Wednesday, May 21, 2014

SOMA MUHTASARI WA HOTUBA YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015

UTANGULIZI:
1.0        Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja kwamba Baraza lako Tukufu likae kama Kamati ya Mapato na Matumizi ili lipokee, lijadili na hatimae liidhinishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya   Makamu wa Pili wa Rais kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015.

2.0        Mheshimiwa Spika, tumekutana tena katika kikao hiki cha nne cha Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya kuzungumzia mipango na masuala muhimu ya nchi yetu kwa nia ya kuleta maendeleo ya nchi na wananchi wake.  Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uwezo huu wa kukutana tena na ninamuomba aendelee kutupa afya njema na kutuwezesha kuendesha kikao chetu hiki kwa hekima, busara na uadilifu mkubwa. Ni imani yangu kuwa tutamaliza kikao hiki tukiwa tunaendelea kubakia wamoja na wenye mshikamano mkubwa katika kuendeleza nchi yetu.

3.0        Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumshukuru kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuiongoza nchi yetu kwa umahiri na umakini mkubwa.  Sote ni mashahidi kuwa chini ya uongozi wa Dkt.  Ali Mohamed Shein, nchi yetu imeendelea kupata mafanikio makubwa katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa.  Aidha, nchi yetu imeendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu mkubwa hali ambayo imetoa nafasi kwa wananchi kuendelea na shughuli zao za maisha za kila siku bila bughudha wala usumbufu wowote. Namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema na umri mrefu yeye na familia yake, amzidishie hekima na busara ili aendelee kutuongoza katika hatua za kuiletea nchi yetu maendeleo zaidi.

4.0        Mheshimiwa Spika, vile vile, nachukua nafasi hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuendelea kumsaidia na kumshauri vyema Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na  kwa  mashirikiano yake mazuri kwa Ofisi yangu.

5.0        Mheshimiwa Spika, pongezi za pekee nazitoa kwako wewe mwenyewe binafsi Mheshimiwa Spika, kwa jinsi unavyoliendesha Baraza letu hili kwa umahiri na umakini mkubwa kwa kufuata sheria na kanuni za Baraza. Uongozi wako wa busara kwa hakika umeimarisha demokrasia ndani ya Baraza na kulipa Baraza letu mafanikio makubwa katika kutekeleza majukumu yake. Tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akuzidishie uwezo na hekima katika kutekeleza majukumu yako makubwa katika Taifa letu.  Pia napenda kuwapongeza kwa dhati Naibu Spika, Mhe. Ali Abdalla Ali Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini na Wenyeviti wa Baraza Mhe.  Mgeni Hassan Juma, Mwakilishi wa Viti Maalumu na Mhe. Mahmoud Mohamed Mussa, Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni kwa namna wanavyokusaidia katika kuliendesha Baraza letu hili.

6.0        Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii pia kuwashukuru Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa malengo na maagizo mbali mbali wanayoyatoa kwa Wizara wanazozisimamia. Aidha, natoa shukrani maalum kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Mhe. Hamza Hassan Juma, Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, Makamu Mwenyekiti, Mhe. Saleh Nassor Juma Mwakilishi wa Jimbo la Wawi na Wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa kuyapitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na kutupa ushauri unaotuongoza na kutusaidia katika utekelezaji wa malengo na majukumu ya Ofisi yetu.

7.0        Mheshimiwa Spika, pia nawapongeza Wajumbe wote wa Baraza hili Tukufu kwa kuipitisha Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Bajeti hiyo ndiyo itakayotuwezesha kuendesha kazi za Serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015.

8.0        Mheshimiwa Spika, maelezo ninayoyasoma hapa ni muhtasari wa hotuba yangu iliyomo katika kitabu changu cha hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015 kilichowasilishwa katika Baraza hili. Aidha, naomba maelezo yaliyomo katika kitabu hicho cha bajeti yaingie katika hansard kama yalivyo.

HALI YA SIASA:
9.0        Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijaalia nchi yetu amani na utulivu. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 hakukua na matukio makubwa ya uvunjifu wa amani yaliyotokea katika nchi yetu. Hali hii inatokana na wananchi wengi kuzidi kuelewa umuhimu wa amani na kushirikiana na Serikali yao kudumisha amani na utulivu kwa maendeleo ya Taifa letu na Ustawi wa jamii.  

10.0     Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, nchi yetu imefanya chaguzi ndogo mbili (2) ambazo zilihusisha Uchaguzi wa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Wilaya ya Magharibi Unguja na Uchaguzi wa Diwani Wadi ya Kiboje, Wilaya ya Kati Unguja. Tunavishukuru vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika chaguzi hizo ambazo ziliendeshwa kwa haki, uwazi, amani na utulivu mkubwa. Aidha, tunawapongeza sana viongozi walioshinda katika chaguzi hizo na tunawatakia mafanikio katika kuwatumikia wananchi waliowachagua na nchi yetu kwa ujumla. Vile vile, nachukua nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza sana wananchi wa Jimbo la Kiembesamaki  na wananchi wa Wadi ya Kiboje kwa kuweza kutumia demokrasia yao vizuri kuwachagua viongozi wao kwa imani ya kuwaletea maendeleo katika maeneo yao.

MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR:
11.0     Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha, nchi yetu imeadhimisha Miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Maadhimisho ya Sherehe hizo yalizinduliwa rasmi tarehe 15 Agosti, 2013 na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein na kufikia kilele chake tarehe 12 Januari, 2014, Uwanja wa Amani, Zanzibar.

12.0     Mheshimiwa Spika, kwa muda wote wa maadhimisho haya hadi siku ya kilele tumeshuhudia shughuli na matukio mbali mbali ambayo wananchi na viongozi walishiriki kikamilifu katika maeneo yote ya Unguja na Pemba. Miongoni mwa matukio hayo ni Maonesho ya Miaka 50 ya Mapinduzi yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), Kampasi ya Beit el Ras kuanzia tarehe 2 – 5 Januari, 2014; Maonesho ya Fensi; Maonesho ya Biashara yaliyofanyika katika viwanja vya Maisara; Utoaji wa Nishani kwa viongozi na wananchi mbalimbali waliotoa mchango wao katika Mapinduzi ya Januari 12, 1964 pamoja na waliochangia katika maendeleo ya Zanzibar kwa jumla.  Pia palifanyika Matamasha ya Michezo na Burudani, Ujenzi wa Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Michenzani, Uwekaji wa jiwe la msingi na uzinduzi wa miradi ya maendeleo mbali mbali.  Na mwisho maonesho mbali mbali yaliyofanywa siku ya kilele katika Uwanja wa Amani.

13.0     Mheshimiwa Spika, sote ni mashahidi wa namna sherehe zetu hizi zilivyokuwa zimefana sana na kuleta haiba kubwa kwa nchi yetu. Hii imeonesha jinsi gani wananchi wetu wanavyoyathamini Mapinduzi yetu ya Januari 1964 pamoja na maendeleo wanayoyaona kutokana na Mapinduzi hayo.

14.0     Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako napenda kutoa pongezi na shukurani zangu za dhati kwa wananchi na viongozi wote walioshiriki kwa njia moja au nyengine katika kufanikisha Maadhimisho ya Sherehe hizo. Ni matumaini yangu kuwa sote kwa umoja wetu tutaendelea kudumisha Mapinduzi haya ili kuendeleza amani na maendeleo katika nchi yetu.

15.0     Mheshimiwa Spika, pamoja na kutoa pongezi hizo, naomba kutoa masikitiko yangu kuona kwamba hadi leo hii wapo watu wachache miongoni mwetu ambao wanauliza uhalali wa Mapinduzi Matukufu ya Mwaka 1964. Ni dhahiri kwamba hata hawa wanaohoji uhalali wa Mapinduzi kwa kiasi kikubwa wamefaidika na Mapinduzi haya.  Mwenye macho haambiwi tazama kwani ni baada ya Mapinduzi ya 1964 ndio nchi hii imeshuhudia mafanikio makubwa ya maendeleo katika nyanja zote. Hivyo, hatuna budi kuyalinda na kuyaendeleza Mapinduzi yetu kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo.

16.0     Mheshimiwa Spika, dhana ya Mapinduzi ilikuwa ni kuleta maisha bora kwa kila Mzanzibari na kuondoa ubaguzi wa aina zote na kuleta umoja na maendeleo na ndio kilichofanyika. Haya mengi ambayo leo tunayaona hayakuwepo kabla ya Mapinduzi ambayo ni pamoja na kuwepo kwa nyumba bora za kuishi, nyumba bora kwa wazee, kuimarika kwa huduma za elimu, afya na kupatikana kwa maendeleo makubwa katika Sekta ya Miundombinu, Kilimo, Maji na Umeme, Uchumi na Biashara, na kuwepo kwa uhuru wa kushiriki shughuli za kisiasa.

17.0     Mheshimiwa Spika, naomba tuelewe kwa nini tunatoa kipaumbele katika kuweka kumbukumbu za Mapinduzi hasa katika maadhimisho yake. Kwa kweli ni jambo la ajabu kuona miongoni mwetu bado wapo watu wanaohoji umuhimu wa Sherehe za Mapinduzi au kuweka vielelezo vya Mapinduzi. Tunasema tutaendelea kuenzi na kuheshimu kazi nzuri iliyofanywa na Wazee wetu ya kutukomboa na kutupatia Uhuru wa nchi yetu.

18.0     Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya kuweka kumbukumbu ya kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi, Serikali kwa makusudi imefanya uamuzi wa kujenga Mnara katika eneo la Michenzani. Hii inatokana na historia ya eneo hilo katika harakati za kuikomboa nchi yetu. Aidha, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuendeleza azma ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kuendeleza eneo hilo na kulifanya kuwa eneo la biashara na kuwa kivutio kwa wageni, watalii na wananchi kwa ujumla.

