Thursday, April 10, 2014

WAZIRI MEMBE ALIVYOPOKEA TUZO YA RAIS JAKAYA KIKWETE WASHINGTON DC MAREKANI

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe, akimsikiliza mwendesha shughuli Lady Kate Atabalong Ndi, Kamishna Masuala ya Afrika wa Gavana wa jimbo la Maryland nchini marekani kabla ya  kupokea  Tuzo la Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi Katika Maendeleo ya Bara la Afrika kwa mwaka 2013 kwa niaba ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika  sherehe ya kutunuku Tuzo hiyo kwenye Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C., usiku wa Jumatano, Aprili 9, 2014. Kushoto ni Naibu Spika Mhe Job Ndugai ambaye yuko katika ziara ya kikazi nchini Marekani, ambapo alialikwa kuhudhuria hafla hiyo. Nyuma yake ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe Liberata Mulamula.
Balozi wa Nigeria nchini Marekani Profesa Adebowele Adufye, akiongea machacha kabla ya  kumkabidhi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe Tuzo la Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi Katika Maendeleo ya Bara la Afrika kwa mwaka 2013 kwa niaba ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika  sherehe ya kutunuku Tuzo hiyo kwenye Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C., usiku wa leo, Jumatano, Aprili 9, 2014. Kushoto ni Naibu Spika Mhe Job Ndugai ambaye yuko katika ziara ya kikazi nchini Marekani, ambapo alialikwa kuhudhuria hafla hiyo. Kulia kwake  ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe Liberata Mulamula.
 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe akimshukuru Balozi wa Nigeria nchini Marekani Profesa Adebowele Adefuye baada ya kupokea Tuzo la Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi Katika Maendeleo ya Bara la Afrika kwa mwaka 2013 anayopokea kwa niaba ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika  sherehe ya kutunuku Tuzo hiyo kwenye Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C., usiku wa , Jumatano, Aprili 9, 2014.
 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe akimpa Naibu Spika Mhe Job Ndugai  Tuzo la Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi Katika Maendeleo ya Bara la Afrika kwa mwaka 2013 aliyopokea kwa niaba ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika  sherehe ya kutunuku Tuzo hiyo kwenye Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C., usiku wa , Jumatano, Aprili 9, 2014.
 Naibu Spika Mhe Job Ndugai akifurahia Tuzo la Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi Katika Maendeleo ya Bara la Afrika kwa mwaka 2013 aliyopewa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika  sherehe ya kutunuku Tuzo hiyo kwenye Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C., usiku wa , Jumatano, Aprili 9, 2014.
 THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tuzo ya Rais Kikwete yakadhibiwa Washington
Apokea Waziri Bernard Membe kwa niaba katika sherehe ya kuvutia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa leo, Jumatano, Aprili 9, 2014, ametunukiwa Tuzo ya Utumishi Bora wa Umma Barani Afrika katika sherehe kubwa iliyofanyika kwenye Hoteli ya St. Regis kwenye mji mkuu wa Marekani wa Washington.

Tuzo hiyo ambayo imepokelewa, kwa niaba ya Rais Kikwete, na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe imetolewa na jarida maarufu la kimataifa la African Leadership Magazine kwa Rais Kikwete kwa kuwa “Kiongozi wa Afrika aliyetoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya kiuchumi ya wananchi wake kwa mwaka 2013.”
Pamoja na Rais Kikwete, Waafrika wengine ambao wamepewa heshima kwenye sherehe hiyo ni Dkt. Kingsley Moghalu, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Nigeria na Bwana John Kennedy Opara, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mahujaji Wakristo wa Nigeria ambaye pia ni mshauri wa Rais Gooluck Jonathan wa nchi hiyo kuhusu mahusiano ya kidini nchini Nigeria.

Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Mheshimiwa Membe, kwa niaba ya Rais Kikwete, na Balozi wa Nigeria katika Marekani, Profesa Ade Adefuye ambaye naye ametoa Tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Jonathan ambaye, kama alivyo Rais Kikwete, hakuweza kuhudhuria sherehe hiyo ya kuvutia.
Jarida la African Leadership Magazine ambalo huchapishwa mjini London, Uingereza na mjini Washington, lilimchagua Rais Kikwete kushinda Tuzo hiyo kwa mwaka 2013 baada ya wasomaji na wadau wake wengine wa Jarida hilo kuwa wamemchagua kwa njia ya kura ya maoni Rais Kikwete kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya wananchi wake katika Bara la Afrika. Rais Kikwete anamfuatia Rais wa Sierra, Mheshimiwa Ernest Bai Koroma, ambaye alishinda Tuzo hiyo mwaka 2012.

