MSHAURI maarufu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), ameonya kuwa hali ya ongezeko la watoa huduma za afya waliopata maambukizi ya ugonjwa wa ebola inaweza kuongezeka hata katika nchi zilizoendelea.
Mshauri huyo, Peter Piot alisema hajashangazwa na kitendo cha muunguzi kutoka Spain aliyepata maambukizi ya ugonjwa huo. Muuguzi huyo, Teresa Romero ni mgonjwa wa kwanza kupata maambukizi hayo ambaye anatokea nje ya Afrika Magharibi.
Romero alikumbwa na mkasa huo baada ya kuwahudumia wamisionari wawili kutoka Hispania waliopata maambukizi na kufa jijini Madrid nchini humo.
Muuguzi huyo mwenye umri wa miaka 40 alikuwa ni mmoja wa wajumbe kwenye timu iliyokuwa na wafanyakazi wa afya takribani 30 kutoka hospitali ya Carlos III nchini humo na kutoa huduma ya wamisionari hao ambao ni Manuel Garcia Viejo na Miguel Pajares, waliotokea Sierra Leone na Liberia.
Baada ya kupata maambukizi hayo muuguzi huyo aliwekwa katika eneo la pekee akiwa na mumewe pamoja na familia yake ambapo hata hivyo, mtu anayedhaniwa kuwa rafiki wa muuguzi huyo naye alilazimika kujiunga na familia ya Romero baada ya kuhisiwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Hadi sasa nchini Hispania zaidi ya watu 50 wanahisiwa kupata maambukizi ya ebola na wametengewa eneo maalumu wakiendelea na uchunguzi wa afya zao.
Muuguzi huyo alipozungumza na waandishi wa habari, alibainisha kuwa alifuata taratibu zote zinazotakiwa kujikinga na maambukizi hayo wakati akiwahudumia wagonjwa walioathirika na ebola na kwamba hadi sasa hajafahamu amepataje maambukizi ya ugonjwa huo.
Chanzo: HABARILEO
0 comments:
Post a Comment