Thursday, April 3, 2014

WEMA SEPETU ALIVYOZIVAMIA OFISI ZA GLOBAL PUBLISHERS KUTOKANA NA STORY YA "DIAMOND ATAMANI USHOGA"

Wema Isaac Sepetu aliyekuwa Miss Tanzania 2006, amejitoa fahamu kwa kupandisha mzuka na kutinga makao makuu ya Kampuni ya Global Publishers, Bamaga-Mwenge, Dar na kuzua timbwili la aina yake kisa kikiwa ni kuandikwa kwa habari zake na mpenziwe, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Tukio hilo la kumchoresha staa huyo mwenye vituko kila kukicha, lilijiri Jumatatu iliyopita kwenye ofisi za Global ambao ni wachapishaji wa gazeti hili (Amani), Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Championi na Risasi majira ya mchana kweupe hivyo kufunga mtaa huku wapita njia wakimzodoa kwa maneno ya kejeli.

Akiwa na kundi la wapambe dhaifu na goigoi wakiongozwa na meneja wake, Martin Kadinda waliosimama nje ya ofisi hizo, Wema alifika kwa upole akionekana mkarimu kwa mlinzi ambapo aliomba kuonana na mwandishi nguli wa magazeti pendwa, Imelda Mtema.
Mlinzi alimruhusu kwa vile Global ni mjengo wa mastaa na watu wasio mastaa, huwa hawakauki kuingia na kutoka kwa mambo mbalimbali.
Wema alipofika mapokezi, pia aliomba kuonana na mwandishi huyo lakini tofauti na utaratibu ambapo huwa mgeni akifika huulizwa kama ana ‘apointimenti’ ili aitiwe anayemhitaji, Wema alipitiliza kwa nguvu hadi chumba cha habari akifuatana na kijana aliyekuwa akimrekodi.
            
Akiwa ndani ya chumba cha habari, Wema aliuliza kwa sauti ya juu na ya kujiamini: “Imelda yupo wapi? Nauliza Imelda yupo wapi?

Katika kumtafuta Imelda kwa macho kwa sababu chumba cha habari ni kikubwa huku akionywa na wahariri kwamba atulize mzuka kisha aeleze shida yake, Wema alimuona Imelda akitoa maelezo kwa Mhariri Kiongozi wa Magazeti Pendwa ya Global, Oscar Ndauka kuhusu habari aliyokuwa ameifuatilia. 
Cha kushangaza, Wema alimfuata Imelda mpaka kwenye meza ya mhariri huyo kisha kuanza kufoka kwa sauti ya juu.
Kwa nini mnafuatilia maisha yangu? Kila siku mnaniandika na Diamond. Kwa nini Imelda unaniandika kuwa mimi msagaji?”
Katika kuhoji huko, mhariri kiongozi alijaribu kumtuliza Wema ambaye alikuwa kama amewehuka: ”‘Wema tuelewane, eleza shida yako kwa utaratibu kwani hakuna ofisi isiyokuwa na utaratibu.” 
Pamoja na kuambiwa hivyo bado Wema aliyekuwa ameshika Gazeti la Ijumaa Wikienda toleo la Jumatatu iliyopita, aliendelea kumng’ang’ania Imelda ambaye alikuwa akijaribu kumtuliza: 
Wema twende tukakae pale kwenye meza ya mkutano uwaeleze viongozi wangu tatizo lako. Hiyo stori kuwa wewe ni msagaji mbona haipo, ni gazeti gani?”
Licha ya kupewa mwongozo huo, Wema aliendelea kufoka: “Hivi mnajua mimi ni chizi? Kwa taarifa yenu mimi ni chizi zaidi ya machizi wote, ohooo!
Baada ya hali kuwa tete, mlinzi wa geti kuu alipigiwa simu ya mezani na kujulishwa juu ya Wema kusababisha kazi kusimama ambapo alifika haraka tayari kwa kumtoa nje kwa hiyari yake au lazima. 
Ndipo kukatokea timbwili kubwa, wapambe wake ‘goigoi’ nao waliingia wakitaka kufanya vurugu ili kumteka mwandishi huyo lakini kikosi imara cha Global kikiongozwa na Mhariri Kiongozi wa Magazeti ya Championi, Saleh Ally kilijiimarisha na kutuliza fujo hizo huku kikiwa makini kuhakikisha Wema na timu yake hawajeruhiwi hata kidogo.

Katika purukushani hiyo, Wema alionesha udhaifu wa kumudu varangati pale alipotumia gazeti aliloshika kumpiga nalo mwandishi Imelda, jambo lililodhibitiwa kama Waasi wa M23 wa Kongo walivyodhibitiwa na Majeshi ya Umoja wa Mataifa, akatolewa nje.
Ukiachia mbali Wema kutulizwa kwa kutolewa nje kwa nguvu, vijana wake walegevu nao waliwekwa chini ya himaya ya Global kwa kunyang’anywa  kamera ya video iliyokuwa ikitumika kuchukua matukio huku nao wakipigwa picha za kutosha na wapiga picha wetu.
Nje ya ofisi, ‘vita’ kubwa kati ya Wema na walinzi wa Global (alifika mwingine kutoka lindo la mbali) ilizuka ambapo staa huyo alivua vile viatu vyake virefu vya rangi ya bluu bahari na kuanza kumpiga navyo mmoja wa walinzi hao akiamini anamkomesha lakini pia akadhibitiwa!
Wema akiwa ameshika viatu vyake vya mchuchumio mkononi baada ya kutolewa nje ya ofisi na wapambe wake akiwemo meneja wake, Martin Kadinda (kulia)
Wema akiwa anarandaranda kwenye geti kuu akiwa peku, alidondosha matusi ya nguoni ambayo hayaandikiki gazetini kwa namna yalivyokuwa makali. Ilikuwa si rahisi kuamini kuwa yeye ni kioo cha jamii. 
Timbwili la Wema na wapambe wake akiwemo Petit Man, ambao hawakufua dafu kwa walinzi na vijana wa Global nje ya ofisi hizo, lilichukua zaidi ya nusu saa huku likikusanya kadamnasi na kusababisha mtaa kujifunga wenyewe.

Hata hivyo, uongozi wa Global uliwasiliana na Polisi wa Kituo cha Kijitonyama ‘Mabatini’, Dar ambao walifika na kumkuta Wema na timu yake wakiwa wamepoa mlangoni, wakaambiwa timbwili limetulia hivyo wakatimua zao.

Baadaye Wema aliomba kupewa kamera yake ambapo zoezi hilo lilifanyika lakini ‘memori kadi’ yenye picha walizoanza kurekodi, ilitolewa ili kupisha maridhiano kwanza. Waliambiwa kadi hiyo ilitolewa kwa sababu walirekodi bila idhini au kibali cha Kampuni ya Global.
Baada ya kugundua kadi ya kamera ipo chini ya ulinzi wa Global, Wema alitaka kulianzisha tena akidai hawezi kuondoka hadi apewe kadi hiyo lakini uongozi uliweka ngumu. Baadaye aliondoka kimyakimya. Wakati huo wapambe wake walishaondoka kitambo.

Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, kadi ya kamera hiyo bado ilikuwa inashikiliwa na uongozi wa Global ili kumthibitishia Wema kuwa hawezi kufanya umafia wowote dhidi ya waandishi wa kampuni hiyo yenye nguvu kihabari nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Wema, magazeti ya Global yamekuwa yakimwandika vibaya yeye na mpenzi wake Diamond huku akitolea mfano wa habari iliyomhusu yeye na mwigizaji Aunt Ezekiel baada ya kunaswa kwa picha zao zilizoashiria vitendo vya usagaji.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI