songea, Mbinga, Namtumbo na Tunduru iliyopo katika mkoa huo ambapo kwa mji wa Songea, mradi wa ukarabati wa chanzo cha maji cha mto Ruhila Darajani umekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 2.6.
Amefafanua kuwa kukamilika kwa chanzo hicho mnamo mwezi Februari mwaka huu kumeongeza kiasi cha upatikanaji wa maji wa jumla ya lita milioni 6 kwa siku ambapo wakazi 164,162 wamenufaika katika Manispaa hiyo.Aidha, Mhandisi Lwenge amebainisha kuwa kwa sasa Serikali imekamilisha usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya uboreshaji wa huduma hizo katika miji iliyopo katika mkoa huo.
“Serikali inaendelea na jitihada ya kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo ambayo kwa mji wa Tunduru mradi utagharimu Dola za Kimarekani milioni 7.3, mji wa Namtumbo ni Dola za Kimarekani 12.08, na Dola za Kimarekani 11.86 kwa ajili ya mji wa Mbinga”, alisema Mhandisi Lwenge.
0 comments:
Post a Comment