Na Princess Asia, Lubumbashi
WASHAMBULIAJI wawili wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu leo wanatarajiwa kuiongoza klabu yao, TP Mazembe katika mchezo wa kuwania kutinga Nane Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakapoikaribisha Sewe Sport ya Ivory Coast Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, DRC.
Samatta au ‘Sama Goal’ aliifungia bao muhimu la ugenini Jumapili iliyopita Mazembe ikifungwa 2-1 mjini Abidjan na leo wakiwa nyumbani watahitaji japo ushindi wa 1-0 ili kusonga mbele.
Mtu muhimu, bao muhimu; Mbwana Samatta aliifungia bao la ugenini TP Mazembe ikifungwa 2-1 na leo itahitaji ushindi wa 1-0 kusonga mbele |
Kumbuka mwaka jana Mazembe ilitolewa katika hatua hii ya 16 Bora na Orlando Pirates ya Afrika Kusini iliyofika hadi fainali na kufungwa na Al Ahly ya Misri.
Mazembe iliangukia kwenye Kombe la Shirikisho ambako pia ilifika fainali na kufungwa na CS Sfaxien ya Tunisia.
Timu hiyo ya Moise Katumbi safari hii imepania kurudi kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na imejiandaa kiasi cha kutosha kujaribu kufuzu mtihani huo mgumu. Kila la heri Samatta na Ulimwengu pamoja na TP Mazembe.
Mechi nyingine za leo ni kati ya mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri dhidi ya Ahly Benghazi ya Libya itakayochezwa mjini Cairo, CS Sfaxien ya Tunisia itakayokuwa mwenyeji wa Horoya ya Guinea, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini itaikaribisha AS Vita ya DRC.
Michuano hiyo itaendelea kesho wakati Zamalek ya Misri itakapokuwa mwenyeji wa Nkana ya Zambia, Coton Sport ya Cameroon na ES Setif ya Algeria, Esperance ya Tunisia na AS Bamako ya Mali, Al-Hilal ya Sudan na AC Leopards ya Kongo.
Chanzo: Bin Zubeiry
0 comments:
Post a Comment