19.0     Mheshimiwa Spika, mnara unaoendelea kujengwa utakuwa pia ni kituo kwa wananchi na wageni kusoma historia ya Mapinduzi na waanzilishi wake kwani kutakuwa na maktaba maalum. Katika eneo hilo kutakuwa na mkahawa na bustani ya mapumziko ambayo itasaidia sana kupunguza msongamano katika maeneo ya Forodhani hasa wakati wa sikukuu. Naomba wananchi waelewe kuwa mnara huo unajengwa kwa fedha za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) na utaendeshwa kibiashara na kwa faida.

MASUALA YA MUUNGANO:
20.0     Mheshimiwa Spika, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hivi sasa umetimiza miaka 50 (Nusu Karne) tangu ulipoasisiwa tarehe 26 Aprili, 1964. Sherehe za kutimiza miaka 50 ya Muungano wetu zilizinduliwa rasmi hapa Zanzibar na Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 01 Machi, 2014 katika Ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani na kilele chake kilifanyika Dar es salaam tarehe 26 Aprili, 2014.  Kipindi cha miaka 50 ni kirefu na nchi yetu ina kila sababu za kujivunia kutokana na kuudumisha Muungano wetu kwa kipindi chote hicho. Yapo mafanikio mengi yanayotokana na Muungano, lakini makubwa kati ya mafanikio hayo ni kuwa na amani na utulivu katika nchi yetu. Aidha, Muungano huu umeweza kutoa fursa ya kuendeleza na kuimarisha mahusiano ya kidugu yaliyopo kati ya wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.

21.0     Mheshimiwa Spika, licha ya kuwa na mafanikio hayo, Muungano wetu huu umekuwa na changamoto katika baadhi ya maeneo ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele na wananchi wa pande zote mbili za Muungano.  Juhudi kubwa tayari zimechukuliwa na viongozi wetu katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo ili kuimarisha Muungano wetu huu wa kihistoria. Mambo ambayo mpaka sasa yameshapatiwa ufumbuzi kupitia Kamati Maalumu inayoongozwa na Mhe. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kama yafuatayo:-

·         Utekelezaji wa Sheria ya Haki za Binaadamu.
·         Utekelezaji wa “Merchant Shipping Act” katika Jamhuri ya Muungano na uwezo wa Zanzibar kujiunga na Shirika la Kimataifa la Usafiri Baharini [International Maritime Organisation (IMO)].
·         Misamaha ya mikopo ya fedha kutoka IMF.
·         Uwezo wa Zanzibar kukopa ndani na nje nchi.
·         Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo wa SMT.
·         Kodi ya Mapato (Mgao wa Mapato yatokanayo na PAYE).

22.0     Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo ambayo yameshapatiwa  ufumbuzi  kuna mambo ambayo yapo katika hatua nzuri ya kupatiwa ufumbuzi,  mambo hayo ni kama yafuatayo:-
·         Mgawanyo wa mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
·         Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
·         Ushirikiano wa Zanzibar na Taasisi za nje.
·         Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano.
·         Usajili wa vyombo vya moto.
·         Tume ya Pamoja ya Fedha.
·         Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

MASUALA YA KIUCHUMI NA KIJAMII:
23.0     Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu hii nimegusia masuala mbali mbali ya kiuchumi na kijamii ikiwemo hali ya uchumi na mipango ya Serikali katika kuimarisha uchumi, uwezeshaji wananchi kiuchumi, Sekta ya huduma ya kiuchumi, Sekta ya huduma ya kijamii, masuala ya migogoro ya ardhi, masuala mtambuka pamoja na Sekta ya utumishi na maslahi ya wafanyakazi. Masuala haya yameelezwa kwa kina kuanzia ukurasa 12 mpaka ukurasa wa 24 katika hotuba ya makadirio.


MWELEKEO WA VIPAUMBELE VYA OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015:
24.0     Mheshimiwa Spika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais katika kutekeleza majukumu yake katika mwaka wa fedha 2014/2015 imejipangia kutekeleza vipaumbele vifuatavyo:-

         i. Kuimarisha huduma za usafiri na makaazi ya Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais.
        ii. Kuongeza hadhi katika Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa.
       iii. Kujenga uwezo wa kiutendaji kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa kuwapatia mafunzo na vitendea kazi.
       iv. Kujenga uwezo wa jamii katika kujikinga, kukabiliana na kuhimili majanga na maafa.
        v. Kushughulikia malalamiko na migogoro ya wananchi kwa kushirikiana na Sekta husika.
       vi. Kusimamia masuala ya utafiti kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa vya Utafiti (National Research Agenda).
     vii. Kuweka Muundo mpya wa Kitaasisi na Kiutumishi wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Dar es Salaam utakaoongeza ufanisi na tija.
    viii. Kuongeza mapato yatokanayo na kuongezeka kwa huduma za upigaji chapa.
       ix. Kuandaa mazingira bora kwa ajili ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa 2015, ikiwemo kutoa elimu ya wapiga kura, kufanya uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya majimbo na kufanya mapitio ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, na
        x. Kuendesha mikutano ya Baraza la Wawakilishi na kusimamia kazi za Kamati za Kudumu za Baraza.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI