Tuesday, August 18, 2015

LOWASSA ADAI CCM ITAPATA LAANA KUBWA KWA WALICHOMFANYIA MZEE KINGUNGE BILA YA HURUMA...

SIKU mbili baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kumvua Ukamanda Mkuu, mwanasiasa mkongwe nchini, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, uamuzi huo umepokewa tofauti na mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Edward Lowassa.

Tamko la UVCCM ambalo lilitolewa na Katibu Mkuu wa umoja huo,Sixtus Mapunda, lilisema wamefikia uamuzi huo kutokana na tabia, mwenendo wa Mzee Kingunge aliounesha hivi karibuni tofauti na maadili pamoja na taratibu za CCM.

Umoja huo ulipendekeza vikao vya CCM, kuuangangalia upya uanachama wake na kuchukua hatua kubwa zaidi.

Bw. Lowassa ambaye pia ni mgombea urais anayeviwakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), alisema CCM itapata laana kama itaridhia kuondolewa kwa Mzee Kingunge.

Akiwahutubia mamia ya wafuasi wa UKAWA katika Viwanja vya Kibandamaiti, Mjini Zanzibar, jana ambako alikwenda kutambulishwa na kutafuta wadhamini, Bw. Lowassa alisema Mzee Kingunge ni mmoja kati ya wazee muhimu ndani ya CCM.

"Nasikitika sana kwa hatua kali alizochukuliwa Mzee Kingunge, kama isingekuwa yeye, CCM isingefika hapo ilipo, watapata laana," alisema.

Mapokezi yake
Lowassa aliwasili Zanzibar jana asubuhi akitokea jijini Mwanza kwandege ya kukodi akiwa na viongozi wengine wa UKAWA pamoja na mgombea mwenza, Bw. Juma Duni Haji.

Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, msafara huo ulipokewa na Katibu Mkuu wa CUF Taifa ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Akihutubia mkutano huo, Lowassa aliwaambia Wazanzibar kuwa atahakikisha anazingatia taratibu za kisheria ili Masheikh wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu (Uamsho) wanaoshikiliwa katika mahabusu jijini Dar es Salaam, wanapata haki zao.

Ahadi hiyo ya Lowassa ilisababisha umati huo kulipuka kwa furaha na vifijo huku ukimuita `Rais, Rais, Rais.

Alisema kwa mara zote alizokwenda Zanzibar, hajawahi kushuhudia umati mkubwa kama aliouona jana.

Lowassa alisema amekwenda Zanzibar kuomba dhamana ya wananchi na kurudia kauli yake kwamba anawania urais kwa kuwa anauchukia umaskini.

“Nataka kuwahakikishia Watanzania popote kwamba mabadiliko yataletwa na vyama vya upinzani. Nimetembea sehemu mbalimbali nimeona wananchi wanataka mabadadiliko ya uongozi,” alisema.

Kuhusu Katiba, alisema yeye ni muumini wa Serikali Tatu zitakazosaidia kuimarisha Muungano na kwamba msimamo wake huo aliouonyesha tangu miaka ya 90 wakati wa harakati za kundi la G55.

Alisema suala hilo litafafanuliwa vizuri wakati wa uzinduzi wa ilani ya uchaguzi Jumamosi wiki hii na wakati wa kampeni.

Hata hivyo, Lowassa alisema njia ya kuiondoa CCM madarakani, ni kwa kupiga kura na wananchi wajiandae pia kulinda kura.

Masheikh  waliofungwa

Alisema Masheikh mkoani Mwanza walimwomba azungumzie jambo hilo na kwamba atakachofanya atakapoingia madarakani, atazingatia taratibu za kisheria kufuatilia stahili zao.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI