Wednesday, October 15, 2014

CHADEMA YAWATAKA WALIMU WASITOE MICHANGO YA MAABARA

Na Mohab Matukio.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), kanda ya Ziwa Victoria Mashariki, kimewataka walimu katika mikoa ya Shinyanga,Simiyu na Mara wasikubali kuchangia shilingi 10,000 kutoka katika mishahara yao kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya sekondari za kata.
Pia Chama hicho kimewataka wafanyabiashara nao wasikubali kulazimishwa kuchangia michango hiyo kwa vile hilo ni jukumu la serikali kuhakikisha inatekeleza ahadi zake katika ujenzi wa maabara kama Chama Cha Mapinduzi kilivyo ahadi katika ilani yake ya uchaguzi. 
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama hicho kanda ya Ziwa Victoria Mashariki, Prof. Silyvester Kasulumbayi, jana alipokuwa akiwahutumbia wananchi wa mji wa Kahama katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Nyihogo mjini humo.
Kasulumbayi ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki (Chadema),alisema,ujenzi wa maabara hayo ni jukumu la serikali iliyoko madarakani na michango kutoka kwa mwananchi yeyote ni wa hiyari,kama ulivyo mchango wa harusi.
Alisema walimu na wafanyabiashara wasikubali kulazimishwa kutoa fedha hiyo kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa maabara,kwa lengo la kutekeleza agizo la wakuu wa wilaya baada ya kuamriwa na Rais Jakaya Kikwete,kukamilisha ujenzi huo ndani ya mwezi wa oktoba.
Akijibu swali la mmoja wa wananchi katika mkutano huo, Kasulumbayi alisema kuwa,inashangaza kuona serikali ya CCM imetumia mabilioni ya fedha kwa ajili ya bunge maalum la Katiba,kwa kuwalipa wajumbe wa bunge hilo,na kutunga katiba isiyo na tija kwa watanzania,na kuwa ingekuwa busara serikali kutumia mabilioni hayo kujenga maabara na siyo kulazimisha michanago kutoka kwa wananchi.
“ndugu zangu walimu,msikubali kuchangia shilingi 10,000,na ninyi wafanyabiashara,hilo ni jukumu la serikali,serikali isingetumia mabilioni ya fedha kwa bunge maalum la katiba na kutunga katiba isiyo na tija, ingetumia fedha hizo kujenga maabara’alisema Kasulumbayi.
Mwenyekiti huyo pia aliwataka wafanyabiashara wasikubali kuchangia michango hiyo kwa lazima,kama inavyoamriwa kwani michango hiyo ni ya hiyari kama michango mingine.
Akizungumzia Katiba mpya Mwenyekiti huyo aliwataka wananchi kutoiunga mkono,na kuwataka walimu kuunga kampeni ya Chadema kuipinga katiba hiyo na kuwataka walimu watumie njia ya simu kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu za kiganjani (SMS),kupinga Katiba hiyo.
Kuhusu uchaguzi ujao Mwenyekiti huyo alisema kuwa,wananchi hawanabudi kuunga mkono UKAWA ambayo wameamua kusimamisha mgombea anayekubalika katika kila eneo husika na kuwa umoja huo utadumu katika changuzi zote kuanzia zile za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao na kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandisha katika daftari la wapiga kura.
Akijibu swali juu ya alama ya bendera ya Chadema kuwa na rangi nyekundu na vidole viwili,Mwenyekiti huyo aliwatoa hofu wananchi juu ya bendera yenye rangi nyekundu kuwa inaashiria hatari na umwagaji damu,na ile alama ya vidole viwili kuwa ni chama cha wezi na kudai kudai kuwa, rangi nyekundu inashiria upendo kwani hata siku ya wapendao duniani ambao watu huvaa nguo nyekundu, na vidole viwili vinavyoelekezwa juu siyo wizi,bali ni alama ya mshikamano na ushindi.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI