SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar Mhe. Pandu Ameir Kificho akiwa katika mazungumzo na Viongozi wa Jumuiya ya nchi za Ulaya ( EU) hapo Baraza la Wawakilishi Chukwani
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar Mhe. Pandu Ameir Kificho akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Jumuiya ya nchi za Ulaya ( EU) hapo Baraza la Wawakilishi Chukwani
Na, Himid Choko BLW.
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar Mhe. Pandu Ameir Kificho ameelezea matumaini yake kwamba uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki.
Amesema hali hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu hapa nchini suala ambalo ni muhimu kwa mustakbali wa maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii.
Spika Kificho amesema hayo leo, huko Afisini kwake Chukwani wakati akizungumza na Viongozi wa Jumuiya ya nchi za Ulaya ( EU) waliongozwa na Balozi wa Umoja huo hapa nchini Bwa Filiberto Sebregondi.
Kificho ameufahamisha ujumbe huo kwamba, ameridhishwa na ahadi zinazotolewa na wadau wote wa uchaguzi ikiwemo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Viongozi wa vyama vya Siasa na vyombo vya Ulinzi na Usalama kwamba kila kimoja kitatekeleza vyema wajibu wake ili kufanikisha uchaguzi huo kwa njia ya haki, amani na usalama.
“Kila taasisi, tayari imetuhakikishia kwamba itatekeleza wajibu wake na kuondosha vikwazo vyote kwa lengo la kuendesha salama mchakato wote wa Uchaguzi ambao tunaamini utakuwa wa haki na utulivu mkubwa” alisisitiza Spika Kificho.
Aidha spika Kificho ameuhakikishia umoja huo kwamba Serikali zote mbili zitafanya kila liwezalo kuhakikisha kwamba hali ya amani na usalama inaendelea kuwepo wakati na baada ya uchaguzi .
Kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa Spika kificho amesema mfumo huo ambao umekubaliwa na wananchi wenyewe upo kikatiba hivyo Baraza la Wawakilishi litafanya kila liwezavyo kulinda matakwa hayo ya wananchi.
Amesema chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambao ni adimu duniani, maendeleo makubwa ya kisiasa na kiuchimi yamepatikana na umoja wa wananchi unazidi kuimarika hapa Zanzibar.
Amesema Baraza la Wawakilishi la Nane linalomaliza muda wake lilikua la aina yake ambapo chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Wajumbe wasiokua Mawaziri waliibana vyema serikali kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji , suala ambalo lilitoa mvuto mkubwa kwa wananchi kufuatilia mikutano ya Baraza hilo.
Nae Balozi Filiberto Sebregondi amewaomba wadao wote wa uchaguzi kufuata sheria na taratibu zote ili kufanikisha vyema mchakato wote wa uchaguzi huru na wa haki.
Amesema jumuiya ya ulaya kwa kiasi kikubwa inafuatilia mchakato huo na kuwatakia kila la kheri wananchi na hatimae waweze kufuka salama katika uchaguzi huu.
Mwisho.
Imetolewa na
Himid Choko
Afisi ya Baraza la Wawakilishi, Zanziabar,
25 August 2015
0 comments:
Post a Comment