Awali, Rais Kikwete alikuwa akabidhiwe Tuzo hiyo tokea Desemba mwaka jana, lakini kutokana na kuingiliana kwa shughuli za Rais, sherehe hiyo iliahirishwa hadi mwaka huu.
Akizungumza kabla ya kukabidhi Tuzo hiyo kwa Mheshimiwa Membe, Balozi Adefuye wa Nigeria katika Marekani amemwelezea kwa undani anavyomfahamu Rais Kikwete akisisitiza kuwa kiongozi huyo wa Tanzania ni kielelezo cha rika jipya la viongozi wa Afrika ambao dira na visheni yao ni maendeleo ya Bara la Afrika na wananchi wake.
“Kwa niaba ya Nigeria, kwa niaba ya Bara la Afrika, nawasilisha kwenu Mwafrika wa wakati huu, mtoto maarufu wa Tanzania na mtoto maarufu wa Bara la Afrika – Rais Jakaya Mrisho Kikwete,” amesema Dkt. Adefuye katika sherehe iliyotangazwa na kuonyeshwa moja kwa moja na mitandao mbali mbali ya kijamii duniani.
Sherehe hiyo imehudhuriwa na watu mbali mbali mashuhuri wakiwamo baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Marekani, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai ambaye yuko Washington kwa shughuli za kikazi, Mwakilishi katika Bunge la Wawakilishi wa Jimbo la Georgia katika 
Marekani, Bi. Dee Dawkins
Haigler ambaye pia ni mwenyekiti wa wabunge weusi katika Bunge hilo na Balozi wa Tanzania katika Marekani Mheshimiwa Liberata Mulamula.
Aidha, akizungumza katika hotuba yake ya utangulizi mwanzoni wa sherehe hiyo, Mchapishaji wa Jarida la African Leadership Magazine, Dkt. Ken Giami ameeleza jinsi Rais Kikwete alivyochaguliwa kwa kishindo na wasomaji na wadau wengine wa Jarida hiyo kutokana na mafanikio yake katika uendeshaji na utawala bora wa Tanzania pamoja na mafanikio yake katika ustawi wa kiuchumi wa wananchi wa Tanzania wakati wa kipindi chake cha uongozi.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
9 Aprili, 2014

 *Membe: Hakuna maendeleo bila kushirikiana na sekta binafsi
TANZANIA itaendelea kufanya jitihada kubwa na kwa hakika itakufa ikijaribu kuimarisha ushirikiano wa karibu zaidi kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, kama njia bora zaidi ya kuleta na kudumisha maendeleo endelevu ya kiuchumi nchini.
Aidha, Tanzania imesisitiza kuwa nchi za Afrika ni lazima ziendelee kutafuta namna ya kumaliza migogoro na mizozo yake ya kisiasa na kijeshi, kama msingi mkuu wa kutafuta na kupata maendeleo endelevu na ya kudumu ya kiuchumi kwa watu wake.
Hayo yameelezwa usiku wa leo, Jumatano, Aprili 9, 2014 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe, wakati alipopokea Tuzo la Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi Katika Maendeleo ya Bara la Afrika kwa mwaka 2013 ambalo ametunikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Akizungumza katika sherehe ya kutunuku Tuzo hiyo kwa Mheshimiwa Rais Kikwete kwenye Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C., Mheshimiwa Membe amesema kuwa uzoefu wa Tanzania unaonyesha kuwa ushirikiano na uhusiano wa karibu kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ni msingi mkuu wa maendeleo ya nchi yoyote, ikiwamo Tanzania.
Amesema kuwa ushirikiano kati ya sekta hizo mbili umeleta manufaa na faida kubwa katika maendeleo ya Tanzania katika sekta za huduma za jamii na katika huduma za kiuchumi.
Waziri Membe amesema kuwa mifano ya mafanikio ya ushirikiano kati ya sekta hizo mbili ni wazi katika sekta kama ya elimu ambako Tanzania imefanikiwa kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia katika usajili wa watoto kuingia shule na katika kuleta usawa katika watoto wa kike na kiume wanaoandikishwa kuanza shule kwa sababu Sekta Binafsi inasaidiana na Sekta ya Umma katika kuwekeza katika elimu.
“Kwa sababu ya ushirikiano huo wa karibu, sisi katika Serikali, tumefanya uamuzi kwamba mikopo ya wanafunzi isitolewe kwa wananchi wanaosoma kwenye vyuo vya umma pekee bali kwa wanafunzi wote wakiwamo wale wanaosoma katika vyuo vikuu binafsi. Hivyo, uhusiano kati ya sekta hizo mbili umeleta mafanikio makubwa katika sekta hiyo ya elimu,”amesema Mheshimiwa Membe.
Waziri Membe pia ametaja mafanikio makubwa yaliyopatikana katika maeneo mengine ya maendeleo kwa sababu ya ushirikiano huo yakiwemo ya utunzaji wa mazingira, usambazaji wa huduma ya maji safi na salama, uboreshaji wa huduma za afya, maendeleo ya miundombinu hasa ya barabara na uboreshaji wa huduma katika kilimo.
Aidha, Waziri Membe amezungumzia hatua zinazochukuliwa na Serikali kuleta uwazi na usimamizi mzuri katika sekta ya gesi hata kabla ya Tanzania haijaanza kuchimba gesi akisisitiza kuwa bila uwazi sekta hiyo itagubikwa na utawala duni, rushwa na usimamizi dhaifu.
 Kuhusu umuhimu wa amani kama sharti la Maendeleo ya Afrika, Waziri Membe amesema kuwa uzoefu wa Afrika na dunia nzima unaonyesha kuwa hakuna maendeleo yoyote na hasa ya kiuchumi bila kuwepo na amani.
Wakati huo huo, Waziri Membe amekutana na kufanya mazungumzo na Gavana wa Jimbo la Maryland, Mheshimiwa Mark O’Malley katika mazungumzo yaliyofanyika kwenye Hoteli ya St. Regis mjini Washington, Marekani.
Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Membe amemwalika Gavana O’Malley kutembelea Tanzania na kutumia nafasi yake kuhakikisha kuwa Jimbo la Maryland linaanzisha ushirikiano na mkoa mmojawapo wa Tanzania.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI