Wednesday, October 15, 2014

VIJIJI 1,800 KUPATA MAWASILIANO YA SIMU MWAKANI

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba (Kulia) akizungumza katika mkutano wa wadau wa teknolojia ya Tehama (Capacity Africa 2014) ambapo amesema serikali itaondoa tatizo la mawasiliano nchini na huku ikitarajia kusambaza huduma hiyo kwa vijiji 1,800 ifikapo mwakani na vijiji 4,000 ikikapo mwaka 2017. Kushoto kwa Naibu Waziri Makamba ni mkurugenzi wa kampuni ya Seacom Byron Clatterbuck na Mwakilishi wa kampuni ya internet solution Prenesh Padayachee.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Six Telecoms, Rashid Shamte akifafanua jambo kuhusiana na maendelea ya teknolojia ya Tehama nchini. Kampuni hiyo ni moja ya wadhamini wa mkutano huo unaofanyika nchini kwa mara ya pili. Kulia ni Ofisa Biashara mkuu wa kampuni hiyo, Tinashe Bgoya.
Afisa Biashara mkuu wa kampuni ya Six Telecoms, Tinashe Bgoya (kushoto) akizungumzia maendeleo ya maendelea ya teknolojia ya Tehama nchini. Kulia ni Saidi Mohmed Alli ambaye ni Mkuu wa kitengo cha ‘Data’ cha kampuni hiyo.
 
 Ofisa Mkuu wa Masoko na Mauzo wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Peter Ngota (Kushoto) akifafanua jambo katika mkutano wa wadau wa mawasiliano ya Tehama ujulikanao kwa jina la Capacity Africa. kampuni hiyo ni moja wa wadhamini wa mkutano huo. Kulia ni Mwakilishi wa kampuni ya internet solution Prenesh Padayachee.
**********
JIJINI Dar es Salaam. Jumla ya vijini 1,800 vinatarajia kupatiwa mawasiliano ya simu ya na teknolojia ya mawasiliano ya habari na mawasiliano (Tehama ) ifikapo mwakani.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa Tehama wa Africa (Capacity Africa), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba alisema kuwa mpango huo upo katika hatua za mwisho na ifikapo mwaka 2017, jumla ya vijiji 4,000 zitakuwa vimepatiwa huduma hiyo.
Makama alisema kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho kuzungumza na kampuni ya simu kutoka Vietnam ijulikanayo kwa jina la Viettel na hivi karibuni wanatarajia kuzindua rasmi mpango huo.Alisema kuwa kuna vijiji mbali mbali Tanzania havina kabisa mawasiliano na jukumu la serikali kuhakikisha kuwa tatizo hilo linatatuliwa. 
Kwa mujibu wa Makamba sekta ya mawasiliano inazidi kukuwa na serikali imeweka mpango maalum kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hiyo tena kwa ubora wa hali ya juu. Alisema kuwa sekta hiyo ina changamoto nyingi kutokana na kupanuka kwa teknolojia ya mawasiliano na tayari serikali imechukua hatua kukabiliana na tatizo hilo hasa baada ya kukamilika kwa hatua ya tatu ya mkongo wa Taifa wa mawasiliano.
“Mpaka sasa ni mkoa wa Simiyu tu haujafikiwa na mkongo wa taifa na hiyo imetokana na kugawanywa kwa mkoa wa Shinyanga, hata hivyo mikakati inafanyika ili kuhakikisha mkoa huo unapata huduma hiyo na kuanza kufurahia huduma ya Tehama,” alisema Makamba.Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Six Telecoms, Rashid Shamte alisema kuwa anaamini kuwa kukamilika kwa mkongo wa Taifa kutanufaisisha nchi jirani ambazo hazina bahari.
Shamte ambaye kampuni yake ilidhamini mkutano wa mwaka 2012 alisema kuwa wanafuraha kubwa kuona nchi inafanya juhudi za kutatua tatizo la mawasiliano vijijini na nchi takribani nane zinazoizunguka Tanzania.
Ofisa Mkuu wa Masoko na Mauzo wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Peter Ngota alisema kampuni yao imeanzisha kitengo cha mtandao wa internet ambacho kitatoa huduma hiyo kwa bei nafuu.
“Lengo letu kubwa ni kurahisisha mawasiliano, hivyo tunawahikikishia kuwa watu wote wanaoishi vijijini watapata huduma hii kwa bei nafuu,” alisema Ngota.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI