MWENYEKITI wa ushirika ‘’Nia njema’ wa wasioona uliopo Mtambile Mkoani Pemba, Ali Hemed Khalifa, akimuuzia moja kati ya wateja wao Shemsia Khamis Zubeir, zulia lililotengenezwa kwa usumba, ambapo zulia moja ni shilingi 15,000/= (picha na mpiga picha wetu, Pemba)
MWENYEKITI wa ushirika wa ‘Nia njema’ wa wasioona uliopo Mtambile Mkoani Pemba, Ali Hemed Khalifa, akiwa na wanaushirika wenzake ambao wanajishughulisha na utengenezaji wa mazulia na madometi yanayotokana na usumba, wakiwa katika kazi hiyo huko Mtambile, ambapo Dometi moja huuzwa shilingi 18,000/= na zulia ni shilingi 15,000/= hadi shilingi 15,000/= (picha na mpiga picha wetu, Pemba)
Na mwandishi wetu - PEMBA
‘’SISI macho yetu ni vidole, na ndio vinavyotulisha siku zote...’’,
Ni neno la mwanzo la Mwenyekiti wa ushirika huo wa wasioona wa ‘’Nia njema’’uliopo Mtambile Mkoani Pemba, Ali Hemed Khalifa.
Nikiwa na Mwenyekiti wa ushirika huo na wanachama wake wawili, sikupata picha kamili, kuwaona wasioona wakitengeneza Madometi na Mazulia.
Macho juu na wakati mwengine akielekeza kichwa na sehemu ya kiwili wili chake upande mwengine, lakini mkono wao wenye vidole kumi, ndio macho ya kuzipanga kamba za usumba.
Hapo ni mazungumzo kwenda mbele, huku wao wakiendesha kazi zao za kushona bidhaa hizo zinazotokana na usumba, na kisha mkono wao kwenda kinywani.
Jamani Muungu haachi mjawe, aso hili ana lile, lakini nikasema hupati kile ukakosa mwendo,,,,,,,niliyasema haya kwenye moyo wangu huku machozi ya furaha yakimwagika.
Kalamu yangu ya kuandikia makala hii, wakati mwengine nilikuwa nikiisahau, kutokana na umahiri na ujuzi wa hali ya juu, uliokuwa ukifanywa na wanushirika huo.
Ali Hemed Khalifa, ndie Mwenyekiti na ndie muanzilishi wa ushirika huo wa wasioona, ambae yeye alionekana kuwa na mengi yanayohusu ushirika wao pamoja na wasioona wanavyoweza kuleta mabadiliko.
Alinihadithia kuwa ushirika wao, ambao haujapatapo ufadhili ulianza rasmi mwaka 2001, kwa mafunzo ya awali yaliofanyika Unguja juu ya kutengeneza mazulia na madometi ya usumba.
Ali Hemed alienda huko kama yeye na kurudi ndioa akaona kumbe hakuna mlemavu anaeshindwa na kijio chake kama atapata mafunzo kutokana na mazingira yake.
‘Kumbe mlemvu kuwa omba omba si jambo la lazima kama wanavyofanya wengine, bali kama atafundishwa na kuweza kuyatala mazingira yake anaweza kujiletea maendeleo’’,alisema huku akiendelea na kazi ya kutengeneza dometi.
Baada ya yeye kufanyaka kazi hiyo akiwa peke yake, ndipo alipoaanza safari ya kusaka wasioona wenzake mmoja baada ya mwengine kwa kila eneo analoishi mwanachama wa Jumuia ya Wasioona Zanzibar Wilaya ya Mkoani (ZANAB).
‘’Unamuona huyo mwanachama wangu Mkasi, alikuwa hajawahi kutoka nje tokea azaliwe, na nipofika kwa wazazi wake shughuli ilikuwepo maana walikuwa hawataki kumtoa’’, alisema.
Juhudi kubwa ilifanyika, hadi mwanachama huyo kuweza kuingia kwenye ushirika huu, na wazazi wake kuridhia ingawa kwa hapo awali ni kwa ushingo upande.
Mwaka 2004, kwa mujibu Mwenyekiti huyo alisema sasa ushirika huo ukatimia ukiwa na wanachama sita wote wakiwa wasioona, ingawa baadhi yao wenye uoni hafifu na wengine kiza kabisa.
‘’Sitaisahau semina moja ya TASAF, ambayo hii ndio hasa iliotutoa sisi na ushirika huu, kutambulika maana kama kawaida yangu niliyachukua Madomet na Mazulia na yakanunuliwa huko’’,alifafanua.
Miaka nenda, miaka rudi ushirika huo ambao ulikumbwa na changamoto kadhaa kuliko faida, uliendelea kwa kuchangishana fedha, na kujinunulia malighafi ya usumba.
Mwaka 2010, hapo pia wanachama hao sita walichangishana fedha tena kila mmoja shilingi 5,000/=, ingawa baadhi yao walikuwa wagumu kutoa wakidhani wanataka kuibiwa.
‘’Wengine walikuwa wangumu kutoa fedha, maana si unajua dunia imejaa wajanja na hata wao walikuwa wagumu ,lakini baadae walikubali na kupata fedha za kununulia malighafi’’, alisema huku akiendelea kutengeneza Dometi.
Mwenyekiti huyo alizidi kunipa maajabu kuwa, katika ushirika wao, wanatengeneza mazulia na madometi ya aina mbili kuu, ikiwa ni pamoja na madogo na makubwa.
Dometi moja kutokana na nafasi yao baada ya kukamilisha vifaa vyote hulitengeneza kati ya siku mbili hadi tatu, ambapo moja huliuza kati ya shilingi 18,000/= na shilingi 15,000/=.
Mwenyekiti huyo alilalamikia kutupwa na Serikali licha ya kuwepo kwa Idara maaluma ya watu wenye ulemavu, wakiwemo wao wasioona katika kijiji hicho cha Mtambile.
‘’Tulikuwa tukipigiwa kelele wee,,,, anzisheni vikundi ,,,,,,anzisheni sacos lakini tokea siku tulioanzisha hadi leo, hatujapatiwa uafadhili wowote tupo tu kingu nguvu’nguvu’,alieleza kwa masikitiko.
Pamoja na uhaba wa mtaji, lakini kwa sasa tayari wanachama wote wa ushirika huo, wameshapata uelewa wa kutengeneza madometi na mazulia ambapo pia hujipatia fedha ndogo ndogo ya sabuni.
Mkasi, vipi kuhusu hali ya kipato, ukilinganisha na wakati wote ulipokuwa umewekwa ndani na wazazi,,,, nilimuuliza mwanachama huyo na kusema ‘’hamna hamna ndio muliwamo.
Mkasi ambae alikuwa amewekwa ndani kwa muda wa miaka zaidi ya 20, na wazazi hadi hapo alipokwenda Mwenyekiti wake, kwa sasa anajisikia faraja.
‘’Mimi nilijua kutokana na ulemavu wangu wa uoni, siwezi kufanya lolote, lakini kwa sasa naweza kufanya makubwa, maana hata sabuni yangu hainipigi chenga’’,alisema wakati akitengeneza zulia.
Mwanachama huyo wa ushirika wa ‘Nia njema’ uliopo Mtambile, alitamka kuwa huu sio wakati wa walemavu kuwekwa ndani, na badala yake watolewe nje ili wafanyekazi.
Baada ya kufika ndani ya ushirika huo, pia ameweza kujiari mwenyewe, kwa kuanzisha mpango wa kujishonea mikoba, makawa na mikeka jambo ambalo hapo awali hakulitarajia.
‘’Kwa kweli ushirika huu, umeniwezesha kuyatawala mazingira yangu, na hata kujidai kwa kupata walau sabuni yangu, na hata kusaidia wenzangu, lakini nayo Serikali ituone’’,alisema.
Nae mwanachama Riziki Juma Omar, alisema kama iwapo ushirika wao utasaidiwa na wafadhili unaweza kupiga hatua, na wasiiona katika ukanda huo wa Mtambile kuondokana na utegemezi.
Kubwa zaidi wanachama wa ushirika huo pomoja na kulilia mtaji, lakini pia wamepaza sauti zao juu, kutaka kupatiwa mafunzo zaidi ya kazi yao hiyo ili waingie katika soko la ushindani.
Mwenyekiti wa ushiriki huo Ali Hemed Khalifa, alirudi tena na kusema suala la soko sio tatizo kubwa sana, hasa baada ya ujio wa soko la Jumapili, lakini changamoto kubwa kwa sasa ni malighafi.
‘Utaamini kuwa baadhi ya siku inanibidi mimi nisafiri hadi Bumbwini au Kakazini Pemba, kuyafuata makumbi au kamba, sasa angaalia safari hizo kisha uliuze shilingi ngapi zulia ili upate faida’’,alisema.
‘’Soka la jumapili lipo, lakini ugumu wetu kwa sasa ni upatikanaji wa malighafi (makumbi), yamekuwa adimu na mali, sasa na hata ukiamua kununua kamba ni ghali mno’’,alifafanua.
Ushirika huo wa utengenezaji wa Madometi na Mazulia ya kamba za umba una malengo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanachama wasioona.
Hata hivyo wanachama hao wametoa wito kwa wazazi na walezi, kuacha tabia ya kuwafungia ndani watu wenye ulemavu, kwani wakiwezeshwa kwa mujibu mazingira yao wanaweza kuleta mabadiliko.
Pia wakaikumbusha Serikali kuhakikisha wanawatupia macho, ili uweze kujikongoja na kufikia malengo yaliojipangia, ikiwa ni pamoja na kukuza pato lao.
Ushirika huu ambao hadi sasa, haujafanya usajili rasmi, unajiendesha kwa nguvu za wanachama na wamekuwa na utaribu wa kugawana shilingi 20,000/- baada ya kuuza mazulia na fedha nyengine kununua maliaghafi.
Idara ya watu wenye ulemavu, Umoja wa Watu wenye ulemavu na Jumuia ya wasioona Zanzibar, hapa ndio pakuanzia kwa kuvipa mitaji vikundi kama hivi ili visonge mbele.
0 comments:
Post a Comment