Katibu Bodi ya Filamu Bibi Joyce Fisoo akisoma salamu za rambirambi wakati wa kuuaga mwili wa aliyekua mtayarishaji wa filamu nchini George Otieno Okumu “Tyson” katika viwanja vya Leaders’ Kinondoni. Tyson alifariki mwishoni mwa wiki iliyopita kwa ajali ya gari.
NDUGU zangu nashindwa hata niseme nini kutokana na mfululizo wa misiba ya wanatasnia wenzetu, nashindwa kueleza simanzi kubwa niliyonayo, nakosa la kuongea ninabaki kusema kazi ya Mungu haina makosa katika yeye tumeubwa na yote yanayotokea ni kwa mapenzi yake yeye aliye muumba.
Bodi ya Filamu nchini inaungana na wadau wote wa filamu pamoja na familia kufuatia kifo cha ghafla cha mwongozaji mahiri wa filamu ndugu yetu George Otieno Okumu (Tyson) kilichotokea kwa ajali ya gari. Ninatambua wakati mgumu ambao familia yake unao, watoto wake, wanatasnia wote na wafanyakazi wenzake wa TV 1.
Jina George Tyson lipo masikioni mwa watanzania tangu mwanzoni mwa mwaka 2000 na limetambulishwa na umahiri wa kazi alizoziongoza ikiwemo filamu iliyoitwa Girl friend ambayo ilitikisa soko la filamu. Tyson ni miongoni mwa wanatasnia waliotoa mchango mkubwa katika kuinua tasnia ya filamu hapa nchini na katika kuongoza vipindi mbalimbali vya runinga.
Nyote mnakumbuka kundi la Mambo Hayo ambalo ndugu yetu Tyson alikuwa mmoja wa waasisi wakubwa. Wanatasnia wengi walio mahiri hapa nchini wamebahatika kupata fursa ya kufundishwa na Tyson.
Tyson ameweza kutambulisha na kukuza vipaji vingi, kimsingi aliwekeza katika kufundisha makundi mbalimbali ya wanatasnia, alikua mahiri na kwa hakika amechangia katika kukua na kuendeleza tasnia ya filamu nchini.
Ni ukweli usiopingika kuwa msisimko mkubwa miongoni mwa wafanyakazi wa tasnia ya filamu nchini uliongezwa na kazi alizofanya ndugu yetu Tyson. Kuondoka kwake ni pigo kubwa sana kwetu wanatasnia. Daima tutamkumbuka kwa mchango wake, katika kuendeleza juhudi zake nawasihi wanatasnia tuenzi yale yote mema aliyotuachia na tuyaendeleze.
Narudia kutoa pole nyingi na Mungu atupe subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
Daima tumkumbuke na kumuenzi.
MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU GEORGE OTIENO OKUMU (TYSON) MAHALI PEMA PEPONI AMENI.
0 comments:
Post a Comment