Wednesday, March 26, 2014

TASWA YAKUTANA YAJADILI TAREHE YA KUTOA TUZO ZA WANAMICHEZO BORA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KAMATI ya Kusimamia Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania zinazotolewa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) ilikutana Dar es Salaam juzi na kukubaliana masuala mbalimbali juu ya kuboresha tuzo hizo. 
Tarehe ya Tuzo
Kamati imepanga kuwa tuzo hizo zifanyike Juni 27, 2014 jijini Dar es Salaam katika ukumbi utakaotangazwa kwa ushirikiano wa Kamati ya Tuzo na Kamati ya Utendaji ya TASWA.
Tayari Kamati ya Tuzo na Kamati ya utendaji ya TASWA, zimeanza juhudi za pamoja za kuzungumza na wadhamini mbalimbali wakubwa na wadogo kwa nia ya kufanikisha tuzo hizo katika tarehe iliyopangwa na kuna muelekeo mzuri kuhusiana na suala hilo.

Watakaopewa Tuzo
Kamati yetu kwanza inawaomba radhi viongozi wa vyama vyote vya michezo kutokana na tuzo kushindwa kufanyika mwaka jana na hilo kwa mujibu wa taarifa ya uongozi wa TASWA iliyowasilishwa kwenye kikao chetu, ilitokana na sababu mbalimbali lakini kubwa ni kujitoa dakika za mwisho kwa baadhi ya kampuni zilizokuwa zimethibitisha kudhamini tuzo hizo.
Hata hivyo tunawaomba tuendelee kushirikiana nao mwaka huu na kwa kuanzia tutawatumia barua rasmi za kuomba majina ya wanamichezo wao waliofanya vizuri kuanzia Januari 2013 hadi Aprili mwaka huu, ambapo matarajio yetu wanamichezo wasiopungua 40 watapewa tuzo.

Ujumbe wa Tuzo
Pia kamati imeamua kwamba kila mwaka tuzo hizo zitakuwa na ujumbe maalum kwa wanamichezo, ambapo kwa kuanzia tuzo za mwaka huu ujumbe wake utakuwa ni: ‘Wanamichezo Tupige Vita Ujangili’.
Tunaamini wale wote wataowania, wale watakaoshinda tuzo hizo na wanamichezo wote wakiwemo waandishi wa habari za michezo tutashirikiana na jamii kwa ujumla kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha vita dhidi ya ujangili kwa namna tutakavyomudu.
Pia katika kuhakikisha tuzo za mwaka huu zinakuwa bora kwa maslahi ya wanamichezo wote hapa nchini, kamati imeteua baadhi ya viongozi wa kiserikali kuwa washauri wa kamati katika masuala mbalimbali na sasa tunasubiri majibu yao ili tuweze kuwatangaza rasmi.
Nawasilisha.
Rehure Nyaulawa
Mwenyekiti Kamati ya Tuzo
26/03/2014
0713 985907

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI