Wednesday, May 21, 2014

MAPYA YAIBUKA CHAPA YA NAMBA MIILINI NA KUFARIKI: MUTUKULA WAVAA KAMBA ZA JADI, ROZARI BAADA YA IDADI YA WALIOFARIKI KUFIKIA 3 KWA MADAI YA UGONJWA WA AJABU.

WAKAZI wa mji mdogo wa Mutukula wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, bado wanaishi kwa hofu ya kupigwa chapa ya namba miilini mwao inayosadikiwa kusababisha kifo baada ya kumalizika siku zenye idadi sawa na namba aliyopigwa mgonjwa.
Hadi kufikia sasa watoto 3 wamefariki dunia wakihusisha vifo hivyo na chapa za namba walizokuwa wamepigwa miilini mwao huku Idara ya Afya wilayani humo ikikanusha kuwepo uhusiano wa vifo hivyo na chapa hizo za namba.
Vifo hivyo vya watoto wengine wawili vimefuatia kifo cha mtoto Elizabeth Nantare 13.05.2014 aliyekuwa na umri wa miaka minne (4) aliyefariki baada ya kupigwa chapa ya namba 3 mgongoni.
Idara ya afya wilayani Missenyi, imetoa ufafanuzi kuhusu sababu zilizopelekea watoto 3 kufariki dunia katika mji mdogo huo wa Mutukula na imekanusha uvumi wa wananchi kwamba wamefariki dunia kwasababu yakupigwa namba mwilini kimiujiza.
Afisa afya wa wilaya ya Missenyi Edward Kagari, amesema kuwa baada ya wakazi wa mji mdogo wa Mutukula wilayani humo kutoa taarifa kuwa watoto watatu wamefariki baada ya kupigwa chapa za namba mwilini, madai hayo si sahihi na uchunguzi wa kitabibu unaonesha kuwa wamefariki kutokana na magonjwa ya degedege na malaria.
“Geofrey Godfrey (10), Aiani Ndugwa (21/2) walikufa kwa ugonjwa wa malaria ingawa walikuwa na mabarango ya namba hizo. Mabarango hayo husababishwa na uvimbe mwilini ambao hurundikana sehemu moja na kuonekana kama namba mgonjwa anapojikuna”. Amesema afisa Kagari.
Licha ya kwamba wakazi wa eneo hilo wamezidi kuamini kwamba kupigwa namba kunamsababisha mtu kufariki dunia baada ya kumalizika kwa siku alizopigwa mwilini, Kagari ameshauri watu kutoa taarifa vituo vya afya mara tu wanapoona hali hiyo kwa mgonjwa ili afanyiwe vipimo vya kitibabu.
”Mtu yeyote atakayebainika kuwa na dalili zozote zisizokuwa za kawaida, apelekwe kwenye kituo cha huduma Mutukula ili kubaini madai ya watu ya kuwepo chapa za namba na kifo. Watu wanaongelea tatizo hilo kwa mtu ambaye tayari amefariki hivyo kutuwea vigumu kuthibitisha madai hayo”. Ameongeza afisa Kagari.
Mpaka sasa baadhi ya wakazi wa mji wa Mutukula wanajifunga kamba za jadi sehemu mbalimbali za mwili na wengine wanavaa rozali kwa imani kuwa mtu aliyevaa hivyo hawezi kupigwa namba mwilini zinazoashiria kifo cha mtu huyo.
Baadhi ya watu wenye chapa za namba miilini mwao akiwemo mtoto mwenye umri wa miaka 14 mwenye chapa ya namba 12, wanaendelea kuombewa makanisani ili kunusuru maisha yao, na tayari kuna dalili za chapa za namba hizo kuanza kupotea.
Wakazi hao wanadai kuwa kupigwa chapa ya namba kimiujiza mwilini na mtu kufariki baada ya kuisha siku zenye idadi ya namba ya chata ilianzia nchini Uganda na kuua watu wengi. 
Hata hivyo idara ya afya imesisitiza kuwa wanaobainika kuwa na dalili hizo wapelekwe kwenye vituo vya afya mara moja ili kupata matibabu baada ya kufanyiwa vipimo jambo ambalo bado jamii ya Mutukula inaamini kuwa mtu mwenye chapa ya namba hawezi kupona hospitalini isipokuwa kwa kufanyiwa maombi kanisani na kuvaa kamba za jadi na rozari.

Ni vema mamlaka husika zikachukua hatua ya kutoa elimu kwa wakazi hao ili kuwaondolea hofu waliyonayo kwa sasa.
Na Hilal Ruhundwa, Bukoba.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI