WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, amesema, si makosa raia wa Tanzania kuhofia majeshi ya ulinzi kuchukua nchi ikiwa muundo wa Muungano wa serikali mbili ukibadilishwa na kuwa serikali tatu.
Aidha, amesema pia ana hofu kuhusu mwenendo wa CUF unaoshirikiana kisiasa na Taasisi ya kidini ya Uamsho, inayotekeleza majukumu yake Zanzibar kwamba umelenga kuua Muungano na kuhatarisha amani kwa mgongo wa dini ya Kiislamu.
Lukuvi alisema hayo bungeni, alipotoa ufafanuzi wa kauli zake alizozitoa katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma wakati wa Ibada ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa Askofu wa Kanisa hilo.
Kauli hiyo ndio iliyodaiwa na Ukawa kuwa moja ya sababu ya kutoka nje ya Bunge kususia kikao.
Madai mengine ya Ukawa yalikuwa ni ubaguzi, matusi na vitisho vinavyoendelea bungeni. Katika ufafanuzi wake Lukuvi alisema kwamba mfumo wa serikali tatu unaweza ukasababisha nchi kupinduliwa na Jeshi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaweza ikaongozwa na CUF kwa Sera za Kikundi cha Uamsho jambo linalompa hofu ya udini na kuvunjika kwa amani.
Lukuvi ambaye jana alilazimika kukatisha safari yake ya kwenda India kwa matibabu, alisema alichoeleza katika hafla hiyo ya kumsimika Askofu ni hofu zake binafsi kuhusu muundo wa serikali tatu.
“Wote nikiwauliza hapa uamsho ni nani mtasema ni CUF, kwa nini sasa nisiwe na hofu ya kidini wakati kuna chama cha siasa ambacho kinamiliki taasisi inaitwa Uamsho lakini ina ladha ya kidini, hizo ndizo sera zao, unakuwaje na chama cha siasa kinachojipanga kutawala Zanzibar lakini kinaendeshwa na sera za Uamsho?
“Wanachosema CUF ndicho wanachosema Uamsho, wakisema serikali tatu ngangari, wakisema serikali ya mkataba sawa kabisa, wapi umeona vikundi kama hivyo, ukiona chama kinajitayarisha kuchukua madaraka na kinatumia taasisi hii kueneza sera zake ni hatari kwa mustakabali wa nchi,” alisema.
Akizungumzia hofu ya nchi kupinduliwa, Lukuvi alisema katika muundo wa Serikali tatu, Rais wa shirikisho hawezi kuwa Amiri Jeshi Mkuu, kutokana na kutokuwa na vyanzo vya mapato hivyo haiwezi kuendesha vyombo vya dola kama Jeshi na Polisi ambao mara nyingi bajeti zao ni kubwa na hazijawahi kutosha hata katika serikali mbili za sasa.
“Kwa mfumo huu wa serikali tatu, tusiwatafute sababu wanajeshi wetu, mimi nilishasema sitashiriki kutafuta vyanzo kwa serikali ya tatu badala yake naukataa muundo huu,” alisema Lukuvi na kuongeza kuwa katika ukosefu mkubwa wa mapato, majeshi yahawezi kuvumilia lazima kutokee uasi na hiyo ndio hofu yake
0 comments:
Post a Comment