Saturday, January 3, 2015

MKE WA MTU SUMU, KWANINI URUHUSU WATU WAMPE MAZIWA? SOMA MADA YA KUSISIMUA *PICHA*


BILA shaka mpenzi msomaji wa safu hii uko vizuri na ndiyo tunaanza mwaka mpya, 2015 pamoja. Najua kuna malengo ambayo ulipanga kuyafanya mwaka 2014 hayakutimia, yapange upya na hakika kwa uwezo wa Mungu utafanikiwa.

Kama wewe na mpenzi wako mlipanga kufikia hatua ya kutambulishana nyumbani kwa wazazi, kuvalishana pete au hata kuoana na hamjafanikiwa basi mwaka mpya ndiyo huu, bado mnayo nafasi ya kupanga siku au mwezi ambao mnaona unafaa kufanikiwa malengo yenu.

Tukirudi katika mada yetu ya leo, tutapata kujifunza kuhusiana na namna ambavyo wapendanao wanapaswa kutimiza majukumu yao. Iwe ni kwenye uchumba au hata mkiwa tayari kwenye maisha ya ndoa. 

Nitazungumza na wale ambao wako kwenye ndoa lakini hata wale ambao hawapo kwenye ndoa naamini watajifunza kwani kila aliye kwenye uchumba, safari yake hukamilika kwenye maisha ya ndoa. 

Marafiki zangu, mnapoamua kuingia kwenye ndoa lazima mtambue wajibu wenu na changamoto za ndoa. Mnapaswa kutambua kwamba, kama baba una wajibu gani kwa mama na mama hivyohivyo una wajibu gani kwa baba. 

Kuna baadhi ya watu huwa wanashindwa kutimiza majukumu yao na badala yake huruhusu tatizo kwa upande wa pili. Anashindwa kutambua kwamba kama baba ana wajibu wa kuhakikisha mama anapata ‘tiba’ sahihi ya mahabati na kujikuta akiangusha lawama kwa mwenzake. 

Baba anakuwa bize zaidi ya ile ya wahudumu wa ‘customer care’. Kila siku anachelewa kurudi nyumbani na mbaya zaidi akirudi anakuwa amechoka kiasi cha kushindwa hata kufanya tendo la ndoa. Tena wengi wao kati ya wale wanaoshindwa tendo hilo, ndiyo haohao ambao kila kukicha wanawapiga wenza wao pasipokuwa na kosa la msingi. 

Kila kukicha mume anarudi amelewa chakari, anaangusha gari popote. Hiyo ndiyo inakuwa staili ya maisha yako, inakomaa na inadumu hivyo kwa muda mrefu. 

Nini cha kujifunza hapo? Kwa tabia kama hizo, mama anaweza kukuvumilia kwa miezi kadhaa au hata miaka kadhaa lakini ipo siku anaweza kusema; “nimechoka.” 

Hapo ndipo wanapotokea wale watu ambao msemo wa ‘mke wa mtu sumu’ umewapitia kushoto, hawaujui kabisa. Wanageuka suluhisho la maumivu ya mke wako, anampa mkeo tiba ambayo hajawahi kuipata kwa miaka mingi. 

Wanajua kujali, wanajua kuonesha mapenzi utafikiri wameyasomea. Asubuhi mkeo ataulizwa ameamkaje, mchana amekula nini na usiku ataambiwa ‘good night sweet heart’.


Ukishtukia mchezo, unageuka mbogo. Kabla ya kugeuka mbogo kwa nini usiwe makini katika kutimiza majukumu yako hadi wenzio wakusaidie halafu uwalamu? Sihalalishi watu kuchepuka lakini ukweli ni kwamba, kesi nyingi za wanandoa kusaliti husababishwa na mmoja wa wanandoa kutotimiza majukumu yake. 


Kama unahisi kuna tatizo kwa mwenzako, tenga muda mzuri na umueleze ili muweze kupata suluhu ya tatizo husika. Kwa kutumia lugha nzuri, mama anapaswa kumueleza mumewe kama anahitaji haki yake ya ndoa.



Baba anayerekebishwa juu ya tabia fulani, ili kuepuka maafa huko usoni ni vyema ukajitathmini na kufanyia kazi mapungufu yako. Kama baba kuna kitu pia unaona haukipati kwa mkeo na kukusababisha uwe mtu wa kuchepuka na kumsahau mkeo ni vyema pia ukamueleza. 

Mueleze ili naye ajue, ajitathmini na kuona namna anavyoweza kujinasua katika eneo ambalo ana mapungufu. Hakuna haja ya kuficha maradhi. Ukweli ndiyo unaoweza kuwafanya penzi lenu lishamiri.
Kwa leo tuishie hapo, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI